1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la kijeshi Sudan lasema liko tayari kuzungumza tena

Iddi Ssessanga | Bruce Amani
5 Juni 2019

Mkuu wa baraza la kijeshi la Sudan amesema baraza hilo liko tayari kwa majadiliano kuhusu mustakabali wa taifa hilo, siku moja baada ya kuyasimamisha. Amesema wako tayari kuzungumza kwa maslahi ya kitaifa na mapinduzi.

https://p.dw.com/p/3Jrdi
BG Sudan Proteste
Picha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Luteni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan ametoa matamshi hayo katika ujumbe wa sherehe ya Eid al- Fatr, siku moja baada ya kutangaza kwamba baraza la mpito MTC limefuta makubaliano yote na muungano wa waandamanaji na makundi ya upinzani, na badala yake walikuwa wanakwenda kwenye uchaguzi wa taifa katika kipindi cha miezi tisa.

"Sisi katika Baraza la Kijeshi tunafungua mikono yetu kwa majadiliano bila vikwazo vyovyote zaidi ya maslahi ya kitaifa ya kuendelea kujenga mamlaka halali inayoakisi malengo ya mapinduzi ya Sudan kwa kila njia," alisema Burhan katika hotuba kupitiatelevisheni ya taifa.

Idadi ya vifo yafika 60

Kamati kuu ya madaktari wa Sudan, imesema idadi ya waliouawa katika ukandamizaji wa kijeshi imepanda na kufikia watu 60, na kwamba zaidi ya 300 walijeruhiwa, ingawa imekuwa vigumu kubainisha hasa idadi ya waliojeruhiwa kwa sababu baraza la kijeshi limezima mawasiliano ya intaneti katika maeneo mengi ya nchi.

BG Sudan Proteste
Mwandamanaji akiwa amevaa bendera ya Sudan mbele ya matairi yanayowaka moto mjini Khartoum, Juni 3, 2019.Picha: picture-alliance/AP Photo

Idadi ya awali ya waliouawa ilikuwa 40, lakini kamati ya madaktari inasema vikosi vya usalama viliuwa watu wasiopungua 10 mapema Jumatano katika mji mkuu Khartoum na mji wake pacha wa Omdurman.

Hii ni baada ya watu wengine 10 kuuawa siku ya Jumanne, wakiwemo watano katika jimbo la White Nile, watatu mjini Omdurman na wawili katika kiunga cha Bahri mjini Khartoum.

Wahalifu kuwajibishwa bila kujali nafasi zao

Viongozi wa upinzani wameutaja ukandamizaji wa jeshi kuwa uhalifu dhidi ya ubinadamu na kukosoa pia mpango wake wa kuitisha uchaguzi wa mapema.

"Mapambano sasa ni dhidi ya Baraza la Kijeshi, linalozuwia malengo ya watu wa Sudan na kupinga utawala wa kiraia. Hakuna mhalifu ataekwepa adhabu ya uhalifu wote uliotendeka katika miezi mwili iliyopita, bila kujali wadhifa wake," alisema Omar al-Dukair, katibu mkuu wa chama cha Congress.

Wanaharakati wamesema mapambano ya mitaani yameendelea Jumanne jioni na mapema leo katika wilaya za Bahri na Buri za mji wa Khartoum kati ya waandamanaji wa vikosi vya usalama.

BG Sudan Proteste
Wafuasi wa Baraza la kijeshi wakiwa na bango lenye picha ya Jenerali Abdel Fattah al-Burhan (kulia) na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo "Hamidati" likiwa na maandishi yamesemayo: TMC ndiyo mlinzi wa mapinduzi.Picha: Getty Images/AFP/A. Shazly

China, Urusi zazuwia azimio la Umoja wa Mataifa

Ukandamizaji huo wa kijeshi umekosolewa vikali na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika na waangalizi wengine. Hata hivyo azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kulaani hali hiyo lilipigiwa kura ya turufu hapo jana na China, ikiungwa mkono na Urusi.

Azimio hilo lililowasilishwa na Uingereza na Ujerumani katika kikao cha faragha cha baraza hilo, lilikuwa linawatolea mwito watawala wa kijeshi na waandamanaji kuendelea kushirikiana kuelekea kuutafutia suluhisho mgogoro wa sasa, kulingana na mswada wake.

Lakini China ilipinga kwa nguvu zote maandishi yake, huku Urusi ikisisitiza kuwa baraza linapaswa kusubiri jibu kutoka Umoja wa Afrika. Naibu balozi wa Urusi Dmitry Polyanskiy alisema taatifa hiyo iliyopendekezwa haikuwa na urari na kusisitiza haja ya kuwa waangalifu kwa waakti huu.

Vyanzo: mashirika