1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al Shabaab yatangaza vita zaidi Somalia

30 Julai 2010

Ni kufuati Azimio la Umoja wa Afrika kuongeza majeshi ya kulinda amani

https://p.dw.com/p/OY21
Viongozi wa nchi za kiafrika,wakipiga picha ya pamoja na katika eneo la ziwa Victoria,katika siku ya kwanza ya ufunguzi wa mkutano wa viongozi wa Afrika,jijini Kampala Julai 25,mwaka huu.Picha: AP

Licha ya Umoja wa Afrika kutangaza kuongeza majeshi ya kulinda amani nchini Somalia,kundi la Al Shabaab limetoa kitisho kipya kuwa litaligeuza eneo la Mogadishu kuwa makaburi ya wanajeshi hao,na kuzidi kutishia amani nchini Somalia.

Ikumbukwe kuwa kundi la Al Shabaab ambalo linatajwa kuwa na mafungamano na mtandao wa Al Qaeda,lilitangaza hapo kabla kuhusika katika mashambulio ya mabomu jijini Kampala,na kuwaua raia 76 Julai 11.

Msemaji wa kundi la Al Shabaab Sheikh Ali Mahmoud Rage ameuonya umoja wa Afrika,ambao hadi sasa una vikosi vya wanajeshi 6,000 kutoka nchi za Uganda na Burundi kuwa uamuzi wa kupeleka majeshi zaidi nchini humo,ni sawa na kujitangazia vita vitakatifu baina yao.

Ameongeza kuwa majeshi yatakayoongezwa nchini humo,hayatakuwa na uwezo na nyenzo mpya zaidi ya zile walizonazo wanajeshi wa sasa waliopo Somalia,hivyo ameeleza kuwa wajiandae kuzikwa katika maeneo ya Mogadishu,ambayo Al Shabaab imeapa kuwa yatakuwa ni makaburi yao.

Kitisho hicho cha Al Shabaab,kinafuatia kutangazwa kwa maazimio ya viongozi wa Afrika, ambapo Mwenyekiti wa tume ya umoja huo, Jean Ping, alitangaza jijini Kampala kuwa wataongeza vikosi vya wanajeshi 4,000 kwa ajili ya kuongeza nguvu katika jeshi la kulinda amani nchini Somalia, AMISOM litakalopambana na kundi la Al Shabaab.

Rage,ameeleza kuwa Serikali ya mpito ya Somalia imeshindwa kuwashawishi washirika wake ambao amewaita kuwa hawana mwongozo wa kidini,katika kusaidia kuongeza majeshi nchini Somalia,ambapo sasa wameamua kutangaza kuongeza wanajeshi huko Mogadishu,na kueleza kuwa Al Shabaab,linatangaza kuingia katika vita vya jihad.

Hali nchini Somalia bado ni tete,ambapo hapo kabla majeshi ya Marekani na Umoja wa mataifa yalishindwa kupambana na vikundi vya uasi nchini humo,ambapo matukio ya mauaji ya mamilioni ya watu yamekuwa yakitokea,hali inayoelezwa kuwa inaweza kuwa mbaya zaidi,licha ya jitihada za kuongezwa majeshi.

Katika jiji la Mogadishu eneo hilo linatajwa kuwa ni miongoni mwa maeneo yanayotazamwa kuwa ni hatari zaidi kwa usalama na utekelezwaji wa haki za binaadamu,ambapo wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaeleza kuwa kuongezwa kwa majeshi zaidi ya AMISOM nchini humo,ni sawa na kuzidisha mashambulizi zaidi kutoka kwa vikundi vya uasi.

Tathmini iliyofanywa na Shirika la haki za binaadamu nchini Somalia katika kipindi cha miezi 7 iliyopita kwa mwaka huu,imeonyesha kuongezeka kwa matukio ya mapigano zaidi katika maeneo ya katikati ya mji,na inatajwa kupindukia ile ya mwaka 2009,ikielezwa kuwa mashambulizi mengi yalifanywa kufuatia vitisho vya makundi ya uasi.

Zaidi ya watu 745 wameripotiwa kufa na wengine 3,435 wamejeruhiwa katika kipindi kama hiki kwa mwaka jana jana pekee.

Mashambulio ya mara kwa mara yametajwa kufanywa na vikundi vya Ahlu Sunna na kundi la Al Shabaab,yanayochanganyika na mapigano ya kikabila,yamekuwa yakisababisha vifo vya raia kadhaa wasio na hatia.

Wakati hayo yakijiri,Sheikh Mohammed Saiid Atom ambaye anatajwa kuwa kuongoza kundi la wapiganaji katika mkoa wa Puntland,amewatangazia wananchi kuchukuwa silaha na kuingia katika mapambano ya vita vitakatifu vya Jihad,kwa nia ya kuhakikisha kuwa Serikali inakubali kuingizwa na kutumika kwa Sharia ya kiislamu.

Kwa mujibu wa mkaazi wa eneo hilo,Hussein Ali,ameeleza kuwa Sheikh Mohammed Saeid Atom anatajwa kuwafunza wapiganaji wa vikundi vya uasi tangu mwaka 2005, kwa kuwatumia vijana na fedha nyingi alizonazo kutokana na kufanya biashara ya kuuza silaha,hali inayotajwa kuwa ni vigumu kulidhibiti eneo hilo.

Mwandishi; Ramadhan Tuwa/ RTRE/DPAE/AFPE

Mhariri:Josephat Charo