1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Angela Merkel-Likizoni

24 Julai 2008

Kanzela Angela Merkel anaenda likizoni mara tu akisha mkaribisha seneta Barack Obama huko Berlin.

https://p.dw.com/p/Eiw7

Kanzela Angela Merkel wa Ujerumani, alikua jana na mkutano wake wa mwisho na waandishi habari kabla likizo yake ya majira ya kiangazi.

Mabishano ya kisiasa yanayomkabili si kidogo:siku za usoni za serikali yake ya muungano wa vyama vikuu,mpango wa kuachana na nishati ya nuklia,mvutano wa mradi wa kinuklia na Iran,vita nchini Afghanistan na mzozo wa Mashariki ya kati.Mbali na mizozo hiyo yote,Angela Merkel anatembelewa wakati huu na Seneta Barack Obama wa Marekani mjini Berlin.

Baada ya kukutana leo hii na mtetezi wa wadhifa wa Urais wa Marekani kutoka chama cha Democratic party,Seneta barack Obama, Kanzela Angela Merkel atasahau kwa muda pirika pirika zake za kisiasa na kwenda likizoni.Kwanza, atafunga safari ya Bayreuth ,kusini mwa Ujerumani kuhudhuria sherehe za kitamaduni za Richard-Wagner,mojawapo ya mwahala muchache ambako mumewe Joachim Sauer, huonekana ubavuni mwa m kewe.Kutoka hapo ataelekea kusini milimani kutembea kwa mguu.

Na hii alisisitiza sana katika mkutano wake wa jana na waandishi habari mjini Berlin kwamba anakwenda kulala na kupumzika huko.Kupumzika anastahiki kwani, kinyume na wafanyikazi wa kawaida, Kanzela wa Ujerumani hatumiki masaa 40 kwa wiki-manane kwa siku bali zaidi.

Muandishi mmoja alimuuliza: iwapo ataitumia likizo yake hii kuzingatia kipindi cha miaka 3 cha utawala wake ? Alijibu kuwa hii itatimia hapo novemba na si sasa. Akaongeza ana hiyari kuangalia mbele kuliko nyuma.

Ikiwa yeye hataki kuangalia nyuma, tumfanyie sisi:

Pale Angela merkel alipoingia Ikulu Berlin kama kanzela wa serikali ya muungano ya vyama vikuu kati ya CDU na SPD,ni wachache tu waliotarajia kuwa ndoa hiyo ingedumu miaka 4 kamili ya utawala.Na sasa miaka 3 imepita na ishara zote zabainisha kwamba hata mwaka wa 4 ataumaliza kama kanzela.

Ukitupia macho mapatano ya 2005 ya maafikiano ya vyama ya serikali ya muungano, utaona hadi thuluthi-mbili ya miradi ilioafikiwa imetimizwa.Uchumi unastawi bora zaidi kuliko katika baadhi ya nchi nyengine za magharibi na siasa ya nje ya busara inayofuatwa na ujerumani inathaminiwa ulimwenguni.

Hata mvutano uliokuwapo na China pale Kanzela Merkel alipompokea Dalai Lama huko ikulu,Berlin, sasa umefifia.Hatahivyo, Kanzela Merkel atachukua tatizo moja kichwani mwake anapokwenda likizo:Mzozo wa mradi wa kinuklia unaofuka moto wa Iran.

Angela Merkel anaionesha ameingiwa na wasi wasi mno na ishara zinazotatanisha kutoka Teheran na anadai endapo hali ikibaki hivyo, vikwazo vikali zaidi iwekewe Iran na baraza la Usalama la UM.Na hilo ni onyo lililowazi kwa Russia na china, dola 2 zenye turufu ya veto kuwa zishirikiane nazo ili kuepusha balaa kubwa zaidi.

Endapo suluhisho la kidiplomasia litashindwa kufumbua kitandawili cha mradi wa nuklia wa Iran,na vita vipya vikiripuka juu ya Iran na kuzusha balaa kubwa katika ghuba na mashariki ya Kati ,Angela Merkel hapo atakabiliwa na mtihani mpya,tangu katika sera za nje hata za ndani nchini.Haya ni mawazo ambayo hata akiwa likizoni milimani hataweza kuyaepuka.Hatahivyo, tumtakia Kanzela Merkel likizo njema,kwani anaihitaji kweli.