1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD : Iraq na Syria zarudisha uhusiano wa kibalozi

21 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCqh

Iraq na Syria hapo jana zimekubali kurudisha uhusiano kamili wa kibalozi baada ya kutokuwepo kwa uhusiano huo takriban kwa robo karne hatua ambayo Iraq inataraji yumkini ikasaidia kukomesha kile inachosema kuwa ni uungaji mkono wa Syria kwa wanamgambo.

Waziri wa mambo ya nje wa Syria Walid al Moualem akifanya ziara ya kwanza kabisa kuwahi kufanywa na waziri wa Syria nchini Iraq tokea uvamizi uliongozwa na Marekani kwa nchi hiyo hapo mwaka 2003 amesaini makubaliano na waziri mwenzake wa Iraq Hishiyar Zebari ambapo kwayo wamekubali kwamba vikosi vya Marekani viendelee kubakia nchini humo kwa hivi sasa.

Moulaem awali alitaka kuwekwa kwa ratiba ya kuondolewa kwa wanajeshi 140,000 wa Marekani walioko nchini humo.

Waraka huo una maudhui yaliotumiwa na serikali za Iraq na Marekani kwamba vikosi hivyo vinapaswa kuondoka kwa awamu mara vitakapokuwa havihitajiki tena.

Wakati huo huo imefahamika kwamba Rais Jalal Talabani wa Iraq anatarajiwa kwenda Tehran mwishoni mwa juma hili kwa mazungumzo na Rais Mahmoud Ahmedinejad wa Iran.

Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kwamba Rais Bashar al Assad wa Syria huenda akajiunga na mazungumzo hayo mjini Tehran lakini maafisa wa serikali ya Iraq wamekanusha taarifa hizo.