1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
5 Septemba 2019

Yaliyozingatiwa kwenye magazeti ya Ujerumani kuhusu bara la Afrika wiki hii ni pamoja na msaada wa fedha utakaotolewa na Ujerumani ili kuisaidia Namibia na kushambuliwa raia wa kigeni nchini Afrika Kusini.

https://p.dw.com/p/3P3QU
Namibia Bundesentwicklungsminister Gerd Müller in Windhoek
Picha: Imago Images/photothek/U. Grabowsky

Frankfurter Allgemenine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine limeandika juu ya msaada wa fedha utakaotolewa na Ujerumani ili kuisaidia Namibia kukabiliana na athari za ukame ulioikumba nchi hiyo kwa miaka kadhaa sasa. Ahadi hiyo ilmetolewa na waziri wa maendeleo wa Ujerumani Gerd Müller alipofanya ziara nchini Namibia.

Gazeti la Frankfurter Allgemeina linaeleza kwamba Ujerumani itatoa kiasi cha Euro Milioni 10 kwa Namibia kuisaidia nchi hiyo kupambana na athari za ukame. Akizungumzia juu ya msaada huo waziri wa maendeleo wa Ujerumani Gerd Müller amesema Namibia imekumbwa na ukame uliosababishwa na madibilidiko ya hali ya hewa. Fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kununulia mbegu na kuchimba visima. Pia zitatumika kwa ajili ya kuendeleza mbinu za kilimo za kisasa. Katika ziara yake nchini Namibia waziri Gerd Müller pia alizungumzia juu ya suala la fidia kwa watu wa nchi hiyo waliotendewa uhalifu na wakoloni wa kijerumani.

Ujerumani iliitawala Namibia kuanzia mwaka 1884 hadi mwaka 1915. Gazeti la Frankfurter Allgemeine limemnukulu waziri wa Müller akisema. Kwa muda mrefu uhalifu uliotendwa na wakoloni wa kijerumani nchini Namibia umepuuzwa. Kwa muda mrefu Ujerumani imenyamaza kimya juu ya uhalifu huo. Waziri Müller amesema kuizingatia historia juu ya yaliyotokea nchini Namibia wakati wa ukoloni wa kijerumani, kutaweka msingi wa mustakabali wa pamoja baina ya Ujerumani na Namibia.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung limeandika juu ya habari za kusikitisha. Nchini Afrika Kusini kwa mara nyingine tena raia kutoka nchi nyingine za Afrika wameshambuliwa na magenge ya watu wanaochukia wageni. Ghasia hizo ziliwalenga hasa watu kutoka Nigeria. Na nchini Nigeria watu walifanya ghasia za kulipiza kisasi. 

Katika mji wa Ibadan kusini magharibi mwa Nigeria watu waliokuwa na ghadhabu walichoma moto kumpuni ya simu ya Afrika Kusini. Na kabla ya hapo watu wengine walishambulia duka kubwa la Afrika Kusini la Shoprite katika mji huo wa Ibadan. Wiki iliyopita magenge ya watu wanaochukia wageni nchini Afrika Kusini, walifanya ghasia za kuvamia maduka na kupora mali. Watu watano walikufa kutokana na ghasia hizo. Rais Muhammadu Buhari amesema atamtuma mjumbe maalumu nchini Afrika Kusini na huenda yeye mwenyewe akafanya ziara mwezi ujao.

Süddeutshce

Nalo gazeti la Süddeutsche limeandika juu ya ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas nchini Sudan. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba waziri Maas amefanya ziara hiyo muda mfupi tu baada ya kuundwa baraza la mpito nchini humo. Katika ziara hiyo waziri wa mambo ya nje Maas alikutana na viongozi wa baraza hilo la mpito, na kujadili misaada ya maendeleo. Waziri huyo aliahidi msaada wa fedha zaidi, mbali na dola Milioni 11 ambazo Ujerumani imeshaipa Sudan. Waziri Maas pia amejadili na wenyeji wake, uwezekano wa kuanzisha tena misaada ya maendeleo iliyosimamishwa hapo awali, kutokana na utawala wa rais Omar al Bashir.

Gazeti la Süddeutsche pia linatilia maanani kwamba bwana Heiko Maas ni waziri wa mambo ya nje wa kwanza, kutoka nchi ya Ulaya, kufanya ziara nchini Sudan, mara tu baada ya Omar al -Bashir kuondolewa madarakani.

Neue Zürcher 

Na gazeti la Neue Zürcher linatupeleka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na linazungumzia juu ya kutatizika kwa juhudi za kupambana na maradhi ya Ebola katika nchi hiyo. Linauliza iwapo hatua zilizochukuliwa zilikuwa sahihi, kwa sababu watu zaidi ya 2000  wameshakufa nchini  humo tangu kulipuka kwa maambukizi mwaka mmoja uliopita na linasema maambukizi bado yanaendelea kuenea. Sababu ni kwamba mashirika ya kimataifa yanayotoa misaada bado hayajaweza kujenga imani miongoni mwa wananchi wa Kongo.

Gazeti la Neue Zürcher linaeleza kwamba nusu ya watu waliokumbwa na homa ya Ebola wamekufa kwa sababu watu hao hawakupelekwa kwenye vituo maalumu vya matibabu. Watu hao waliamua kuugulia majumbani mwao. Maradhi ya Ebola yameenea katika sehemu yenye mapigano.

Vita vimetanda kwa miaka zaidi ya 25. Baadhi ya wagonjwa hawatoki nje ya nyumba zao kwa sababu ya kuhofia magenge ya  waasi, na siyo kwa sababu ya imani za kishirikina kama inavyoenezwa. Magenge ya waasi yanajificha milimani na misituni ili kuwashambulia wananchi. Watu hawana imani kubwa na majeshi ya usalama ya nchi yao.

Vyanzo/Deutsche Zeitungen