1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bado wiki mbili kabla ya ligi ya Uingereza kunguruma

Sekione Kitojo2 Agosti 2010

Wiki mbili zimesalia kabla ya kuanza kwa ligi kuu ya Uingereza, premier League na mashindano ya ubingwa wa riadha barani Afrika na Ulaya yamalizika.

https://p.dw.com/p/OaLz
Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson akishangilia baada ya timu yake kuishinda AC Milan katika champions league.Picha: AP
Wiki  mbili  zimesalia  hadi  viwanja  kutimua vumbi  katika  ligi  kuu  ya  Uingereza, Premier League,  na mashindano  ya  ubingwa  wa  riadha   kwa  bara  la  Afrika na  hapa  Ulaya  yamalizika  huko  Nairobi, Kenya  na Barcelona  Uhispania.

Tuanze  na  soka.

Ikiwa  zimesalia  wiki  mbili  hadi  kuanza  kwa  msimu mpya  wa  soka   katika  premier  League  nchini Uingereza, mabingwa   Chelsea  na Manchester  United ambazo  ni  timu  zinazoonekana  kuwania  ubingwa  wa msimu  huu zinajitayarisha   kwa  dhidi  ya  upinzani mkubwa  kutoka  kwa  Manchester  City  ambayo  imetumia fedha  nyingi  kuwapata  mastaa  kadha.

Wakati  kocha  wa  Chelsea  Carlo  Ancelotti  na   bosi  wa Manchster  United Sir  Alex Ferguson  wameridhika  na   kufanya mabadiliko  madogo  katika  vikosi  vyao, meneja  wa Manchester City  Roberto  Mancini  amekuwa akiwakaribisha  mastaa  wapya.

Mancini  ametumia  kitita  cha  pauni  milioni  80  kwa wachezaji  wanne, Yahya  Toure  kutoka  Barcelona, mchezaji  wa  pembeni  David  Silva  kutoka   Valencia, Alexander  Kolarov  kutoka  Lazio  Rome  na  mlinzi Jerome  Boateng  kutoka  Hamburg SV.

Matumizi  ya  fedha  nyingi  hayaonekani  kuishia  hapo kwani  Mancini  anatamani  kuwapata  Mario  Baloteli kutoka   mabingwa  wa   kombe  la  champions  league Inter  Milan  na  pia  anatafuta  saini  ya  James  Milner  wa Aston  Villa.

Huko  nchini  Ufaransa  msimu  unaanza  rasmi  Jumamosi ijayo  huku  wachezaji  pamoja  na  mashabiki  wakitambua wazi  kuwa  kuna  haja  ya  mabadiliko  makubwa   kuweza kuiweka  vizuri   hadhi  ya  soka  la  nchi  hiyo  baada  ya kampeni  iliyoleta  maafa  ya  kombe  la  dunia nchini  Afrika kusini.

Timu  ya  taifa  ilikumbana  na  wakati  mgumu  uwanjani , ikipoteza  michezo  miwili   kati  ya  mitatu  katika  kundi lake  na  kutoka  sare  mmoja.

Wachezaji  wanajiweka  tayari  kwa  ghadhabu  ya mashabiki  wa  nchi  hiyo  kutokana  na  vituko vilivyoonyeshwa  na  timu  hiyo  huko  Afrika  kusini  ikiwa ni  pamoja  na  mgomo  wa  siku  moja  kufanya  mazowezi.

Kocha  wa  Liverpool  ya  Uingereza  Roy  Hodgson  amekiri jana  Jumapili  kuwa  ana  wasi  wasi  na  kuwapo  tayari kwa  timu  yake  wakati  wa  kuanza  Premier  League.

Hodgson  aliweza   kumuingiza  kikosini  Joe  Cole  aliyetia saini  kuichezea  timu  hiyo  majira  haya  ya  joto, pamoja na  mchezaji  mwenzake  katika  timu  ya  taifa  Steven Gerrard, Jamie  Carragher  na  Glen  Johnson  kwa  mara ya  kwanza   jana  Jumapili  wakati  timu  hiyo  ilipolala  kwa bao  1-0  dhidi  ya  Borussia  Moenchengladbach  katika mchezo  wa  kirafiki. Lakini  kocha  huyo  amesema  kuwa ilikuwa  vigumu  sana  kujitayarisha  kwa  ajili  ya  msimu mpya  kutokana  na  wachezaji  wake  wazoefu kutokuwapo  kambini.

