1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Alexei Navalny aruhusiwa kutoka hospitali Berlin

Iddi Ssessanga
23 Septemba 2020

Kiongozi wa upinzani nchini Urusi Alexei Navalny ameonekana kwa mara ya kwanza hadharani baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali ya mjini Berlin ambako alikuwa anatibiwa kutokana na sumu inayouwa mishipa ya fahamu.

https://p.dw.com/p/3iuJE
Berlin Charite Alexei Navalny Instagram Post
Picha: Alexey Navalny/Instagram

Mwanasiasa huyo wa upinzani mwenye umri wa miaka 44 amekaa hospitalini mjini Berlin kwa siku 32, 24 kati yake akiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi, kabla ya madaktari kujiridhisha kuwa hali yake imeimarika vya kutosha kuweza kumruhusu. Timu yake imesema hata hivyo, kwamba atasalia nchini Ujerumani kwa muda kuendelea na matibabu ya uangalizi.

Katika ujumbe wa mtandao wa Instagram ulioambatanishwa na picha yake, Navalny amesema alikuwa anajifunza kurejesha urari wake kwa kusimama juu ya mguu mmoja, na amewashukuru madaktari wa hospitali ya Charite ya mjini Berlin kwa matibabu waliompatia.

Berlin I Oppositionsführer Alexei Navalny mit Ehefrau Yulia
Navalny akiwa na mke wake Yulia katika hospitali ya Charite mjini Berlin, Septemba 21, 2020.Picha: Navalny Instagram/AP/picture-alliance

Ujerumani yashusha pumzi

Msemaji wa serikali ya Ujerumani, Steffen Seibert amesema serikali imepata ahueni kutokana na kuruhusiwa kwa Navalny, lakini amekataa kutoa taarifa juu ya wapi alipo na kwa muda gani ataendelea kuwepo Ujerumani kabla ya kuomba hifadhi, akisema hilo litategemea mamlaka za uhamiaji.

Soma pia: Ujerumani yatishia kuiwekea vikwazo Urusi kuhusu Navalny

Serikali ya Ujerumani inasema vipimo vilivyofanywa nchini Ujerumani, Ufaransa na Sweden vimeonyesha kuwa alipewa sumu ya kemikali aina ya Novichok, ambayo inauwa mishipa ya fahamu.

Mataifa ya Magharibi yametaka maelezo kutoka Urusi. Seibert amesema Ujerumani na washirika wake wa Umoja wa Ulaya wataendelea kuishinikiza Urusi kutoa maelezo.

Soma pia: Navalny hatimaye asafirishwa Ujerumani kwa matibabu zaidi

''Bado tunaendelea na mawasiliano na majadiliano na washirika wetu wa Ulaya, na tutazidi kufanya hivyo, ili kuweza kufikia hitimisho juu ya namna ya kutathmini taarifa za Urusi kuhusu kesi hii na namna tunavyopaswa kujibu,'' amesema Seibert.

Deutschland Berlin Logo Charité
Hospitali ya Charite ambako Alexei Navalny amekuwa akitibiwa.Picha: John MacDougall/AFP/Getty Images

Kremlin yashikilia msimamo wake

Serikali mjini Moscow imesema bado haijaona ushahidi ya uhalifu na imekataa kuanzisha uchunguzi kamili mpaka sasa, badala yake imeanzisha uchunguzi wa awali,  huku ikulu ya Kremlin ikikanusha kuhusika kabisa na kadhia hiyo. Hata hivyo, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema Navalny yuko huru kurejea Moscow.

Soma pia: Afya ya Navalny yazidi kuimarika

''Ni habari njema ikiwa kweli mgonjwa anaendelea vyema. Tunamtakia uponaji wa haraka. Kuhusu kurejea kwake Moscow - kama ilivyo kwa kila raia wa Urusi, ana haki ya kufanya hivyo wakati wowote.''

Siku ya Jumanne, gazeti la Ufaransa la Le Monde liripoti kwa kunukuu vyanzo, kwamba Rais wa Urusi, Vladmir Putin alisema Navalny huenda alikunywa sumu mwenyewe kwa sababu isiyojulikana.

Lakini Peskov amesema gazeti hilo lilipotosha mazungumzo ya hivi karibuni kati ya Putin na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, na kwamba ripoti hiyo haikuwa sahihi.

Chanzo: Mashirika