1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AMMAN : Mfalme Abdallah wa Jordan amuonya Rice

15 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCaW

Mfalme Abdallah wa Jordan na ameitaka Marekani kushinikiza kwa nguvu zote ufufuaji wa mchakato wa amani wa Mashariki ya Kati.

Maafisa wa Jordan wamesema Mfalme Abdullah amemuonya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Condoleezza Rice alieko ziarani nchini Jordan kwamba kushindwa kufikia maendeleo ya kweli kwenye mchakato huo kutazidisha umwagaji damu katika eneo hilo.

Rice ambaye yuko katika ziara ya Mashariki ya Kati mapema hapo jana alikuwa na mazungumzo na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina mjini Ramallah.Abbas amekataa mipango ya Marekani ya kuundwa kwa taifa la Palestina la kipindi cha mpito likiwa na mipaka ya muda na kusisitiza haja ya kuwepo kwa amani ya kudumu.

Katika mkutano na waandishi wa habari Rice amesisitiza kwamba kauli hiyo ya Abbas isitafsiriwe kuwa ni kukataa utekelezaji wa awamu kwa mchakato huo wa amani Mashariki ya Kati ujulikanao kama ramani ya amani.

Rice pia anatazamiwa kukutana na Rais Hosni Mubarak wa Misri na Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert katika ziara yake hiyo ya Mashariki ya Kati.