1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yaipiku Anderlecht ligi ya Mabingwa Ulaya

Josephat Charo
13 Septemba 2017

Michuano ya ubingwa wa Ulaya imeanza huku timu kubwa kubwa zikipata ushindi uliotarajiwa. Kwa timu hizo ligi itaanza kikamilifu Februari mwaka ujao wakati wa duru ya mchujo.

https://p.dw.com/p/2jq33
Champions League - FC Bayern Munich vs RSC Anderlecht
Picha: Reuters/M.Rehle

Mkwaju wa Thiago Alcantara katika kipindi cha pili uliisaidia Bayern Munich ya Ujerumani kuicharaza Anderlecht mabao 3-0 katika mechi ya kwanza ya msimu huu wa michuano ya kombe la mabingwa Ulaya, Champions League iliyochezwa katika uwanja wa Allianz Arena mjini Munich. Baada ya Robert Lewandowski kufunga balo la kwa kwanza la mapema kupitia mkwaju wa penalti dakika ya 12 ya mchezo, Thiago alifunga la pili dakika ya 65 na Joshua Kimmich akagonga msumari wa mwisho katika jeneza la Anderlecht dakika ya 90.

Hata hivyo licha ya kudhibiti mpira kwa karibu dakika 80 wakiwa wengi, baada ya Sven Kum wa Anderlecht kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 11, mchezo wa Bayern Munich haukuwa katika kiwango cha kuridhisha. "Tulitakiwa kutumia fursa hiyo kufunga mabao mengi," amesema Joshua Kimmich. Mwishoni Anderlecht walipata fursa chache za kukomboa wakati hawakutakiwa hata kulikaribia lango letu. Kwa kuwa tuliwazidi kwa mchezaji mmoja, tulitakiwa kuitumia fursa hiyo vyema zaidi," akaongeza kusema.

Arjen Robben amekubali kwamba Bayern walitakiwa kutumia mbinu zaidi. Mchezo wetu haukuwa na kasi - tulihitajika kuonesha ari zaidi," akasema winga huyo raia wa Uholanzi. "Mashabiki walihitaji burudani zaidi, tunahitaji kutia bidii zaidi. Tulitakiwa kuwamaliza baada ya mchezaji wao kutolewa nje ya uwanja," akaongeza kusema Robben.

Kocha wa Bayern Munich, Carlo Ancelotti, alikifanyia mabadiliko kikosi chake baada ya kufungwa mabao 2-0 na Hoffenheim katika ligi kuu ya kandanda ya Ujerumani, Bundesliga, mwishoni mwa juma, kwa kumuondoa Thomas Müller na kumpa nafasi James Rodriguez kuanza kucheza kama kiungo mshambuliaji. Arjen Robben na Frank Ribbery, ambao wote hawakuanza mechi na Hoffenheim, walirudi katika kikosi cha kwanza jana. Thiago alicheza kama kiungo mkabaji akisaidiama na Mfaransa Corentin Tolisso.

Champions League - FC Bayern Munich vs RSC Anderlecht Kimmich
Joshua Kimmich wa Bayern Munich akimpita Dennis Appiah wa AnderlechtPicha: Reuters/M. Rehle

Dakika 15 kabla mechi kuisha, Müller aliingia kuchukua nafasi ya Ribbery, huku Jerome Botaeng naye akiingia kucheza mechi yake ya kwanza msimu huu baada ya kukaa nje akiuguza jeraha.

Bayern Munich itahitaji kujiimarisha kabla kukwaana na Paris Saint Germain katika mechi nyingine ya kundi B wiki mbili zijazo, ambayo jana iliigaragaza Celtic mabao 5 bila majibu mjini Glasgow.

Matokeo mengine ya mechi

Katika michuano mingine ya Champions League, katika kundi A, Machester United iliichapa Basel mabao 3 kwa nunge nyumbani Old Trafford.  Maroune Fellaini, Romelu Lukaku na Marcus Rushford walifumania wavu huku Man United wakirejea katika mashindano ya mabingwa Ulaya kwa ushindi wa wazi. Nahonda wa Manchester United na kiungo wa Ufaransa, Paul Pogba, alitoka nje ya uwanja baada ya dakika 18 alipoumia katika mguu wake wa kushoto. Kocha Jose Mourinho amesema hana hakika ikiwa Pogba ameumia sana ama la.

Katika mechi nyingine ya kundi A, CSKA Moscow iliishinda Benfica Lisabon mabao 2-1.

Chelsea ilipata ushindi mnono kwa kuinyeshea mvua ya magoli 6-0 Qarabag katika mechi ya kundi C, huku Atletico Madrid ikitoka sare tasa na AS Roma.

Champions League - FC Barcelona vs Juventus
Lionel Messi (katikati) akishangilia bao la tatu la Barcelona na Luis Suarez (kushoto) na Ousmanne Dembele (kulia)Picha: Reuters/S. Vera

Katika kundi D, Lionel Messi alianza vyema msimu huu kwa kuifungia timu yake ya Barcelona magoli mawili, dakika ya 45 na 69, na Ivan Rakitic akifunga moja dakika ya 56 na kuishinda Juventus mabao 3-0 katika uwanja wa Camp Nou. Barcelona ililipiza kisasi cha kufungwa na Juventus katika robo fainali msimu uliopita mwaka jana. Ousmane Dembele aliyetokea Borussia Dortmund ya Ujerumani, aliichezea Barcelona mechi yake ya kwanza katika Champions League. Juventus ilikosa huduma za beki Giorgio Chiellini, mshambuliaji Mario Mandzukic na kiungo Sami Khedira kupitia majeraha, huku Juan Cuadrado akifungiwa kucheza.

Sporting Lisabon iliishinda Olympiakos mabao 3-2 katika mechi nyingine ya kundi D.

Leipzig kucheza mara ya kwanza Champions League

Leo jioni RB Leipzig ya Ujerumani inacheza mechi yake ya kwanza katika Champions League kwa kuialika Monaco ya Ufaransa nyumbani Red Bull Arena mjini Leipzig. Borussia Dortmund itakwaana na Tottenham Hotspur huko England.

Real Madrid ya Uhispania itamenyana na APEOL Nicosia ya Cyprus, huku Porto ya Ureno ikicheza na Besiktas ya Uturuki. Feyenoord ya Uholanzi ina miadi na Manchester City huku Shaktar Donetsk ya Ukraine ikiikaribisha nyumbani Napoli ya Italia. Liverpool itavaana na Sevilla na Marobor itacheza na Spartak Moscow.

Mwandishi: John Juma

Mhariri: Yusuf Saumu