1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini mema yachomoza

27 Februari 2015

Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa linakutana kwa dharura kuzungumzia mzozo wa Ukraine katika wakati ambapo hali inadhihirika kuimarika katika uwanja wa mapigano mashariki ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/1EibU
Baraza la usalama la Umoja wa mataifaPicha: Reuters/Carlo Allegri

Kikao hicho cha dharura cha baraza la usalama kimeitishwa na Ufaransa na Ujerumani.Ni kikao cha kwanza kuitishwa na baraza la usalama la Umoja wa mataifa kuhusu Ukraine tangu makubaliano ya amani ya Minsk yalipotiwa saini february 17 iliyopita kati ya Ukraine,Urusi,Ufaransa na Ujerumani.

Mabalozi wa nchi tano wanachama wa baraza la usalama watasikiliza ripoti za maafisa wa shirika la usalama na ushirikiano barani Ulaya-OSCE wanaochunguza kama makubaliano hayo yanaheshimiwa.Baadae kitafuata kikao cha siri cha baraza hilo.

Silaha nzito nzito zaondolewa katika uwanja wa mapigano

Katika uwanja wa mapigano mashariki ya Ukraine,serikali ya mjini Kiev imeanza kuziondowa silaha zake nzito nzito.Ripota wa shirika la habari la Ufaransa-AFP amesema ameiona mizinga isiyopungua 15 ikikokotwa na zana maalum za kijeshi na kufuatwa na dazeni kadhaa ya wanajeshi wa Ukraine waliokua wakiuhama mji wa Artemivsk,umbali wa kilomita 55 kaskazini ya ngome ya waasi Donetsk.

Ukraine Soldaten Artemivsk
Wanajeshi wa Ukraine waondoka ArtemivskPicha: Reuters/Gleb Garanich

"Ukraine imeshaanza kuhamisha silaha zake nzito nzito toka uwanja wa mapigano" uongozi wa kijeshi wa Ukraine umethibitisha.

Awamu hiyo ya kwanza itadumu masaa 24 na kufuatiwa na opereshini ya kuondowa vifaa vya kufyetulia makombora na silaha nyengine nzito nzito-amefafanua msemaji wa kijeshi Anatoli Stelmakh.

Kwa upande wake kiongozi wa jamhuri iliyojitangaza wenyewe ya Donetsk,Alexandre Zakhartchenko amethibitisha vikosi vyake vimeshaondowa asili mia 90 ya silaha zake nzito nzito.

Jumatano iliyopita waasi wanaopigania kujitenga eneo la mashariki la Ukraine waliwaonyesha maripota aina ya kile walichokiita silaha nzito nzito zilizohamishwa kutoka eneo la mapigano karibu na ngome yao ya Donetsk,lakini wasimamizi wa OSCE hawakuweza kudhibitisha habari hizo.

Ukraine inaonya ratiba itabadilishwa pindi waasi wakianza tena uchokozi

Makubaliano ya kuweka chini silaha yanaonyesha kuheshimiwa jeshi la Ukraine linasema hakuna mwanajeshi wake hata mmoja aliyeuwawa kwa siku ya pili mfululizo.

Hata Marekani inazungumzia kuhusu "maendeleo"-huo ukiwa ufafanuzi wa kwanza wa kutia moyo kutoka Washington.

Licha ya utulivu viongozi wa Ukraine mjini Kiev wameonya wako tayari kuibadilisha ratiba ya kuwahamisha wanajeshi wake pindi wasi wanaoelemea upande wa Urusi wakianza tena uchokozi.

Petro Poroschenko Ukraine PK Abzug Debalzewe
Rais Petro Poroschenko wa UkrainePicha: Reuters/Mykhailo Palinchak/Ukrainian Presidential Press Service

Jeshi la Ukraine linalalamika ,vikosi vya waasi vinajikusanya karibu na Marioupol-mji pekee mkubwa wa mashariki unaodhibitiwa na serikali ya mjini Kiev inakokutikana pia bandari muhimu katika bahari ya Azov.

Marioupol ambao ukitekwa,itakuwa hatua muhimu katika ujenzi wa daraja ya nchi kavu kati ya Urusi na Crimea,unaangaliwa kama lengo lijalo la waasi baada ya kuteka kitovu cha safari za reli-mji wa Debaltzeve wiki iliyopita unaoiunganisha miji inayodhibitiwa na waasi ya Donetzk na Luhansk.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP/

Mhariri: Mohammed Khelef