1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AU yaidhinisha mkakati wa kujitoa katika ICC

Mohammed Abdulrahman
1 Februari 2017

Viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika - AU, wameidhinisha kile kinachoitwa wito wa mkakati  wa hatua ya pamoja ya kujitoa katika mahakama ya uhalifu ya kimataifa- ICC

https://p.dw.com/p/2Wm2N
Afrikanische Union Marokko nach 33 Jahren wieder aufgenommen
Picha: picture alliance/AP Photo/M. Ayene

Viongozi hao wa  Umoja wa Afrika waliidhinisha pendekezo hilo wakati wakikaribia kumaliza mkutano wao wa kilele wa siku mbili hapo jana mjini Addis Ababa. Uamuzi wao unaashiria msimamo wa  viongozi wa kiafrika wa kutokuwa tena na uvumilifu  kuhusu utendaji wa Mahakama  hiyo ya Kimataifa-ICC, ambapo baadhi wanadai kwamba imekuwa tu ikiziandama zaidi nchi za kiafrika na kuendesha kesi zinazohusiana na  mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na maovu mengine dhidi ya binaadamu na kushindwa kuchukua hatua  kuhusiana na matukio  ya aina hiyo  kwengineko nje ya bara  hilo.

Mnamo mwaka uliopita Afrika Kusini, Burundi na Gambia  zilitangaza nia ya kujitoa katika mahakama hiyo, na kuzusha wasiwasi kwamba huenda nchi nyengine zikafuata. Mkuu wa ofisi ya  Shirika la Kimataifa la misaada Oxfam katika Umoja wa  Afrika Desire Assogbavi, alithibitisha kuidhinishwa  kwa mkakati huo.

Duru moja  katika  baraza la sheria la umoja huo ambayo haikutaka kutajwa jina kwa kuwa hairuhusiwi kuzungumza na vyombo vya habari  ilisema  nchi wanachama ziligawika  ilipozuka hoja  iwapo zitowe  wito wa kujitoa katika mahakama hiyo ya mjini The Hague kwa pamoja  au kila nchi peke yake.

Äthiopien Treffen Afrikanische Union - Tschad Außenminister Moussa Faki
Mwenyekiti mpya wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Mouusa Faki MahamatPicha: picture-alliance/Anadolu Agency/M. Wondimu Hailu

Baadhi ya nchi za Kiafrika  zimekuwa  zikiikosoa ICC kwa kuwaandama viongozi wa taifa barani Afrika. Kwa mfano  Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan amekuwa akisakwa na mahakama hiyo tangu 2009, kwa madai  ya kupanga mauaji katika jimbo la magharibi mwa Sudan la Darfur.

Mahakama hiyo ya kimataifa  pia ilisababisha  mzozo na mabishano na baadhi ya mataifa ya Kiafrika, baada ya kumfungulia mashtaka ya uhalifu na maovu dhidi ya binaadamu Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya , kufuatia machafuko yaliotokea kufuatia uchaguzi wa  2007 ambapo zaidi ya  watu 1,000 waliuwawa. Kesi hiyo ilishindwa baada ya mwendesha mashtaka wa ICC kusema  ameshindwa kupata ushirikiano kutoka  serikali ya Kenya  . Swali hivi sasa ni iwapo nchi za kiafrika kweli zitakuwa na ubavu wa kujitoa kwa pamoja na  athari za hatua hiyo. Bw Agina Ojwang ni mwanasheria na mchambuzi wa masuala ya ICC, aliyeko mjini Nairobi.

Afisa anayehusika na mpango wa sheria katika Shirika la Haki za Binaadamu Human Rights watch Elise Keppler amesema mkakati wa kujitoa katika Mahakama ya ICC, hakuna  muda maalum na mapendekezo madhubuti kuhusu hatua hiyo ni machache mno. Alisema mnamo miezi ya hivi karibuni nchi kadhaa za Kiafrika zikiwemo Nigeria, Senegal na Congo, zimekuwa zikielezea misimamo yao, zikiiunga mkono Mahakama hiyo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Associated Press,  waraka wa mkakati huo wa pamoja wa nchi za kiafrika kujitoa  katika Mahakama ya uhalifu ya kimataifa ICC, umependekeza badala yake nchi hizo ziimarishe mifumo yao yenyewe ya kisheria na kutanua  uwezo wa kiutendaji wa Mahakama ya  Sheria na Haki za Binaadamu ya Afrika, ili kupunguza kuitegemea Mahakama ya Kimataifa -ICC

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, dpa, ap
Mhariri: Iddi Ssessanga