1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Assad ahutubia hadharani

26 Julai 2015

Katika hotuba yake ya kwanza hadharani katika kipindi cha mwaka mmoja Rais Bashar Assad wa Syria ameapa Jumapili (26.07.2015) kushinda vita vya wenyewe kwa wenyewe wakati akikiri jeshi lake lina uhaba wa askari

https://p.dw.com/p/1G4xJ
Rais Bashar Assad wa Syria akizungumza mjini Damascus. (26.07.2015)
Rais Bashar Assad wa Syria akizungumza mjini Damascus. (26.07.2015)Picha: picture-alliance/Press TV via AP video

Katika hotuba yake ya kwanza hadharani katika kipindi cha mwaka mmoja Rais Bashar Assad wa Syria ameapa Jumapili (26.07.2015) kushinda vita vya wenyewe kwa wenyewe vya muda mrefu nchini mwake wakati akikiri kwamba jeshi lake linakabiliwa na uhaba wa askari.

Hotuba yake hiyo ilionyesha kujiamini imekuja mwaka wa tano wa mzozo unaowapambanisha vikosi vyake na vile vya waasi,wapiganaji wa Kiislamu wa itikadi kali na Kundi la Waislamu wa itikadi kali la Dola la Kiislam. Hotuba hiyo ya Assad iliyoonyeshwa kwenye televisheni wakati wa asubuhi ni ya kwanza kutolewa hadharani tokea aapishwe kwa muhula wa tatu wa miaka saba madarakani hapo mwezi wa Julai mwaka jana.

Katika kipindi hicho Assad alifanya mahojiano na vyombo vya habari kadhaa vya Kiarabu na vya kimataifa.Assad amekiri kwamba magenerali wake ilibidi wahamishe vikosi vyake kutoka eneo moja la mapambano kwenda jengine ili kuyahami maeneo ambayo yana umuhimu kijeshi, kisiasa au kiuchumi.Amesema kwamba kutekwa kwa baadhi ya maeneo na waasi kumewavunja moyo Wasyria.

Vikosi vya Syria vimepata pigo mara kadhaa tokea mwezi wa Machi ikiwa ni pamoja na kupoteza mji wa Idlib kaskazini magharibi ambao ni mji mkuu wa jimbo lenye kupakana na Uturuki.Hapo mwezi wa Mei serikali ilipoteza mji wa kihistoria ulioko kati mwa nchi hiyo wa Palmyra kwa wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu ambao pia waliteka sehemu ya mji wa kaskazini mashariki wa Hassakeh.

Kupoteza kwa miji hiyo kwa kiasi fulani kunaweza kusahihishwa hivi sasa kutokana na msaada mkubwa kutoka kwa mshirika mkubwa wa serikali Iran ambayo imefikia makubaliano ya nyuklia na nchi zenye nguvu duniani ambapo kwayo nchi hiyo itaondolewa vikwazo vya kimataifa iilivyowekewa.

Hotuba yake yashangiliwa

Assad ambaye alikuwa akikatizwa mara kwa mara kwa kushangiliwa katika hotuba yake hiyo amesema "Hatusambaratiki.Tuko imara na tutapata ushindi."

Wanajeshi wa serikali ya Syria.
Wanajeshi wa serikali ya Syria.Picha: picture-alliance/dpa/Dmitriy Vinogradov

Amesema suala la kushindwa haliko katika kamusi ya jeshi la Waarabu wa Syria.

Assad amejaribu kuhalalisha kupoteza baadhi ya maeneo ukiwemo mji wa Idlib.Vikosi washirika wa Assad wakiwemo wapiganaji wa kundi la Hezbollah la Lebanone na washauri wa kijeshi wa Iran wanadhibiti eneo lililo pungufu ya nusu ya Syria yenye ukubwa wa kilomita za mraba 185,000.

Amesema ilikuwa ni muhimu kuweka utulivu katika maeneo muhimu ili wanajeshi wao waendelee kuyashikilia na kwamba wasi wasi juu ya wanajeshi wao umewalazimisha wayaachie maeneo mengine.

Assad amekiri kwamba kuna uhaba wa askari jeshini lakini amesema hataki kutowa taswira mbaya ambayo itatumiwa na vyombo vya habari hasimu kusema kwamba rais anasema watu wanakwepa kujiunga na jeshi. Amesema katika miezi ya hivi karibuni hasa ya April ma Mei idadi ya watu wanaojiunga na jeshi imeongezeka na kwamba kila punje ya ardhi ya Syria ina thamani.

Msamaha waliolikacha jeshi

Hapo Jumamosi serikali ya Assad imetangaza msamaha wa jumla kwa askari waliokimbia jeshini na watu wanaokwepa kujiandikisha jeshini kutimiza wajibu wao wa kutumikia taifa Kuna maelfu ya askari walioliasi jeshi ndani na nje ya Syria wengi wao wamejiunga kupambana upande wa waasi.Vijana wengine wengi wameikimbia nchi hiyo kuepuka kuadikishwa jeshini ambalo ni jambo la lazima.

Wanajeshi wa Syria walioasi.
Wanajeshi wa Syria walioasi.Picha: picture alliance/AP Photo

Assad pia ametowa msamaha kama huo kwa wahalifu lakini hakuna mfungwa yoyote wa kisiasa aliyeachiliwa huru miongoni mwa maelfu ya wafungwa wa kisiasa walioko magerezani nchini Syria.

Shirika la Uangalizi wa Haki za Binaadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza hivi karibuni limeripoti kwamba takriban wanajeshi 49,100 na wapigananji 32,500 wanaoiunga mkono serikali wameuwawa tokea uasi ulipoanza nchini humo hapo mwezi wa Machi mwaka 2011.

Assad amesema serikali yake ilikuwa haikuvitaka vita hivyo lakini kutokana na kwamba vililazimishwa kwao jeshi la Waarabu wa Syria lilikabiliana na magaidi kila mahala akimaanisha wale wanaopambana kuupinga utawala wake kuwa ni magaidi.

Akizungumzia juu ya mazungumzo ya kisiasa kiongozi huyo wa Syria amesema juhudi zozote zile ambazo hazizingatii kupambana na ugaidi zitakuwa hazina maana yoyote ile.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP

Mhariri : Bruce Amani