1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al-Shabaab wadai kuishambulia kambi ya AMISOM

Grace Patricia Kabogo15 Januari 2016

Wapiganaji wa kundi la kigaidi la al-Shabaab wameishambulia kambi ya wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika (AMISOM) kusini magharibi mwa Somalia, huku ikiripotiwa kwamba watu kadhaa wameuawa.

https://p.dw.com/p/1He6S
Wapiganaji wa kundi la al-Shabaab nchini Somalia.
Wapiganaji wa kundi la al-Shabaab nchini Somalia.Picha: picture-alliance/AP Photo/AP Photo/F. Abdi Warsameh

Afisa wa jeshi la Somalia, Kanali Idris Ahmed, alisema wapiganaji hao wa al-Shabaab waliishambulia kambi hiyo ya jeshi inayosimamiwa na wanajeshi kutoka Kenya ambao ni sehemu ya kikosi cha Umoja wa Afrika kwenye mji wa El-Adde kwa kutumia gari lililokuwa na mabomu.

Kanali Ahmed alisema milio mikubwa ya risasi ilisikika wakati ambapo wanamgambo hao waliivamia kambi hiyo na wanajeshi kuanza pia kujibizana kwa kurushiana risasi na kwamba mapigano bado yanaendelea.

Wanajeshi wa Somalia na wanajeshi wa Kenya kwenye AMISOM walipelekwa katika kambi hiyo iliyoko kwenye jimbo la Gedo, ambalo linapakana na Kenya na Ethiopia.

Msemaji wa Al-Shabaab, Abdiaziz Abu Musab, alidai kuwa wamewaua wanajeshi 63 wa Kenya katika shambulizi hilo ambalo amesema limefanikiwa, ingawa taarifa hizo bado hazijathibitishwa. Aidha, amesema wanajeshi wa Umoja wa Afrika wameikimbia kambi hiyo.

Abu Musab alitangaza kupitia redio ya kundi hilo ya mtandaoni kwamba wapiganaji wake wa Mujahedeen walifanikiwa kuingia katika kambi hiyo asubuhi ya leo , na kuongeza kuwa wamewaua wanajeshi wengi Wakristo kutoka Kenya.

Moja ya mashambulizi yaliyowahi kufanywa na al-Shabaab mjini Mogadishu.
Moja ya mashambulizi yaliyowahi kufanywa na al-Shabaab mjini Mogadishu.Picha: Reuters/F. Omar

AMISOM yakanusha kambi yake kushambuliwa

Hata hivyo, kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la Kenya, Kanali David Obonyo, iliyoshambuliwa ni kambi jirani ya wanajeshi wa Somalia, huku watu walioshuhudia wakisema watu kadhaa waliuawa. Kiongozi wa kimila, Hussein Adam, amesema alisikia mripuko mkubwa na kufuatiwa na milio mikali ya risasi iliyodumu kwa takriban dakika 45. Amesema hawajui kuna waathirika wangapi, lakini watu walioshuhudia wameona maiti zikiwa zimetapakaa chini.

Septemba mwaka 2015, wapiganaji wa Al-Shabaab walishambulia kambi ya wanajeshi wa Uganda walioko kwenye kikosi cha AMISOM katika wilaya ya Janale, umbali wa kilomita 80 kusini-magharibi mwa Mogadishu kwenye mkoa wa Lower Shabelle. Mwezi Juni Al-Shabaab waliwaua wanajeshi kadhaa wa Burundi baada ya kuivamia kambi ndogo ya AMISOM iliyoko kaskazini-magharibi mwa Mogadishu.

Wapiganaji hao pia wamefanya mashambulizi ya mara kwa mara kwenye mji mkuu, Mogadishu. Hata hivyo, kikosi cha AMISOM chenye wanajeshi 22,000 pia kimefanikiwa kuwashinda al-Shabaab na kuwafurusha kutoka kwenye ngome zao muhimu kusini-magharibi mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Kundi hilo lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaida, pia limefanya mashambulizi kadhaa yaliyosababisha mauaji ya watu wengi ndani ya Kenya kwenyewe.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,APE,RTRE
Mhariri: Daniel Gakuba