1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Askofu Mixa aomba kujiuzulu

22 Aprili 2010

Je, Baba mtakatifu ataridhia ?

https://p.dw.com/p/N37m
Askofu Walter Mixa wa ausgburgPicha: picture alliance / dpa

Askofu Walter Mixa wa Augsburg,Ujerumani,aliegonga vichwa vya habari hivi punde kwa kuwapiga watoto wadogo vibao na kwa hitilafu katika hesabu zake alizotoa juu ya matumizi ya fedha, yadhihirika, ameamua kuwajibika. Gazeti la "Augsburg Allgemeine " liliripoti jana kuwa, Askofu Mixa, amejitolea kwa Baba Mtakatifu Benedikt XXI kujiuzulu. Katika barua yake kwa Baba mtakatifu ,Askofu Mixa , amejitolea pia kuacha wadhifa wake kama askofu anaewahudumia wanajeshi wa Ujerumani.Kwa desturi, ombi kama hilo la kujiuzulu, hukubaliwa tu na Uongozi wa Vatikani mjini Roma.

Kwamba, Askofu Walter Mixa ataamua haraka hivyo kujiuzulu kama askofu wa mji wa Augsburg, Kusini mwa Ujerumani,hakuna alietazamia hayo mjini humo.Mkaazi mmoja wa jiji la Augsburg alisema,

"Nadhani hakuwa na chaguo jengine bali kujiuzuku."

Mkaazi mwengine akasema,

"Yadhihirika, kuna visa vingi alivyofanya na sio tu kupiga watoto na kwahivyo, nahisi imestahiki kuwa anajiuzulu kutoka wadhifa wake."

Mkaazi mwengine wa mji wa Augsburg akichururikwa na machozi alisema:

"Nahisi ni jambo la kuhuzunisha sana, tena sana kwavile amedhirika kuwa mtu mwenye uwezo mkubwa ,kasisi mwenye heba na bashasha."

Kwa muujibu wa mwenyekiti wa Mkutano wa maaskofu wa Kikatoliki,Askofu Robert Zollitsch na hata Askofu Reinhard Marx,Askofu Mixa, amejiliwa na wakati wa kutubia na kujivuta mbali kidogo huku uvumi ukienea mjini Augsburg , kwa muda gani kisa hiki kingeendelea hadi Askofu Mixa kun'gatuka.

Jana jioni , wakati ukawadia:Askofu Mixa ,alitangaza atamuomba Baba Mtakatifu Benedikt XVI, aridhie kujiuzulu kwake tangu kama Askofu wa Augsburg, hata pia Askofu wa Jeshi la Ujerumani.

Kwani, mjadala hadharani mnamo wiki chache zilizopita kumhusu yeye, uliwaathiri mno tangu makasisi na hata waumini katika kanisa lake -aliandika Mixa katika barua yake kwa Baba mtakatifu.Kwa kuamua kujiuzulu,Askofu Mixa ,amekusudia kuchangia kulipunguzia dhara zaidi Kanisa Katoliki na kufungua mlango mpya.

Makamo wa msemaji wa Baraza la makasisi mjini Augsburg,Michael Sauler, amemvulia kofia na kumpa heko Askofu Mixa, kwa hatua aliochukua.Amevuta pumzi kwani hali ya mambo ilikua haivumiliki tena.

Askofu Mixa, ambae Jumapili hii ijayo anatimiza umri wa miaka 69, aliungama madhambi yake baada ya kukaa kimya muda mrefu kuwa, wakati alipokuwa Padri wa mji wa wilaya ya Schrobenhausen, akiwapiga vibao watoto walioishi katika Bweni la kanisa lake.Isitoshe, alitumia fedha si zake-fedha kutoka wakfu wa mayatima ,ulioendesha Jumba hilo la watoto hao.Miongoni mwa matumizi yake kutoka mfuko wa wakfu huo, akinunua anasa za kale,pete ya kiaskofu na hata kulipia mvinyo.

Mwandishi: Annemarie Ruf/ARD

Mtayarishi: Ramadhan Ali

Mhariri:Abdul-Rahman