1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
23 Agosti 2019

Yaliyoandikwa na magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika mnamo wiki hii ni pamoja na makubaliano yaliyofikiwa nchini Sudan kati ya wapinzani na wanajeshi.

https://p.dw.com/p/3OMpI
Kombobild - Sudan | Machtabgabe Militär - Algerien | Freitagsdemo

die tageszeitung

Baada ya utawala wa dikteta Omar Bashir kuangushwa limeundwa baraza la wajumbe 11 la wanajeshi na wawakilishi wa upinzani litakaloiongoza Sudan. Mhariri anauliza lakini jee ni  kweli kwamba wanajeshi hao watakuwa tayari kusamehe marupurupu yao? Gazeti linasema kuundwa kwa baraza hilo ni hatua muhimu sana katika historia ya Sudan. Jambo la kutilia maanani ni kwamba watu wa Sudan wamechukua hatua ya kuepusha umwagikaji damu kwa kuunda baraza hilo la wanajeshi saba na raia sita ikiwa pamoja na mwanamke mmoja.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa, uenyekiti wa baraza utakuwa chini ya wanajeshi kwa muda wa miezi 21 na baada ya hapo baraza hilo la mpito litaongozwa na raia. Hata hivyo gazeti la die tageszeitung linafahamisha kwamba kabla ya kulifikia lengo la kufanyika uchaguzi wa kidemokrasia, zitakuwapo changamoto kubwa ikiwa pamoja na hali mbaya ya kiuchumi inayoikabili Sudan.

Süddeutsche 

Gazeti la Süddeutsche wiki hii limeandika juu ya wito wa nchi za Afrika wa kutaka Zimbabwe iondolewe vikwazo. Gazeti hilo linasema viongozi wa nchi na wakuu wa serikali wa nchi za jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika, SADC wametaka, kuondolewa kwa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Zimbabwe vikwazo hivyo vimewekwa na Uingereza, Marekani pamoja na Umoja na Ulaya.

Viongozi hao wa Afrika wamesema vikwazo hivyo vya kiuchumi vinapaswa kuondolewa ili kuiwezesha Zimbabwe ijiletee maendeleo. Wametilia maanani kwamba hali ya kisiasa nchini humo imezidi kuwa ya mvutano baada ya kufanyika maandamano mengine hivi karibuni. Viongozi wa Afrika pia wamesisitiza kwamba vikwazo viliyvowekwa dhidi ya Zimbabwe vinaziathiri nchi zote za kanda ya kusini mwa Afrika.

Die Welt

Nalo gazeti la Die Welt limeandika juu ya mwandishi habari Eric Kabendera wa Tanzania anayeripoti pia kwa ajili ya vyombo vya habari vya kimataifa kama vile gazeti la Guardian la Uingeretza. Gazeti la Die Welt  linatueleza kwamba Kabendera alichukuliwa kutoka nyumbani kwake, jijini Dar es salaam, na watu waliojifanya kuwa polisi tarehe 29  mwezi Julai. Watu hao walitwaa simu yake, ya mkewe na ya jirani aliyekuwa anapiga picha tukio la kuchukuliwa kwa mwandishi huyo.

Wakili wa Kabendera alikwenda kumtafuta kwenye kituo cha polisi ambako watu waliomchukua kwa nguvu kutoka nyumbani kwake, walidai kumpeleka lakini kwenye kituo hicho hakuna aliyejua juu ya kukamatwa kwa mwandishi huyo. Gazeti la Die Welt linaeleza kuwa Kabendera aliwahi kuandika makala juu ya mvutano wa kisiasa nchini Tanzania na kudai kuwepo njama za kuzuia kuchaguliwa tena kwa Rais John Magufuli kwa sababu ya kuzidi kuwakandamiza watu wake na vyombo vya habari.

Gazeti la Die Welt linaongeza kusema kwamba baada ya mashirika ya kutetea haki za binadamu na vyombo vya habari vya kimataifa kuandika juu ya kukamatwa kwa mwandishi huyo Eric Kabendera, polisi ilitoa taarifa kwamba mwandishi huyo alikamatwa ili kuhojiwa juu ya uraia wake.Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya nchini Tanzania Eric Kabendera alikamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kutakatisha fedha na kukwepa kulipa kodi.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine limendika juu ya Rais wa Rwanda Paul Kagame. Linasema katika makala yake kuwa Rais huyo anapewa sifa sana. Lakini linauliza, Jee sifa hizo ni za kweli?   Gazeti hilo linaeleza kuwa Rais Kagame ni mtu mwenye pande nyingi. Katika upande mmoja yeye ni mwanamageuzi mkubwa kiuchumi. Na ukweli ni kwamba tangu aingie madarakani mnamo mwaka 2000 uchumi wa Rwanda umekuwa unastawi mtindo mmoja. Idadi ya vifo vya watoto imepungua na umasikini pia umepungua na kutokana na mafanikio hayo Benki ya Dunia imeacha mfuko wake wazi kwa Rwanda. Tangu mwaka 1994 nchi hiyo imepatiwa jumla ya dola bilioni 4 na benki hiyo.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema mpaka sasa mafanikio ya kiuchumi yameilinda hadhi ya Kagame lakini gazeti hilo limenukuu taarifa ya gazeti la masuala ya kiuchumi "Financial Times la Uingereza, linalodai kuwa takwimu juu ya uchumi wa Rwanda si sahihi. Kwa mujibu wa gazeti hilo la Financial Times, mafanikio ya kiuchumi nchini Rwanda ni ya chini kuliko inavyoripotiwa! Yaani taarifa juu ya maendeleo ya uchumi zimefinyangwa. Umasikini haujapungua bali umeongezeka kwa asilimia 6.6 na gharama za maisha zimeongezeka kwa asilimia takriban 30. Rais Kagame amesema taarifa ya gazeti hilo la Financial Times ni propaganda ya vyombo vya habari vya nchi za magharibi.

Badische 

Gazeti la Badische linatupasha habari juu ya msaada unaotolewa na asasi ya Ujerumani inayoitwa "Fair Aid” kwa watoto wa nchini Kenya. Jee hiyo ni asasi ya aina gani na inafanya nini? Mpaka sasa asasi hiyo iliyoko katika mji wa Rheinfelden kusini mwa Ujerumani imeshawasaidia watoto wengi wa Kenya.

Asasi hiyo inashirikiana na shirika la misaada la Kenya linaloitwa "Choice for Life”. Tangu kuanzishwa kwake miaka 13 iliyopita asasi hiyo ya Ujerumani imeshawasaidia watoto180 wa Kenya na hasa wale waliogeuka kuwa yatima baada ya wazazi wao kufariki dunia kutokana na maradhi ya UKIMWI. Gazeti la Badische linatufahamisha kwamba asasi hiyo ya misaada ya Ujerumani inawalipia watoto ada, inagawa sare za shule na pia inagharamia chakula na matibabu ya watoto. Miongoni mwa watoto hao ni wale ambao sasa wako katika vyuo vya elimu ya juu.

Vanyzo:/Deutsche Zeitungen