1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al Shabab yadai imewauwa Wanajeshi 57 wa Kenya

Caro Robi
27 Januari 2017

Kundi la waasi la Somalia la Al Shabab limesema leo wapiganaji wake wamewaua wanajeshi kadhaa wa Kenya walipoivamia kambi ya kijeshi iliyoko Somalia, madai ambayo jeshi la Kenya imeyakanusha.

https://p.dw.com/p/2WU9P
Somalia Kenianische Soldaten im Kampf gegen gegen Al-Shabaab
Picha: picture alliance/AP Photo/B. Curtis

Msemaji wa Kenya Luteni Kanali Paul Njuguna hata hivyo ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa taarifa hizo ni za uongo lakini ameongeza kuna operesheni inayoendelea na wanapokea taarifa.

Kituo cha televisheni cha Kenya cha NTV kimeripoti kuwa wanejeshi kadhaa wa kikosi cha Kenya KDF wanaaminika kuuawa katika shambulizi na mapigano makali yanaripotiwa.

Mwezi Januari mwaka uliopita, kundi la al Shabab lilisema limewaua zaidi ya wanajeshi 100 wa Kenya katika kambi ya jeshi iliyo El Adde. Jeshi la Kenya halikuwahi kutoa taarifa kuhusu idadi hasa ya wanajeshi waliouawa katika shambulizi hilo licha ya vyombo vya habari vya Kenya kuripoti idadi sawa na iliyotolewa na Al Shabab.

Jeshi la Kenya lakanusha madai ya Al Shabab

Msemaji wa operesheni za kijeshi wa Al Shabab Sheikh Abu Musab ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa wanawasaka wanajeshi wa Kenya waliokimbilia msituni. Wapiganaji wawili wa kujitoa muhanga waliivamia kambi hiyo ya wanajeshi wa Kenya kwa magari yaliyojaa mabomu kabla ya kuanza kuwashambulia wanajeshi na kuyachukua magari yao na silaha baada ya kuwaua wanajeshi 57.

Kenia Armeechef Samson Mwathethe in Nairobi
Mkuu wa majeshi ya Kenya Samson MwathethePicha: picture-alliance/dpa/EPA/Str

Kundi la Al Shabab ambalo kwa wakati mmoja liliidhibiti nchi ya Somalia linataka kuiondoa madarakani serikali inayoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa na kuwaondoa wanajeshi wa kulinda amani wa Kenya, Djibouti, Uganda, Ethiopia na nchi nyingine zinazochangia katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika.

Mwaka 2011, Kikosi cha AMISON na wanajeshi wa Somalia waliwafurusha wapiganaji wa Al Shabab kutoka miji mikubwa na bandarani ambazo zilikuwa ngome zao kuu lakini wanajeshi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kukabiliana na mashambulizi ya hapa na pale kutoka kundi hilo hasa katika maeneo ya vijijini yasiyofikika kwa urahisi.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters

Mhariri:Josephat Charo