1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Assad bado yuko madarakani miaka mitano vitani

12 Machi 2015

Licha ya matumaini ya mataifa ya magharibi na nchi za Kiarabu kwamba Rais Bashar al Assad ataishia kwenye pipa la taka la historia, kiongozi huyo anaingia katika miaka mitano ya vita akizidi kujimarisha madarakani Syria.

https://p.dw.com/p/1EpPR
Rais Bashar al-Assad wa Syria.
Rais Bashar al-Assad wa Syria.Picha: Reuters/Sana

Mod

Licha ya matumaini ya mataifa ya magharibi na nchi za Kiarabu kwamba Rais Bashar al Assad ataishia kwenye pipa la taka la historia, kiongozi huyo anaingia katika miaka mitano ya vita huku akizidi kuimarisha hatamu zake za uongozi nchini Syria. Mohamed Dahman anatupia macho miaka minne ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria bila ya kuwepo ishara ya kun'gatuka kwa Assad kulikokuwa kukitumainiwa kwa muda mrefu.

___________________________

Wasi wasi juu ya kundi la wapiganaji wa jihadi wa Dola la Kiislamu kuzidi kuteka maeneo nchini Syria na Iraq unamaanisha kwamba masuala yanayopewa kipau mbele na jumuiya kimataifa hayajumuishi tena suala la kumn'gowa Assad.

"Assad ameimarisha msimamo wake kimataifa" hivyo ndivyo anavyosema Volker Perthes mkurugenzi wa Taasisi ya Ujerumani ya Masuala ya Kimataifa na Usalama na kwamba Marekani na mataifa ya Ulaya na mengineyo hayadai tena kundoka kwake haraka madarakani.

Katika kipindi cha miaka minne tokea kuzuka kwa mzozo huo hapo mwezi wa Machi mwaka 2011 uliogharimu maisha ya watu 210,000 vikosi vya Assad vimefanikiwa kuzuwiya kusonga mbele kwa waasi wanaoungwa mkono na mataifa ya magharibi na wapiganaji wa jihadi wanaotaka kumpinduwa.

Upinzani waregeza kamba

Wapiganaji wa upinzani katika mji wa Allepo.
Wapiganaji wa upinzani katika mji wa Allepo.Picha: picture-alliance/dpa/Sputnik/S. Voskresenskiy

Hata upinzani wa Syria haudai tena kujiuzulu kwake kama sharti la kufanyika kwa mazungumzo ya amani licha ya kwamba mashirika ya kutetea haki za binaadamu bado mara kwa mara yamekuwa yakimshutumu Assad kwa kuwauwa ovyo wananchi wake mwenyewe kwa kutumia helikopta kuwadondoshea mabomu ya mapipa.

Kwa mujibu wa Perthes taarifa zinazotolewa na Marekani na serikali za nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zinadokeza hali iliopo sasa kwa njia ya moja kwa moja au isio ya moja moja kwa moja ya kukubali Assad aendelee kuushikilia urais na kufanya juhudi za kuunda aina fulani ya serikali ya umoja wa kitaifa ambayo itamjumuisha Assad halikadhalika wapiganaji wa upinzani ambao sio majihadi.

Mwandiplomasia huyo wa Ulaya ambaye mara nyingi hufanya safari za Damascus amesema mataifa ya magharibi yamegawika juu ya namna ya kufikia makubaliano na mtu ambaye mwezi uliopita tu alielezewa na Waziri Mkuu wa Ufaransa Manuel Valls kuwa ni "mchinjaji."

Msimamo wa Ulaya ni mgumu kufanikiwa

Rais Bashar al-Assad wa Syria akitembelea vikosi vya serikali mashariki mwa Damascus.
Rais Bashar al-Assad wa Syria akitembelea vikosi vya serikali mashariki mwa Damascus.Picha: picture-alliance/dpa/AP Photo/SANA

Mwanadiplomasia huyo amesema nje ya Ufaransa,Uingereza na Denmark ambazo zimekataa Assad kuwa na dhima yoyote ile katika mustakbali wa Syria nchi nyingi za Ulaya zinafikiri kwamba baada ya miaka minne msimamo huo hauwezi kufanikiwa.

Nchi zikiwemo Sweden, Austria,Uhispania,Jamhuri ya Czech na Poland hazioni faida ya kutengwa kwa Assad na wanataka kuregezwa kwa msimamo wa Ulaya.

Kubadilika kwa msimamo

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Jhon Kerry.
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Jhon Kerry.Picha: Reuters/D. Balibouse

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry hivi karubuni aliweka wazi kubadilika kwa msimamo wa mataifa ya magharibi kuhusiana na kiongozi huyo wa Syria.

Kerry amesema Assad amepoteza sura yoyote ile ya uhalali lakini kipau mbele chao sasa ni kulishinda kundi la Dola la Kiislamu ambalo kwa Kiarabu hutambulika kama Daesh.

Lakini kauli iliyowakasirisha waasi ni ile ya mjumbe wa Umoja wa Mataifa Staffan de Mistura ya hivi karibuni kumuelezea Assad kuwa  ni "sehemu ya suluhisho" nchini Syria.

Hivi sasa serikali inadhibiti asilimia 40 ya ardhi ya Syria ambayo ni maskani ya asilimia 60 ya wananchi wa nchi hiyo.

Takriban miji yote mikubwa ya Syria isipokuwa wa Raqa ambao kundi la Dola la Kiislamu limejitangazia kuwa mji mkuu wao na nusu ya sehemu ya mji wa Allepo iko chini ya udhibiti wa serikali.

Lakini hakuna dalili kabisa kwamba vita hivyo vya Syria vinamalizika.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Yusuf Saumu