Kocha  wa  Chelsea Carlo  Ancelotti  amesisitiza   leo  kuwa klabu  yake  haitamuuza  kamwe  mlinzi  wa  pembeni kushoto  Ashley Cole, ambaye  anahusishwa  na  kwenda katika  timu  ya  Real  Madrid, ambayo  hivi  sasa inafunzwa  na  kocha  wa  zamani  wa  Chelsea  Jose Mourinho. Ripoti  zinasema  kuwa  Mourinho, ambaye alikuwa  karibu  sana  na  Cole  wakati  akiifunza  timu  hiyo ya  Uingereza   ya  Stamford  Bridge, yuko  tayari  kutumia fedha  nyingi  kumpata  mlinzi  huyo.

Naye  meneja  wa   Everton  David  Moyes  amekiri  jana Jumapili  kuwa  nyota  wa  timu  ya  taifa  ya  Marekani Landon  Donovan  huenda  akawa   ghali  sana  kwa  timu yake   kuweza   kumpata  tena  kwa  mkopo  kuja kuchezea  timu  hiyo  ya  Goodison  Park.

Donovan  alikaa  kwa  muda  wa  miezi  mitatu  na  klabu hiyo  ya  premier League  mwanzoni  mwa  mwaka  huu  na mchezaji  huyo  mwenye  umri  wa  miaka  28 amedokeza kuwa  atakubali  kurejea.

Carles Puyol  ametangaza  jana  Jumapili  kuwa ataendelea  kuichezea  timu  ya  taifa  ya  Hispania  kwa muda  wa  miaka  miwili  zaidi, hadi   fainali  za   kombe  la mataifa  ya  Ulaya   zitakazofanyika  mwaka  2012. Puyol mwenye  umri  wa  miaka  32  alidokeza  baada  ya  ushindi wa  Hispania  katika  kombe  la  dunia  Julai  mwaka  huu kuwa  huenda  akajiuzulu  kutoka  timu  ya  taifa.

Nicolas Anelka  aliingia  uwanjani  kwa  mara  ya  kwanza jana   tangu  pale  alipofungishwa  virago  kutoka  katika timu  ya  taifa  ya  Ufaransa   huko  Afrika  kusini  lakini alishindwa  kuzuwia  kipigo  cha  bao  2-1  dhidi  ya Eintracht  Frankfurt  jana  katika  mchezo  wa  kifariki  mjini Frankfurt.

Na  huko  katika  bara  la  Afrika  vigogo   wa  soka  barani Afrika  Enyimba  ya  Nigeria  imeshindwa  kutoroka  mara hii  baada  ya  kubanwa  na  Zanaco  ya  Zambia   na kutolewa  katika  kinyang'anyiro  cha  kuwania   ubingwa wa  bara  la  Afrika. Ikihitaji  magoli  manne  bila  majibu katika  ngome  yao  ya   mjini  Aba  ili  kulazimisha mikwaju  ya  penalti  dhidi  ya  mabingwa  hao  wa  Zambia Zanaco, Enyimba   ilimudu  tu  ushindi  wa   mabao  2-0. Mabingwa  hao  wa  Zambia  wamesonga  mbele  kwa jumla  ya  mabao 4-2.

Lakini  SuperSport  ya  Afrika  kusini  imeendelea  kudorora wakati  ilipoteleza  kwa  bao  1-0  dhidi  ya  FUS Rabat   ya Morocco. Sfaxien  imefanikiwa  nayo  kusonga  mbele  kwa mabao  3-1  dhidi  ya  Petro Atletico  ya  Angola, na  Al Hilal ya  Sudan  nayo  ilifanikiwa  kuingia  katika  ligi  hiyo  ya mabingwa  ngazi  ya  ligi  ndogo  baada  ya  kuishinda CAPS  ya  Zimbabwe  kwa  mabao  3-1  mjini  Harare.

