1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AMMAN : Rice akutana na Mfalme Abdullah wa Jordan

20 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCQA

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleezza Rice amewasili mjini Amman Jordan katika harakati za kutaka kuungwa mkono na Waarabu kwa juhudi za Marekani za kufufuwa mchakato wa amani unaotatizwa na makubaliano ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ya Palestina na kundi la Hamas.

Kukiwa kumepatikana mafanikio kidogo katika mkutano wa viongozi wa Israel na Palestina Rice amekutana na Mfalme Abdullah wa Jordan katika ziara yake hiyo fupi ambapo maafisa wamesema kuwa alimjulisha juu ya mkutano wake wa jana na Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina ambao imeripotiwa kuwa hakuna makubaliano mapya yaliofikiwa.

Rice pia anatazamiwa kukutana na wakuu wa usalama na ujasusi wa Saudi Arabia,Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri na Jordan kujadili serikali ya umoja wa kitaifa ya Palestina.

Rice hapo kesho anatazamiwa kuiwakilisha Marekani katika mkutano wa kundi la pande nne linaloshughulikia amani ya Mashariki ya Kati linalojumuisha Marekani,Urusi, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya mjini Berlin nchini Ujerumani.

Kundi hilo la pande nne limekuwa likishinikiza kutambuliwa kwa taifa la Israel, kukanusha umwagaji damu na kwambaHamas ikubali makubaliano yaliopita kati ya Israel na Palestina venginevyo kususiwa misaada kwa serikali ya Palestina kutaendelea kubakia pale pale.