1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amri ya kutotembea wakati wa usiku Nakuru

26 Januari 2008
https://p.dw.com/p/Cxvf

NAIROBI: Serikali nchini Kenya imetoa amri ya kutotembea wakati wa usiku mjini Nakuru katika mkoa wa Bonde la Ufa.Hatau hiyo imechukuliwa kufuatia mapambano ya kikabila yaliyoua si chini ya watu 10 na kusababisha maelfu ya watu kukimbia makaazi yao.Kiongozi wa upinzani,Raila Odinga amesema machafuko hayo hayakuchochewa na wafuasi wake.Vile vile Odinga kwa mara nyingine tena amesema yeye hatochukua wadhifa wa waziri mkuu katika serikali ya Rais Mwai Kibaki.

Siku ya Alkhamisi katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan alifaulu kuwakutanisha Kibaki na Odinga kwa mara ya kwanza tangu kuchaguliwa kwa Kibaki kufuatia uchaguzi wa Desemba uliozusha mabishano ambao upinzani unasema ulifanyiwa udanganyifu.Kofi Annan anaejaribu kuleta masikilizano kati ya Kibaki na Odinga amesema:

"Bila ya kuwepo upatanisho na ushirikiano hatutoweza kuwa na jamii tunayoitaka yenye amani,utulivu na iliyo imara."

Kiasi ya watu 800 wameuawa na wengine 250,000 wamekimbia makaazi yao tangu machafuko yaliyozuka kufuatia uchaguzi wa Desemba 27.