1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD:Mahafidhina 50 wakisunni wauawa nchini Iraq na majeshi ya Marekani

10 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCc2

Wizara ya Ulinzi ya Iraq imesema kuwa majeshi ya nchi hiyo yakisaidiwa na yale ya Marekani yamewaua wapiganaji wa kisunni 50, katika mapigano yaliyotokea katikati mwa Baghdad.

Kiasi cha cha wapiganaji 20 wa kisunni walikamatwa katika mapigano hayo yalitokea kwenye mtaa wa Haifa jijini Baghdad, ambao unakaliwa na wasunni.

Mapigano hayo yalizuka baada ya wapiganaji wa kisunni kuwashambulia askari wa Iraq, ambao baadaye waliomba msaada kutoka kwa askari wa Marekani.

Mapigano hayo yametokea saa chache baada ya Waziri Mkuu wa Iraq, Nour al Maliki kuahidi hatua kali dhidi ya makundi haramu ya kiharamia.

Rais George Bush wa Marekani leo hii anatarajiwa kuelezea mikakati yake mipya nchini Iraq, ikiwa ni pamoja na kuongeza askari elfu 20 nchini Iraq.

Afisa mmoja wa ngazi ya juu katika Wizara ya Ulinzi ya Marekani amenukuliwa akisema kuwa kundi la kwanza la askari hao linatarajiwa kwenda Iraq kabla ya mwisho wa mwezi huu.

Lakini wabunge wengi wa Democratic ambao kwa sasa ndiyo wenye idadi kubwa katika bunge la Marekani, wanapinga mpango huo.

Katika hatua nyingine watu 34 wamekufa baada ya ndege waliyokuwa wakisafiria kwenda Iraq kuanguka kaskazini mwa Baghdad.

Ndege hiyo ilikuwa ikitokea Uturuki na wafanyakazi wa kazi za ujenzi, ambapo ilianguka kutokana na ukungu mkubwa wakati ilipokuwa ikitua.