1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muasisi wa Zambia, Kenneth Kaunda afariki akiwa na miaka 97

Daniel Gakuba
18 Juni 2021

Mwasisi huyu mchangamfu wa Zambia aliheshimika duniani kote, lakini wakati wa utawala wake Wazambia waliteswa na umaskini na ukandamizaji utawala wa chama kimoja.

https://p.dw.com/p/3v8Xb
Kenneth Kaunda | ehemaliger Präsident Sambias
Picha: Alexander Joe/AFP/Getty Images

Wakati bendera mpya ya Zambia ilipopandishwa tarehe 24 Oktoba mwaka 1964, ndoto ya Kenneth Kaunda ilikuwa imetimia. Hatimaye Zambia ilikuwa imepata uhuru, Kaunda akiwa kinara wa uhuru huo. Hata hivyo uraia wake ulikuwa wenye utata, kwani ingawa alizaliwa nchini Zambia mwaka mwaka 1924, wazazi wa Kenneth Kaunda walikuwa kutoka nj´chi jirani ya Malawi. Baba yake alihamia Zambia kama mchungaji wa kanisa la Kiprotestanti, wakati huo nchi hizo mbili zikiwa makoloni ya Uingereza.

Mwanzoni, mtoto huyo wa mchungaji aliajiriwa kama mwalimu, kazi kubwa kwa mwafrika wakati huo, kwa sababu ajira bora na biashara lilikuwa eneo la wazungu pekee. Kaunda hakukubali mipaka hiyo, na aliingia katika siasa, hatua iliyomsababishia kufungwa jela mara kadhaa. Alimudu kuiongoza nchi yake kupata uhuru, na katika uchaguzi wa kwanza chama chake cha United National Independence Party kilishinda kwa kishindo.

Lakini kazi kubwa zaidi ilikuwa ikimsubiri baada ya uhuru. Kaunda mwenyewe aliwahi kuiambia DW katika mahojiano, kwamba ''ilikuwa muujiza kuwa Zambia iliendelea kusimama kama taifa, kwa kutilia maanani changamoto chungu nzima walizokuwa wakikabiliwa nazo.''

Sababu ni kwamba Zambia inayo makabila zaidi ya 75, ambayo mbali na mipaka iliyochorwa na wakoloni, hakuna kitu kingine kilichoyaunganisha. Kati ya Wazambia milioni 3.5 wakati huo, wapatao 100 tu ndio walikuwa wamepata elimu ya chuo kikuu. Wengi wa raia wake waliishi katika lindi la umaskini.

Sambia Lusaka | Kenneth Kaunda
Kaunda akikagua gwaride la jeshi mara tu baada ya Zambia kupata uhuruPicha: Central Press/Hulton Archive/Getty Images

Siasa ya Utu wa Zambia na mfumo wa chama kimoja cha siasa

Kaunda alifanikiwa kuiunganisha Zambia. Kama Kwame Nkrumah wa Gahana na Julius Nyerere wa Tanzania, alitumia siasa ya Utu wa Zambia kuiunganisha jamii. Siasa hiyo ilikuwa mseto wa maadili ya ukristo, tamaduni za kiafrika na misingi ya Usoshalisti.

Katika mahojiano na DW, Kaunda walisema alisisitiza umuhimu wa mahitaji ya kiroho, akisema ukosefu wa amani unatokana na watu kuzingatia tu mahitaji ya kimwili.

Uchangamfu wake, na hotuba zilizosheheni nukuu za biblia na mitazamo ya kifalsafa vilimjengea heshima kote duniani. Hayati Friedrich Stenger, kasisi wa kikatoliki aliyeishi nchini Zambia kwa miaka mingi, aliiambia DW mwaka 2017 kuwa ''Kaunda alikuwa baba wa taifa, ambaye alibakia kuwa mnyenyekevu, bila tamaa yoyote ya kutukuzwa.''

Rais Kaunda pia aliheshimiwa kwa mchango wake katika usuluhishi wa mizozo ya kikanda, na katika vita vya ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika.

Kaunda ashindwa uchaguzi, Wazambia wajawa na furaha

Lakini pia kama viongozi wengi wa kiafrika, Kaunda alijua namna ya kung'ang'ania madarakani, akiigeuza Zambia kuwa na utawala wa chama kimoja. Kasisi Stenger aliiambia DW kuwa wakati wa utawala wake vyombo vya usalama vilitumia mbinu za kikatili kuzima harakati za upinzani.

Kuba | Sambias Präsident Kaunda und Fidel Castro
Kenneth Kaunda akikutana na Fidel Castro wa CubaPicha: Rafael Perez/AFP

Wakati Zambia iliporudi katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, Kaunda alishindwa katika uchaguzi wa mwaka 1991, na akakubali kushindwa. Serikali iliyofuata ilimfanyia unyanyasaji mkubwa, na kumtangaza kuwa raia wa nchi ya kigeni. Mrithi wake Frederich Chiluba alidiriki hata kutaka kumfuza Kaunda kutoka Zambia, lakini alizuiliwa na maandamano ya wananchi walioipinga hatua hiyo.

Ndoto ya Kenneth Kaunda kisiasa ilikuwa bado haijafa kabisa, kwani mwaka 4996 aliazimia kugombea tena urais, lakini Chiluba alifanya alimuengua kwa ujanja, baada ya kubadilisha katiba, na kuweka kipengele kinachowaruhusu tu watu ambao wazazi wao walizaliwa Zambia kugombea cheo hicho cha juu zaidi nchini.

Aachana na siasa na kujikita katika mapambano dhidi ya UKIMWI

Kaunda alistaafu shughuli za kisiasa na kujikita katika mapambano dhidi ya maradhi ya ukimwi. Kupitia wakfu aliouanzisha, alipigana kuondoa unyanyapaa dhidi ya janga hilo ambalo alisema lisipoangaliwa kwa makini lingeweza kuiangamiza Zambia na Afrika nzima.

Zambia ehem. Präsident Kenneth Kaunda
Mzee Kenneth Kaunda amefariki akiwa na umri wa miaka 97Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Mwape

Mwaka 1987 alikiri hadharani kuwa mwanaye alikufa kutokana na maradhi hayo, wakati ambapo ilikuwa bado ni kama mwiko kuzungumza wazi wazi kuhusu gonjwa hilo lililotia hofu.

Kenneth Kaunda alipelekwa hospitalini Jumatatu wiki hii akiwa na ugonjwa niumonia, na alifariki alasiri ya Alhamisi. Serikali mjini Lusaka imetangaza siku 21 za msiba wa kitaifa kuomboleza kifo cha kiongozi huyo aliyepigania uhuru wa taifa.

Wakati wa miaka ya mwisho wa uhai wake, Kenneth Kaunda na mke wake waliishi maisha ya kawaida kabisa katika mji mkuu, Lusaka.

Imetafsiriwa kutoka makala ya Kijerumani, iliyoandikwa na Martina Schwikowski