1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Angola yafanya uchaguzi wa wabunge

Lilian Mtono
23 Agosti 2017

Angola inafanya uchaguzi wa wabunge unaotarajiwa kumuingiza madarakani waziri wa ulinzi wa nchi hiyo Joao Lourenco baada ya miaka 38 ya utawala wa rais Jose Eduardo dos Santos. 

https://p.dw.com/p/2igqU
Angola Wahl José Eduardo dos Santos
Picha: Getty Images/AFP/M. Longari

Lourenco anakua kiongozi mpya wa kwanza kwa taifa hilo la pili kwa uzalishaji wa mafuta Afrika baada ya miaka 38 ya utawala wa rais Jose Eduardo dos Santos. 

Waandishi wa habari wa shirika la habari la AFP wameshuhudia kuanza taratibu kwa zoezi la kupiga kura katika kituo kimoja katika mji mkuu wa Luanda, ambako dos Santos na Lourenco walipangiwa kupiga kura zao baadaye leo.

Joao Lourenco, ambaye ameahidi kuimarisha ukuaji uchumi na kukabiliana na ufisadi, atarithi taifa hilo linalokumbwa na mdororo wa uchumi wakati hali ya ukosefu wa usawa, mfumuko wa bei na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira vikiwaumiza Waangola ambao hawajanufaika na mapato makubwa ya mafuta katika kipindi cha muongo mmoja.

Chama tawala cha People's Movement for the Liberation of Angola, MPLA kinatarajiwa kusalia madarakani lakini kukiwa na kupungua kwa uungwaji mkono. Uungwaji wake mkono umepungua kutokana na kuongezeka kwa madai ya kuwapendelea watu wake wa karibu kisiasa, ingawa Waangola wengi wameendelea kuwa waaminifu kwa chama hicho ambacho kiliibuka na ushindi baada ya miaka 27 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo mwaka 2002.

Kumekuwepo na maswali kuhusiana na kiwango cha mamlaka atakayokuwa nayo Lourenco iwapo atashinda, kwa kuzingatia kwamba kiongozi wa zamani Jose Eduardo dos Santos ataendelea kuwa kiongozi wa chama cha MPLA na kwa kiasi kikubwa bado ana kauli kuhusiana na kufikiwa kwa maamuzi ndani ya chama.

Angola Luanda Wahlen
Vyombo vya habari vimeripoti kuanza taratibu kwa zoezi hilo la kupiga kura mjini LuandaPicha: DW/A. Cascais

Binti yake Isabel anayeongoza kampuni ya taifa ya uzalishaji mafuta, Sonangol na mtoto wake wa kiume Jose Filomeno akiongoza wakfu wa taifa wa uwekezaji.

Huku vikikabiliwa na hatua kali za kiusalama na vyombo vya habari vinavyopendelea serikali, vyama vya upinzani vinavyoongozwa na UNITA na Casa-CE, vimechochea hasira kwa wafuasi wake dhidi ya serikali kutokana na hali mbaya inayowakabili. Kiongozi wa chama cha UNITA, ambacho awali kilikuwa kundi la waasi Isaias Samakuva alizungumzia masuala ya umasikini, kukosekana kwa nishati ya umeme na ajira.

Chama cha MPLA kilichotawala tangu Angola ilipopata uhuru wake kutoka kwa Wareno mwaka 1975, kinatarajiwa kuviangusha vyama vya upinzani ambavyo vinabanwa na utawala wa kiimla wa dos Santos.

Hata hivyo chaguo la dos Santos, Joao Lourenco,  ambaye ni mwaminifu kwa Rais dos Santos hadhaniwi kufanya mabadiliko ya haraka kwenye serikali ambayo mara nyingi imekuwa ikikosolewa kwa rushwa na kushindwa kukabiliana na umasikini. 

Kiasi ya Waangola Milioni 9.3 wameandikishwa kupiga kura kuchagua wabunge 220 wa bunge la Kitaifa. Chama kitakachoshinda baadae kitachagua Rais.

Mwandishi: Lilian Mtono/eap/afpe.

Mhariri:Josephat Charo