1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern kuwakosa wachezaji muhimu dhidi ya Heidenheim

Josephat Charo
5 Aprili 2024

Bayern Munich itawakosa wachezaji wake kadhaa walioumia katika mechi ya ugenini dhidi ya Heidenheim Jumamosi (06.04.2024). Bayern inahitaji kurudi katika fomu yake na kupata matokeo baada ya kupigwa 2-0 na Dortmund.

https://p.dw.com/p/4eTr3
Kocha Thomas Tuchel wa Bayern Munich.
Kocha Thomas Tuchel wa Bayern Munich.Picha: Martin Sylvest/AP Photo/picture alliance

Bayern Munich itawakosa wachezaji wake kadhaa walioumia katika mechi ya ugenini dhidi ya Heidenheim Jumamosi (06.04.2024) lakini timu hiyo inahitaji kurudi katika fomu yake na kupata matokeo baada ya kipigo cha wiki iliyopita cha 2-0 kutoka kwa Borussia Dortmund kama wako tayari kwa mechi ya ligi ya mabingwa wa Ulaya, Champions, kocha Thomas Tuchel amesema.

Bayern, washindi wa mataji 11 ya Bundesliga mfululizo, wako katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, alama 13 nyuma ya vinara Bayer Leverkusen zikiwa zimesalia mechi saba msimu kukamilika.

Bayern inakwaana na Arsenal wiki ijayo katika mechi ya duru ya kwanza ya robo fainali ya ligi ya mabingwa. Tuchel, ambaye wiki iliyopita aliipongeza Leverkusen ingawa bado kwa hakika hawajaushinda ubingwa wa Bundesliga kimahesabu, ataondoka Bayern mwisho wa msimu.

"Morali wetu hautakiwi kutegemea pale tuliposimama kwenye jedwali. Tumevunjwa moyo na matokeo ya wiki iliyopita tulipopoteza 2-0 dhidi ya Borussia Dortmund. Kwa hiyo tunatakiwa kuwa na ghadhabu ya kutosha ya kutoa jawabu Jumamosi," alisema Tuchel kwenye mkutano na waandishi habari siku ya Ijumaa.

"Hatuwezi kudondosha hata asilimia moja ya kushawishika kwetu na katika mtazamo wetu. Hatujaridhishwa kabisa na hali hiyo."

Bayern kuwakosa wachezaji wake waliojeruhiwa

Bayern Munich itakosa huduma za wachezaji wake kadhaa, wakiwemo mawinga Kingsley Coman na Leroy Sane pamoja na mlindalango Manuel Neuer na kiungo wa kati Aleksandar Pavlovic.

"Tatizo ni kwamba hakuna hata mmoja wao anayepumzishwa kabla pambano la ligi ya mabingwa Jumanne dhidi ya Arsenal. Wote hawamo katika kikosi dhidi ya Heidenheim kwa sababu hawawezi kucheza," Tuchel alisema.

"Hali ya majeruhi inatamausha. Nimekuwa na mawazo kuhusu jinsi ya kucheza dhidi ya Arsenal lakini wachezaji wanakosekana mara kwa mara kwa sababu ya majeraha. Kuanzia Manuel na kumalizia na mawinga wetu."

Soma pia: Tuchel abeba lawama kwa kipigo cha 3-0

Tuchel anatumai kufuzu kwa fainali ya kombe la mabingwa kutasaidia kusahau masaibu ya timu yake katika ligi ya nyumbani msimu huu na kumsaidia kuondoka Bayern akiwa na fahari.

"Hata kama taji la Bundesliga limeshatutoka, kombe la shirikisho lilishatutoka, bado tuna mashindano ya ligi moja ambayo tumo na ikiwa tunataka ndoto yetu itimie tunalazimika kutia bidii kila siku," alisema Tuchel.

(dpa)