1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al Bashir kuhojiwa kwa utakatishaji fedha na ugaidi

Oumilkheir Hamidou
3 Mei 2019

Mwendesha mashitaka mkuu wa Sudan ameamua kumhoji Omar al Bashir kwa madai ya kutakatisha fedha na kufadhili ugaidi. Uamuzi huo umepitishwa huku maandamano yakiendelea mjini Khartoum kudai serikali ya kiraia.

https://p.dw.com/p/3HrkD
Sudan Präsident Omar al-Bashir
Picha: Reuters/M. N. Abdalla

Duru kutoka ofisi ya mwendesha mashitaka mkuu zimethibitisha ripoti za vyombo vya habari vya serikali kwamba kaimu mwendesha mashitaka mkuu, jenerali Al Waleed Sayyed Ahmed ameamuru al Bashir ahojiwe kuambatana na "sheria dhidi ya kutakatisha fedha na kugharamia ugaidi."

Marekani imeiondolea Sudan vikwazo  vya kibiashara vilivyodumu miaka 20, Oktoba mwaka 2017, hata hivyo inaendelea kuishikilia katika orodha ya mataifa yanayounga mkono ugaidi wa kimataifa pamoja na Iran, Syria na Korea ya Kaskazini. Sudan iliingizwa katika orodha hiyo kwa sababu ya tuhuma kuwa ina mafungamano pamoja na wanamgambo wa itikadi kali. Muasisi wa mtandao wa kigaidi wa Al Qaida Osama Bin Laden aliishi Sudan kati ya mwaka 1992 na 1996.

Jenerali Abdel Fattah al Burhane anaeongoza baraza la kijeshi la mpito nchini Sudan alisema  ujumbe wa nchi hiyo utakwenda hivi karibuni Washington kuzungumzia namna ya kuitoa Sudan katika orodha ya nchi zinazounga mkono ugaidi.

Waandamani waliokusanyika mbele ya makao makuu ya jeshi mjini Khartum
Waandamani waliokusanyika mbele ya makao makuu ya jeshi mjini KhartumPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Basheer

Raia wanaendelea kuzozana na wanajeshi kuhusu muundo wa baraza la mpito

Wakati huo huo wiki tatu baada ya Omar al Bashir kupinduliwa na wanajeshi, umati wa waandamanaji walijazana katika eneo linaloyazunguka makao makuu ya jeshi mjini Khartoum kwa kile kilichotajwa kuwa "maandamano makubwa ya kudai serikali ya kiraia."

Waandamanaji walikusanyika kwa wingi mkubwa zaidi kupita siku zote nyengine za hivi karibuni, wakijazana katika njia zote na daraja zinazoelekea katika jengo hilo lililoko kati kati ya mji mkuu Khartoum katika wakati ambapo mazungumzo kati ya waandamanaji na watawala wa kijeshi yanaendelea kukwama.

Pande hizo mbili zimekubaliana kuunda baraza la pamoja litakalokuwa na raia na wanajeshi lakini zinazozana juu ya muundo wa baraza hilo. Katika wakati ambapo waandamanaji wanadai raia wadhibiti taasisi huyo, wanajeshi wao wanahoji, kutokana na mivutano iliyoko nchini wanajeshi wanabidi wawe wengi katika baraza hilo la pamoja.

Waandamanaji wamewakabidhi wanajeshi mapendekezo kuhusu muundo wa utawala wa kiraia nchini Sudan. Naibu kiongozi wa baraza la kijeshi Mohammad Hamdan Dagolo amesema baraza lao lina jukumu la kuzungumza.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Gakuba, Daniel