1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Albania na Macedonia zasubiri ridhaa kuingia Umoja wa Ulaya

Zainab Aziz
26 Juni 2018

Nchi za Umoja wa Ulaya zinajadili uwezekano wa kutoa ridhaa ya kuanzisha mazungumzo ya kuziingiza Albania na Macedonia katika umoja huo. Ufaransa na Uholanzi zapinga milango kuachwa wazi.

https://p.dw.com/p/30Kc0
Rumänien Proteste in Bukarest
Picha: Getty Images/AFP/D. Mihailescu

Mawaziri wa nchi za Umoja wa Ulaya leo wanajadili uwezekano wa kuanzisha mazungumzo juu ya kuziingiza nchi hizo mbili katika umoja huo lakini wakati huo huo baadhi ya nchi zimeelezea wasi wasi wao juu ya hali ya ufisadi na mapungufu ya utawala wa kisheria katika nchi hizo za Balkan.

Halmashauri wa Umoja wa Ulaya ilitoa hoja mnamo mwezi wa Aprili ya kuanzisha mazungumzo  hayo kwa sababu nchi hizo zimepiga hatua kubwa na kwamba zinastahili kuanzisha majadiliano ya kujiunga na Umoja wa Ulaya. Baada ya mzozo uliohusu jina la Macedonia baina ya Ugiriki na Macedonia kutatuliwa idadi kubwa ya nchi za Umoja wa Ulaya zipo tayari kuyaanzisha mazungumzo juu ya Macedonia kujiunga na Umoja wa Ulaya. Nchi hiyo iliyokuwa sehemu ya Yugoslavia ya zamani sasa itaitwa Jamhuri ya Macedonia Kaskazini.

Waziri wa Ujerumani anayeshughulikia masuala ya Umoja wa Ulaya, Michael Roth amesema Macedonia na Albania zimepiga hatua kubwa katika medani za utawala wa kisehria na uhuru wa mahakama na ndiyo sababu Ujerumani inaunga mkono kuanzishwa kwa mchakato wa kuziingiza nchi hizo mbili katika uanachama wa Umoja wa Ulaya. Ujerumani leo imezitaka Ufaransa na Uholanzi ziuruhusu Umoja wa Ulaya uanzishe mazungumzo na Albania na Macedonia ili kuleta utengamano magharibi mwa Balkani baada ya wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya kushindwa kukubaliana juu ya masharti ya mazungumzo.

Waziri wa Ujerumani anayeshughulikia masuala ya Umoja wa Ulaya Michael Roth
Waziri wa Ujerumani anayeshughulikia masuala ya Umoja wa Ulaya Michael RothPicha: DW/K. Delimitov

Ufaransa na Uholanzi zinapinga juhudi za kuacha milango yote wazi ili kuanzisha mazungumzo, badala yake rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anayeungwa na mkono na Uholanzi amesema Umoja wa Ulaya unahitaji kwanza kufanyiwa mageuzi kabla ya kuwaingiza wanachama wapya, lakini wanadiplomasia wa umoja huo wamesema msimamo wa Macron unatokana na wasi wasi wake juu ya kuchochewa kwa hisia za kuwapinga wahamiaji nchini mwake.

Kuingizwa haraka kwa Romania na Bulgaria katika Umoja wa Ulaya mnamo mwaka wa 2007 na mapungufu yaliyojitokeza katika kuwadhibiti wafanyakazi kutoka Ulaya Mashariki walioingia nchini Uingereza, kumeufanya mchakato wa kuwaingiza wanachama wapya uwe mgumu. Idadi kubwa ya wafanyakazi kutoka nchi za Ulaya Mashariki imesababisha hisia za kuupinga mpango wa Umoja wa Ulaya nchini Uingereza.

Waziri wa mambo ya nje wa Poland Jacek Czaputowicz
Waziri wa mambo ya nje wa Poland Jacek CzaputowiczPicha: picture alliance/PAP

Wakati huo huo mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wameitaka Poland itoe maelezo juu ya utawala wa kisheria kutokana na wasi wasi juu ya hatua zilizochukuliwa na serikali ya nchi hiyo za kuubana uhuru wa mahakama. Waziri wa mambo ya nje wa Poland Jacek Czaputowicz amesema wanachama wengine wa Umoja wa Ulaya wanahitaji muda ili kuweza kuyaelewa mageuzi yaliyofanywa na nchi yake kuhusu utawala wa kisheria.

Baraza la Umoja wa Ulaya leo litayajadili mageuzi hayo ya mfumo wa mahakama kwenye mkutano wa Luxembourg. Poland inakataa kabisa kwamba mageuzi katika mfumo wake wa sheria yanakiuka utawala wa sheria. Wizara ya mambo ya nje  imesema uchambuzi wa Tume ya Umoja wa Ulaya una makosa na unapotosha tathmini sahihi na kwamba mabadiliko yaliyofanywa na Poland kulingana na madai ya tume hiyo hayakuzingatiwa.

Mwandishi: Zainab Aziz/DPA/AFPE/RTRE

Mhariri: Iddi Ssessanga