1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barcelona mabingwa wa Uhispania

Bruce Amani
30 Aprili 2018

Barcelona ilinyakua taji lao la 25 la ligi kuu ya kandanda Uhispania – La Liga baada ya kuifunga Deportivo La Coruna mabao manne kwa mawili wakati zikiwa zimesalia mechi nne msimu kukamilika

https://p.dw.com/p/2wvYN
La Liga Deportivo La Coruna v Barcelona Messi
Picha: Getty Images/D. Ramos

Lionel Messi alifunga hat trick na kufikisha mabao 32 ya ligi msimu huu na kuipa Barca taji lao la 7 la Laliga katika miaka 10. Ni kombe la pili la nyumbani kwa Barca ambao waliwazaba Sevilla 5-0 na kutwaa Kombe la Mfalme wiki iliyopita. Erneste Velverde ni kocha wa Barca "bila kujali mengine, tuna furaha sana kwa sababu tulikuwa na msimu mzuri sana. kwa sababu La Liga ndio kitu kinachokuambia wewe ni nani na ni wapi uliko kwa sababu sio kazi ya siku moja tu, bali kazi ya siku nyingi kutokana na mechi nyingi. Na unapaswa kucheza msimu wa baridi, mapukutiko na kisha mapuchiko ndio ufike mwisho na kusherehekea na watu wako. 

Lakini wakati Barcelonsa walipiga muhuri wa muongo mmoja wa udhibiti wa kandanda la nyumbani, nao Real Madrid wanaendelea kutamba katika jukwaa la Ulaya.

Real Madrid kupambana na Bayern

UEFA Champions League Halbfinale | FC Bayern München - Real Madrid
Real wanawakaribisha Bayern uwanjani BernabeuPicha: Imago/DeFodi/R. Krivec

Kocha wa Real Madrid Zinedine Zidane amewataka mashabiki wa klabu hiyo kushangilia vilivyo dhidi ya Bayern Munich uwanjani Santiago Bernabeu hapo kesho, wakati timu hiyo ya Uhispania ikilenga kutinga fainali ya Champions League kwa mwaka wa tatu mfululizo. "sidhani kuwa wanatuogopa. watakuja hapa bila hofu yoyote. nikirudia nilichosema, nadhani tunapaswa kucheza vizuri saan. Nnawaomba mashabiki kutushangilia, tutawahitaji sana kuliko ilivyokuwa awali. Wanafahamu tunachokitaka na wamekuwa nyuma yetu muda wote. Nnawaomba mashabiki. tunawahitaji sana kuliko wakati mwingine wowote.

Real walishinda mabao mawili kwa moja uwanjani Allianz Arena wiki iliyopita. Msimu uliopita, mambo yalikuwa hivyo hivyo, kabla ya MADRID kuwabwaga Bayern katika muda wa ziada. Nyota wa Bayern Frank Ribery amesema vita bado havijamalizika.

Katika mtanange wa Jumatano, Roma watahitaji muujiza kama waliofanya dhidi ya Barcelona walipotoka nyuma mabao manne kwa moja na kuwaondoa katika robo fainali. Mara hii watajitaji kuwakabili vilivyo Liverpool ambao waliwapa kichapo cha mabao matano kwa mawili uwanjani Anfield katika mkondo wa kwanza. Kocha wa Roma Eusebio Di Francesco amesema lazima wajiamini kuwa na matumaini ya kuyageuza matokeo hayo. Mashabiki karibu 5,000 watakuwa mjini Rome na polisi ya Italia imeimarisha ulinzi baada ya shabiki wa Liverpool kujeruhiwa vibaya kabla ya mechi ya mkondo wa kwanza. Hakuna vinyaji vya pombe vitakavyouzwa karibu na uwanja wa Stadio Olimpico na katikati mwa mji.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman