1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
7 Mei 2021

Yaliyoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika wiki hii ni pamoja na uhusiano wa Rais wa Chad aliyeaga dunia Idriss Deby, Changamoto za nchi za Afrika katika kutafuta chanjo dhidi ya corona na mengineyo.

https://p.dw.com/p/3t5F9
Tschad Präsident Idriss Deby
Picha: Guillaume Horcajuelo/POOL/AFP/Getty Images

Die Welt

Na tunaanza na makala ya gazeti la Die Welt juu ya kifo cha aliyekuwa rais wa Chad Idriss Deby. Gazeti hilo linazungumzia uhusiano wake na nchi za magharibi. Linasema madikteta kama Deby wanaungwa mkono na nchi za magharibi mradi tu madikteta hao wanafanya kazi ya kupambana na magaidi.

Hata hivyo gazeti la Die Welt linauliza jee nchi za magharibi sasa zitayaweka mbele malengo gani baada ya kifo cha Deby? Gazeti hilo linatilia maanani kwamba rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alikuwa kiongozi pekee wa Ulaya aliyehudhuria mazishi ya Deby nchini Chad.

Gazeti linasema inaeleweka Ufaransa inataka kuona utulivu katika makoloni yake ya zamani, inajiweka mbali  na malengo ya waasi na wanaharakati wa kiraia wanaopigania haki za binadamu. Kwa nchi za magharibi  chaguo ni kati ya kushirikiana na madikteta wanaoelewana nao au hatari ya kuwapa fursa waasi na makundi ya kigaidi.

Frankfurter Allgemeine

 Gazeti la Frankfurter Allgemeine linatupia macho juhudi na changamoto za nchi za Afrika katika kutafuta chanjo dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona. Na kwa ajili hiyo limezungumza na wadau wa sekta hiyo ya afya miongoni mwao mjumbe wa bodi ya kampuni ya chanjo ya Biovac ya nchini Afrika Kusini, Morena Makhoana ambaye ameliambia gazeti la Frankfurter Allgemeine kwamba nchi za Afrika zinapaswa kujitegemea zenyewe katika juhudi za kupata chanjo.

Mwenyekiti huyo wa bodi ya kampuni ya hiyo ya Afrika Kusini amesema sasa pana ari kubwa miongoni mwa nchi za Afrika ya kutaka kujikidhi zenyewe katika mahitaji ya chanjo na hasa baada ya India kusimamisha uuzaji wa dawa hizo nje ya nchi.

Makhoana ameeleza kuwa sekta ya kutengeneza chanjo haikuwa ya kuvutia mnamo miaka 90 na ndio sababu Afrika ilirudi nyuma katika sekta hiyo na badala yake ilitegemea chanjo kutoka kwa mashirika ya kimataifa. Bwana Makhoana, ameeleza kwamba kampuni ya Biovac ilisema ilikuwa na uwezo wa kutengeneza chanjo za corona kati ya milioni 20 na 30 lakini kwa sasa haina nyenzo za kutosha. Mjumbe huyo wa bodi ya kampuni ya Biovac ya nchini Afrika Kusini amesema Afrika lazima itengeneze chanjo dhidi ya magonjwa ya kuambukiza lakini itaweza kufanya hivyo ikiwa haitajiweka nyuma na kukubali kubandika vizibo katika hatua za mwisho za uzalishaji.

die tageszeitung

Gazeti la die tagezeitung linazungumzia juu ya hatua ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ya kutangaza hali ya hatari kwenye majimbo mawili ya mashariki mwa nchi hiyo. Gazeti hilo linaeleza kuwa  hatua hiyo ilichukuliwa baada ya maafisa wa usalama kutumia mabavu katika kuwakabili raia waliokuwa  wanaandamana kwa amani katika mji wa Beni.

Gazeti la die tageszeizung linaarifu kwamba wanafunzi wapatao 500 walijenga kambi mbele ya manispaa ya  mji wa Beni kwa muda wa siku kadhaa. Die tageszetiung linaeleza kuwa lengo la wanafunzi hao lilikuwa kupinga mauaji yanayofanywa na waasi mashariki mwa Kongo wakati majeshi ya Umoja wa Mataifa hayachukui hazua yoyote.

Wanafunzi hao walimtaka rais wao Felix Tshisekedi aende mashariki ya Kongo ili kukomesha mauaji. Gazeti la die tageszeitung linasema badala ya kwenda huko, rais Tshisekedi aliamua kutangaza hali ya hatari katika  majimbo mawili ya mashariki mwa Kongo. Gazeti hilo limeeleza kuwa serikali ya kongo ilichukua hatua hiyo  kali kwa sababu wanafunzi walitumiwa na wanasiasa kufanya maandamano.

Der Tagesspiegel

Gazeti la der Tagesspiegel linakamilisha makala yetu kwa kutupa taarifa juu ya kaburi la mtoto aliyezikwa  miaka 78,000 iliyopita kwenye sehemu inayoitwa Panga ya Saidi katika kaunti ya Kilifi, kwenye mkoa wa Pwani nchini Kenya. Sehemu hiyo ya pango ina historia ndefu ya tangu enzi za mawe.

Gazeti la der Tagesspiegel linasema kuvumbuliwa kwa mabaki ya mtoto huyo kunathibitisha maendeleo katika mfumo wa kijamii wa  wakati huo. Mabaki ya mtoto huyo yalichimbuliwa na wanasayansi wa historia ya binadamu.

Wanasayansi walioshiriki katika mradi huo,walikuwa pamoja na wa taasisi ya Max Plank ya Ujerumani inayoshughulikia historia ya binadamu. Wanatuhumu kwamba uvumbuzi wa mabaki ya mtoto huyo aliekuwa na umri wa miaka mitatu unaonyesha ustaarabu wa mazishi wa watu wa kusini mashariki mwa Kenya tangu enzi za kale.

Naam hadi hapo tunayakamilisha makala haya ya Afrika katika magazeti ya Ujerumani. Asante kwa kuwa  nami. Mimi ni ZA kutoka DW Bonn. nakuaga kwaheri.

Vyanzo:/Deutsche Zeitungen