Nayo  Al Ahly  ya  Misr  ilipata  ushindi  wa  mabao  2-1 dhidi  ya  Ismailia  pia  ya  Misr  katika  pambano lililofanyika  mjini  Cairo, wakati  JS Kayblie ya  Algeria inaongoza  kundi  lao  baada  ya  kuishinda  Heartland  ya Nigeria  kwa  bao  1-0  katika  mji  wa  Tizi-Ouzou  hapo kabla.

Argentina   haijamtafuta  mrithi  wa   kiti  cha  ukocha  wa timu  ya  taifa  ya  nchi  hiyo  kufuatia   kuondoka  kwa Diego  Armando  Maradona, amesema  meneja  Carlos Bilardo  jana.

Julio  Grondona  rais  wa   shirikisho  la  kandanda   nchini Argentina  hajazungumza  na   mtu  yoyote  na hajaniambia  kitu  chochote, amesema  Bilardo. Tunasubiri. Kitu  chochote  kinaweza  kutokea.

Na  Mdachi  Han Berger  anatarajiwa   kuchukua  hatamu za  kuifunza  Australia  kwa  ajili  ya  mchezo  wa  kirafiki wa  nchi  hiyo  mwezi  huu  dhidi  ya  Slovenia, limesema shirikisho  la  kandanda  la  Australia  leo.

Mkurugenzi  wa  ufundi  wa  kikosi  hicho  cha  soccerroos amepandishwa  cheo  na  kujukua  wadhifa  wa  meneja wa  mpito  wakati  shirikisho  hilo  linaangalia  njia  ya kumteua  mtu  mwingine  kuchukua  nafasi  ya  kocha  wa zamani  Pim Verbeek , ambaye  ameondoka  baada  ya fainali  za  kombe  la  dunia  mwaka  huu  huko  Afrika kusini.

FIFA  imewapatia   maafisa  wa  chama  cha  kandanda nchini  Iraq  mwaka  mmoja  zaidi  kuwapo  madarakani wakijitayarisha   kwa  uchaguzi  wa  chama  hicho, baada ya  mizozo  wa  kimadhehebu  na  kusababisha   shirikisho hilo  kushindwa  kufanya  uchaguzi  kwa  ajili  ya  viongozi wapya.

Uamuzi  wa  FIFA  uliotolewa  leo  una  maana  unaondoka kitisho   cha  Iraq  kuondolewa  uanachama  kutoka  katika shirikisho  hilo  la  kandanda  duniani  na  kuiruhusu  timu ya  taifa  kujitayarisha  kutetea  ubingwa  wake  wa  bara  la Asia Januari  mwakani.

Na  sasa  ni  riadha:

Christophe Lemaitre  amekuwa   mtu  wa  kwanza   kuwa bingwa  wa  michezo  mitatu  ya  ubingwa  wa  riadha barani  Ulaya  akishinda  mbio  za  mita  100, 200  na 100 kupkezana  vijiti  lakini  juhudi  zake  hazikutosha   kuiweka Ufaransa  juu  ya  Urusi  katika  oridha  ya  medali  jana.

Urusi  ilimaliza   mashindano  hayo  ikiwa  ya  kwanza  kwa kunyakua  medali  10  za  dhahabu, mbili  zaidi  ya Ufaransa , ambayo  imepata  medali  8  na  Uingereza ikiwa  ya  tatu  kwa  kupata  medali  6  za  dhahabu.

Ujerumani  imechukua  nafasi  ya  4  ikiwa  na  medali  4 za  dhahabu, sita  za  fedha   na  6  za   shaba.

Na  hadi  kufikia  hapo  ndio  sina  budi  kusema tunaufunga  ukurasa  wetu  huu  wa  michezo  mwishoni mwa  juma. Mimi  ni  Sekione Kitojo  hadi  mara  nyingine kwaherini.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre/afpe/dpae

Mhariri:Josephat Charo