1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Balozi za Marekani kuendelea kufungwa

5 Agosti 2013

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani, imesema kuwa balozi zake katika miji 19 ya Mashariki ya Kati pamoja na Afrika, zitaendelea kufungwa hadi tarehe 10 ya mwezi huu wa Agosti.

https://p.dw.com/p/19Jnd
Ubalozi wa Marekani, mjini Sanaa, ukiwa umewekwa vizuizi
Ubalozi wa Marekani, mjini Sanaa, ukiwa umewekwa vizuiziPicha: picture-alliance/dpa

Balozi hizo zitafungwa kutokana na kuwepo taarifa kwamba mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda unaweza ukazishambulia balozi hizo.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Jen Psaki, amesema kuwa uamuzi wa kuzifunga balozi hizo hadi Jumamosi ijayo, unatokana na kile alichokiita kuchukua tahadhari na sio kwamba pametolewa vitisho vipya vya kufanyika kwa mashambulizi mengine.

Mmoja wa viongozi wa Al-Qaeda, Said al-Shihri
Mmoja wa viongozi wa Al-Qaeda, Said al-ShihriPicha: picture alliance/AP Photo

Psaki, amesema kuwa hatua hiyo ni kwa ajili ya kuwalinda wafanyakazi wa balozi hizo wakiwemo wale wa Marekani na raia wa nchi husika pamoja na kuwalinda wageni wanaozitembelea balozi hizo.

Amesema kuwa balozi zitakazoendelea kufungwa ni pamoja na zile zilizoko kwenye miji ya Abu Dhabi, Amman, Cairo, Riyadh, Dhahran, Jedda, Doha na Dubai. Balozi nyingine ni zile zilizopo, Kuwait, Manama, Muscat, Sanaa, Tripoli, Antananarivo, Bujumbura, Djibouti, Khartoum, Kigali na Port Louis.

Balozi kadhaa zafunguliwa tena leo (05.08.2013)

Hata hivyo, Marekani imezifungua tena hii leo balozi zake za Afghanistan, Algeria, Bangladesh, Mauritania, Iraq na Israel. Balozi hizo zilifungwa jana Jumapili (04.08.2013), kwa sababu za kiusalama.

Jumamosi iliyopita, Serikali ya Rais Barack Obama, ilitangaza hatua ya kuzifunga balozi zake mwishoni mwa juma lililopita kwa sababu za kiusalama, na pia kutoa tahadhari kwa raia wake kutosafiri, ikionya kuwa Al-Qaeda au washirika wake wanaweza kuwalenga maafisa wa Marekani au raia wa nchi hiyo.

Rais wa Marekani, Barack Obama
Rais wa Marekani, Barack ObamaPicha: REUTERS

Tahadhari hiyo iliwataka raia wake kuwa makini zaidi katika safari zao nje ya nchi, ikibainisha kuwa mashambulio hayo yanaweza kufanywa katika sehemu za umma na hasa kwenye usafiri na vituo vya kitalii.

Aidha, kwa mujibu wa tahadhari hiyo, mashambulio ya kigaidi yaliyowahi kufanyika, yametokea kwenye usafiri wa treni za chini kwa chini, treni za kawaida, ndege pamoja na boti.

Raia wa Marekani watakiwa kujisajili

Raia wote wa Marekani wanaosafiri nje ya Marekani, wametakiwa kujisajili kwenye balozi na balozi ndogo za Marekani katika nchi wanazokwenda na kwamba tahadhari hiyo itamalizika tarehe 31 ya mwezi huu wa Agosti.

Aidha, wabunge wa Marekani, wamesema wameichukulia tahadhari hiyo ya kijasusi kama muhimu kabisa kuwahi kutolewa katika miaka ya hivi karibuni.

Tahadhari hiyo ya kijasusi ilisababisha pia mataifa kadhaa ya Ulaya kuzifunga balozi zake huko Yemen jana Jumapili na leo Jumatatu.

Nchi hizo ni pamoja na Uingereza, Ujerumani na Ufaransa. Viongozi wa Uingereza wamesema kuwa baadhi ya wafanyakazi wake katika ubalozi wa Yemen, wameondolewa kutokana na sababu za kiusalama.

Rais wa Interpol, Khoo Boon Hui
Rais wa Interpol, Khoo Boon HuiPicha: picture-alliance/dpa

Katika hatua nyingine, Polisi wa Kimataifa-Interpol, pia limetoa tahadhari ya usalama wa dunia kutokana na kuhusika kwa Al-Qaeda katika matukio kadhaa ya hivi karibuni ya kutoroka kwa wafungwa, ikiwemo katika magereza ya Iraq, Libya na Pakistan.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE,AFPE
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman