1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AU yataka kesi dhidi ya Kenyatta katika ICC iahirishwe

13 Oktoba 2013

Viongozi katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa, Ethiopia, wametaka kesi inayoendelea katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu - ICC dhidi ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta icheleweshwe

https://p.dw.com/p/19yh3
Picha: John Muchucha/AFP/Getty Images

Haya yanajiri baada ya viongozi hao wa Afrika kulalamika kuwa mahakama ya ICC inalilenga tu bara la Afrika katika kesi zake. Rais Kenyatta pamoja na naibu wake William Ruto, wanakabiliwa na mashitaka ya uhalifu wa kivita kuhusiana na machafuko yaliyofuatia uchaguzi mkuu uliokuwa wa utata wa mwaka wa 2007, ambapo zaidi ya watu 1,000 waliuawa na wengine wengi kuwachwa bila makao. Kesi ya Kenyatta inatarajiwa kuanza mwezi ujao wa Novemba.

Umoja wa Afrika pia umeunga mkono azimio linalosema kuwa hakuna kiongozi yeyote wa nchi barani Afrika atakayefika katika mahakama ya kimataifa. Suala la kujiondoa kutoka ICC pia lilijadiliwa katika mkutano huo wa kilele mjini Addis Ababa, lakini halikuungwa mkono kwa kutosha.

Kesi dhidi ya Makamu wa Rais wa Kenya William Ruto tayari inaendelea katika mahakama ya ICC, The Hague
Kesi dhidi ya Makamu wa Rais wa Kenya William Ruto tayari inaendelea atika mahakama ya ICC, The HaguePicha: Reuters

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia ambaye pia ni mwenyekiti wa baraza kuu la AU, Tedros Adhamom Ghebreyesus, amesema AU haina mamlaka ya kumzuia kiongozi wa taifa kushitakiwa mjini The Hague, ikiwa ni pamoja na Kenyatta, lakini nchi za Afrika zinapanga kuwasiliana na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka kesi ya Kenyatta icheleweshwe kabla ya mashitaka yake kuanza rasmi mnamo Novemba 12.

Baraza la Usalama lina mamlaka ya kuamuru kesi hiyo kucheleweshwa kwa mwaka mmoja, lakini kama hilo litafanyika au la, ndio suali kuu. Kesi haijawahi kucheleweshwa hapo kabla. Ghebreyesus amesema kama uamuzi huo hautachukuliwa, basi AU itaomba kesi dhidi ya Kenyatta iahirishwe, na kama hilo halitafanyika, basi viongozi wa Afrika wataamua kuwa Kenyatta hastahili kufikishwa katika mahakama hiyo mjini The Hague.

Uamuzi huo uliofanywa katika siku ya mwisho ya mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi wa Umoja wa Afrika ulikuwa wa kauli moja, kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn. Kenyatta na Rais wa Sudan Omar al-Bashir ambaye pia anatakiwa kwa uhalifu wa kivita, walihudhuria kikao hicho.

Kilio kutoka makundi ya haki za binaadamu

Hatua hiyo ya AU maramoja ilishutumiwa na makundi ya kutetea haki za binaadamu, kutoka Kenya na pia ya kimataifa. Naibu mkurugenzi mkuu wa Tume ya Kutetea Haki za Binaadamu nchini Kenya – KHRC Davis Malombe anasema wito wa kutaka kesi hiyo icheleweshwe “ni jaribio jengine la kuvuruga na kuchelewesha haki kwa waathiriwa wa Kenya na unasaliti madai ya ahadi ya AU ya kupambana na ukwepaji sheria“.

Wajumbe katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika - AU, mjini Addis Ababa, Ethiopia
Wajumbe katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika - AU, mjini Addis Ababa, EthiopiaPicha: AFP/Getty Images

Baada ya kuwasili mjini Addis Ababa, Ethiopia kabla ya kikao, Kenyatta alitoa hotuba iliyokuwa na maneno makali, akiishutumu ICC kuwa wakala wa himaya ya kibeberu inayosambaratika. Alisema “Hata ingawa tuliongozwa na kudhibitiwa na mabeberu na maslahi ya kikoloni katika miaka iliyopita,sasa sisi ni mataifa yenye fahari, na yaliyo na uhuru . Zaidi ya yote, hatima yetu iko mikononi mwetu. Na wakati huo huo, zaidi kuliko yote, ni muhimu kwetu kuwa macho dhidi ya mifumo inayoendelea kuwekwa na watu wa nje, wenye nia ya kuidhibiti hatima hiyo”.

Rais huyo wa Kenya aliupongeza Umoja wa Afrika kwa kumuunga mkono akisema “kama Rais wa Kenya, inanipa hisia za kina za majivuno ya kudumu kujua kuwa ninaweza kuutegemea Umoja wa Afrika, kunisikiliza na kunisaidia wakati wa matatizo. Afrika daima imesimama na mimi”. Bunge la Kenya tayari limepitisha mswada unaoitaka nchi hiyo ijiondoe kutoka ICC.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Abdu Mtullya