1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barack Obama amshinda Hilary Clinton

Nijimbere, Gregoire4 Juni 2008

Mbio za kuwania tikiti ya kukiwakilisha chama cha demokrate kwenye uchaguzi wa urais ujao nchini Marekani, zimekwisha jana kwa ushindi wa Barack Obama licha ya kwamba hajatangazwa rasmi mshindi.

https://p.dw.com/p/EDdO
Barack Obama mbele ya halaiki ya watuPicha: AP

Barack Obama na Hilary Clinton waligawana ushindi katika majimbo mawili ya mwisho ya Dakota ya kusini na Montana. Obama alipata ushindi katika jimbo la Montana huku Hilary Clinton akinyakuwa ushindi Dakota ya kusini. Lakini matokeo hayo hayakubadili muelekeo wa uchaguzi huo ndani ya chama cha demokrate kwani Barack Obama alimaliza akiwa na wajumbe 2156 ikiwa ni zaidi ya wale 2118 wanaohitajika kuweza kuchaguliwa kukiwakilisha chama.


Hilary Clinton hajaungama kuwa ameshindwa na kusema kwamba anasubiri ushauri kutoka kwa mafisa wa chama wanaomuunga mkono na hapo ajuwe la kufanya, kukiwa na uwezekano wa kuendelea na kampeni yake hadi mkutano mkuu wa chama mjini Denver mwezi Agosti mwaka huu ambao utampitisha rasmi muakilishi wa chama kwenye uchaguzi wa urais ifikapo mwezi Novemba mwaka huu. Lakini tayari ushindi wa Barack Obama umezusha hamasa kwamba kutatokea mabadiliko makubwa nchini Marekani.

Hata muakilishi wa chama cha republikan kwenye uchaguzi huo wa urais ujao, John Mc Cain amekiri kuwa kutakuwa na mabadiliko makubwa ingawa bado anajitetea:

"Huu ni uchaguzi utakaoleta mabadiliko. Uongozi wa nchi utabadilika sana bila kujali atakayeshinda kwenye uchaguzi. Lakini chaguo litakuwa kati ya mabadiliko mazuri na mabadiliko mabaya".


Kwa jumla nchi bado zimejizuwia kutoa maoni ila baadhi ya mwanasiasa tayari wameanza kujitokeza. Mfano ni Karsten Voigt anayesimamia serikali kuu ya Ujerumani kuhusu uhusiano kati ya Marekani na Ujerumani ambae hakutarajia ushindi wa Barack Obama:

" Awali nilikuwa na utabiri mwingine. Lakini wamarekani wanataka mabadiliko, ukurasa mpya. Ndio sababu kwamba ameshinda ingawa alianza kampeni akiwa na pesa kidogo"


Magazeti na vyombo vya habari kwa jumla nchini Marekani vimezungumzia ushindi huo wa Barack Obama na kuutaja kuwa ni wa kihistoria. Gazeti la Washington Post limeandika kwamba "ushindi wa Obama umeiwezesha Marekani kuvuka kikwazo na kuleta ishara ya maendeleo juu ya swala la ukabila"

Gazeti la New York Times nalo pia limechapisha kuwa "ushindi wa Obama umevunja vizingiti vya kikabila na kudhihirisha kupanda ngazi kwa mtu miaka minne tu iliopita alikuwa seneta wa kawaida wa jimbo la IIlinois"

Na taarifa kutoka Afrika zinasema kuwa wakaazi wa magharibi mwa Kenya eneo la asili la Baba yake Barack Obama, wamefurahishwa na ushindi huo wa Obama.

Na akizungumza juu ya matokeo hayo kwamba Barack Obama atakuwa mueusi wa kwanza kukiwakilisha chama cha demokrate, waziri wa Marekani wa mambo ya kigeni Condoleeza Rice amesema hivi karibuni kuwa huo ni ushahidi kuwa Marekani kunatendeka mambo yasiokuwa ya kawaida.