1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Aung San suu Kyi apoteza uraia wa heshima wa Canada

Admin.WagnerD28 Septemba 2018

Bunge la Canada limepiga kura kumvua uraia wa heshima aliotunukiwa kiongozi wa kiraia wa Myanmar Aung San Suu Kyi kutokana na ukimya wake dhidi ya uhalifu wanaotendewa jamii ya wachache ya waislam wa Rohingya.

https://p.dw.com/p/35dtk
Myanmar Friedensgespräche in Naypyidaw - Aung San Suu Kyi
Picha: Reuters/S.Z. Tun

Hoja ya kumuondolea uraia huo wa heshima Aung Sang Suu Kyi ilitolewa na mbunge wa upinzani Gabriel Ste Marie, ambaye amewambia waandishi wa habari kuwa uamuzi huo uliopitishwa na bunge ni ishara kubwa na ya maana.

Hata hivyo, uamuzi huo wa bunge la Canada hautakuwa na matokeo ya haraka kwa sababu uraia wa heshima hutolewa na kikao cha pamoja cha bunge na baraza la seneti na maafisa nchini humo wamesema itafaa maamuzi hayo yapitishwe na vyombo vyote viwili.

Serikali ya Myanmar haijatoa maelezo yoyote hadi sasa kuhusiana na uamuzi huo .

Serikali ya Otowwa ilimtunuku mwanaharakati huyo wa demokrasia ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel uraia huo wa heshima unaotolewa kwa nadra mwaka 2007.

Lakini heshima ya Suu kyi mbele ya jumuiya ya kimataifa imeporoka katika siku za karibuni kutoka na kushindwa kukemea kile kinachofanywa na viongozi wa kijeshi dhidhi ya jamii ya wachache ya warohingya.

Warohingya wanahofia kurejea nyumbani

Myanmar Flucht Rohingya
Picha: picture-alliance/abaca

Jeshi la Myanmar limekuwa likiendesha kampeni ya kikatili dhidi ya warohingya ambao sasa zaidi ya laki saba wamekimbilia nchi jirani ya Bangladesh wakihofia kurejea nyumbani licha ya hivi karibuni kufikiwa makubaliano ya kuwarejesha Mynamar.

Ripoti zinasema warohingya wengi wanauliwa kiholela, kubakwa na makazi yao kuharibiwa kwa kuchomwa moto. 

Jeshi la Myanmar limekana madai hayo likisema hatua yake dhidi ya warohingya ni halali katika kuwakabili wanamgambo walio kwenye jamii hiyo.

Lakini kutokana na taarifa ya ujumbe wa kutafuta ukweli nchini Mynamar, Umoja wa Mataifa umefikia uamuzi jana Alhamisi wa kuunda kamati maalum kuandaa mashatka dhidi ya mkuu wa jeshi la Myanmar na maafisa wengine kwa kutenda makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu.

Myanmar kuna mauaji ya kimbari

Malala Yousafzai zur kanadischen Ehrenbürgerin ernannt	Malala Yousafzai zur kanadischen Ehrenbürgerin ernannt	Malala Yousafzai zur kanadischen Ehrenbürgerin ernannt
Picha: Reuters/C. Wattie

Wiki iliyopita bunge la Canada pia lilipiga kura kuyataja yanayoendelea Mynamar kuwa mauaji ya halaiki uamuzi ulioungwa mkono na waziri wa mambo ya kigeni wa Canada Chrystia Freeland.

Kupitia msemaji wa wizara hiyo waziri Freeland amesema serikali mjini Otawwa inaunga mkono hoja hiyo kutokana na Suu kyi kushindwa wazi wazi kulaani uhalifu unaofanywa na jeshi la Myanmar linalodhibiti serikali ambayo Suu kyi ni miongoni mwa viongozi wake.

Freeland alikuwa miongoni mwa wanasiasa wa nchi za magharibi waliolaani uamuzi wa hivi karibuni wa mahakama moja nchini Mynamar kuwahukumu kwenda jela kwa miaka saba  waandishi habari wawili wa shirika la habari la Reuters kwa madai ya kuvunja sheria za nchi na kuvujisha siri za taifa.

Waandishi hao Wa Lone na  Kyaw Soe Oo, ambao walikuwa wanachunguza visa vya mauaji ya warohingya yaliyofanywa na  jeshi la Myanmar wamesifu uamuzi huo.

Suu kyi ni miongoni mwa watu watano pekee waliowahi kutunikiwa Uraia wa heshima wa Canada wakiwemo kiongozi wa kiroho wa Tibet Dalai Lama, mwanaharakati wa  elimu ya wasichana Malala Yousafzai na rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela.

Mwandishi: Rashid Chilumba/RTRE/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef