1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AIRBUS lapanga kufuta nafasi elfu kumi za kazi barani Ulaya

Oummilkheir1 Machi 2007

Wafanaykazi wa AIRBUS wapania kupinga hatua za kufunga -mkaja "Power 8"

https://p.dw.com/p/CHJB
Mwenyekiti Louis Gallois
Mwenyekiti Louis GalloisPicha: AP

Watumishi wa viwanda kadhaa vya Airbus barani Ulaya wamesita kufanya kazi tangu jana,wakilalamika dhidi ya mpango wa kulifanyia marekebisho kampuni hilo kubwa la kutengeneza ndege barani Ulaya.Mpango huo wa kufunga mkaja kwa jina “Power nambari nane” utagharimu nafasi za kazi elfu kumi,nyingi kati ya hizo nchini Ufaransa na Ujerumani.

Nafasi elfu kumi za kazi kampuni la AIRBUS linapanga kuzifuta katika kipindi cha miaka ijayo,nusu ya hizo ni za wafanyakazi wa reja reja au wa walioajiriwa kutoka mashirika mengine.Hakuna mfanyakazi mwenye mkataba wa kudumu atakaeachishwa kazi lakini.Huo ndio ujumbe mkuu uliotolewa jana na mwenyekiti wa AIRBUS LOUIS GALLOIS mjini Toulouse.Mwenyekiti wa AIRBUS ameendelea kusema:

“Nnasikia kila kwa mara toka vyombo vya habari,eti kutengenezwa dege kubwa kabisa AIRBUS chapa A 380 ndio sababu ya kutia njiani mpango wa Power nambari nane.Hasha.Ukweli ni kwamba tunabidi kukabiliana na kishindo kilichosababishwa na kudhoofika sarafu ya Dollar.Tangu tulipoanza kuratibu mpango wa kutengeneza dege hilo la chapa A 380-nguvu za AIRBus za kushindana kibiashara ulimwenguni zimepungua kwa asili mia 20-kwasababu ya kuporomoka thamani sarafu ya Dollar.”

Louis Gallois amethibitisha mzigo na faida zitakazotokana na mpango huo wa kufanyiwa marekebisho kampuni la AIRBUS zitagawanywa kati ya nchi zote nne shirika.Nafasi 3700 za kazi zitafutwa katika viwanda vya Ujerumani.Uengereza itapoteza nafasi za kazi 1600 na Hispania nafasi 400.Nafasi nyingi zaidi za kazi zitapotea nchini Ufaransa ambako watu 4300 watajikuta bila ya ajira.

AIRBUS linatafuta wateja watakaogharimia teknolojia mpya katika viwanda vitatu Nordenham nchini Ujerumani,Méaulte cha Ufaransa na Filton cha Uengereza.Viwanda vitatu vyengine,Varel na Laupheim vya Ujerumani na St-Nazaire cha Ufaransa, mwenyekiti wa kampuni la AIRBUS Louis Gallois anafikiria kuviuza kabisa.

Mabaraza yanayowakilisha masihali ya waajiriwa yanapinga mpango huo wa marekebisho.Maandamano yameripotiwa kuzuka tangu jana katika kiwanda cha Méaulte nchini Ufaransa.

Tulijua kama mpango wao utakua na madhara,lakini haya yamepindukia-ni hasara ambayo haiwezi kukubalika.Ni uchokozi huu”” amesema Eric Moyen mjumbe wa vyama vya wafanyakazi wa AIRBUS CFTC.

Mjini Méaulte,wafaanyakazi 600 wa kiwanda cha Saint Nazaire walikusanyika wakilalamika mpango huo Power nambari nane unaipendelea Ujerumani dhidi ya Ufaransa.

Nchini Ujerumani wafanyakazi wa viwanda vinavyokabiliwa na kitisho cha kufungwa au kuuzwa,huko Nordenham,Varel na Laupheim,wamegoma kufanya kazi tangu jana na wanasema mgomo wao utaendelea mpaka kesho.

Uongozi wa AIRBUS unapanga kujadiliana na wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi.Hata katika viwanda ambavyo havijaguswa na mpango huo wa Power nambari nane,marekebisho hayaepukiki.Kiwanda kikuu cha Hambourg siku zijazo kitabidi kijishughulishe zaidi na kutengeneza ndege za Airbus chapa A 320 –za masafa mafupi na masafa ya wastani,huku Ufaransa ikishughulikia ndege za masafa marefu.Ndege kubwa ya Airbus A 380 itakuwa ikichanganywa katika nchi zote hizo mbili.