1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza jipya la mawaziri laundwa nchini Kenya

Andrea Schmidt14 Aprili 2008
https://p.dw.com/p/DhKL

Hatimae kimya cha muda mrefu nchini Kenya kimeondoka. Serikali na upinzani zimeafikiana juu ya baraza la mawaziri. Mvutano wa wiki kadhaa tangu makubaliano ya kugawana madaraka yalipotiawa saini, umetishia kuzusha wimbi jipya la machafuko na kulididimiza zaidi taifa hilo.

Shinikizo zito la kimataifa kutoka Marekani na nchi za Ulaya, hatimae limewaleta pamoja wanasiasa wa vyama vyote. Lakini yote haya ni kwa gharama gani ?

Kwa hakika baraza la mawaziri 40 kwa nchi hii ya Afrika mashariki ni kubwa . Ni baraza kubwa kabisa nchini humo tangu uhuru wake 1963.

Upinzani pia haukufanikiwa katika jitihada za kutaka baraza hilo lipunguzwe na hivyo kuridhia kuweko na mawaziri 20 kutoka upande wa Rais Kibaki na 20 upande wa upinzani, huku Kibaki akibakia na wizara muhimu kama fedha, mambo ya nchi za nje, sheria na ulinzi.

Ni madaraka ya kiasi gani hasa atakua nayo waziri mkuu mteule Raila Odinga pia si jambo lilo wazi. Kwa upinzani kwa hivyo ni maridhiano machungu.

Wakenya wengi wanakubaliana na shaka shaka aliyonayo mshindi wa tunzo ya amani ya nobeli Wangari Mathai, kwamba kulikua na uwezekano wa kuwa na baraza dogo la mawaziri ambalo lingeweza kuwajibika barabara.

Mshahara wa waziri nchini Kenya ni karibu euro 11.000 kwa mwezi mbali na ule wa euro 9.000 kama mbunge, huku mshahara wa waziri mdogo ukiwa euro 10.000 mbali na marupurupu. Ni maridhiano ya gharama kubwa mno na katika nchi ambayo 60 asili mia ya wakaazi wake wanaishi kwa pato la chini ya dola moja kwa siku.

Linabakia suali la kuuliza jinsi gani walipa kodi nchini Kenya wataweza kuugharimia mzigo huu, katika wakati ambao inakabiliwa na ukosefu wa utulivu panapohusika na suala la ardhi na juhudi za kutaka kuimarisha utalii baada ya msukosuko ulioikumba baada ya uchaguzi.

Suali jengine ni vipi baraza jipya la mawaziri litaweza kuyatatua matatizo ya taifa hilo, na wanasiasa kuweza kurudisha imani ya wapiga kura.

Miongoni mwayo ni marekebisho ya umilikaji ardhi, katika sheria pamoja na hali ya kunufaika watu wa makabila na mikoa fulani tu.

Vita dhidi ya rushwa na haki za kijamii kwa wote ni muhimu kwa utulivu wa Kenya na pia kwa utulivu wa eneo zima la Afrika mashariki.