1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yaishushia Barcelona kipigo cha 8 - 2

Bruce Amani
15 Agosti 2020

Bayern iliipa Barcelona kipigo kikubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika enzi ya Lionel Messi na miongoni mwa vichapo vibaya zaidi katika historia ya timu hiyo, mabao 8 - 2 na kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa

https://p.dw.com/p/3h0Ag
Champions League Barcelona Bayern München Tor Müller
Picha: Getty Images/AFP/M. Fernandez

Mwanzo wa bora zaidi wa Bayern katika mtanange huo wa robo fainali kati ya mabingwa hao pekee katika nyuma waliobaki katika nane za mwisho, ulishuhudia Thomas Muller akitikisa wavu mara mbili na Ivan Perisic na Serge Gnabry wakiongeza yao katika nusu saa ya kwanza.

Thomas Muller alisema ushindi huu wa 8 - 2 dhidi ya Barcelona ni bora zaidi kuliko kichapo cha 7 - 1 ambacho Ujerumani iliipa Brazil katika Kombe la Dunia 2014. Kabla ya mechi kulikuwa na mjadala kuhusu umahiri wa washambuliaji wawili msimu huu. Lionel Messi wa Barca na Robert Lewandowski wa Bayern. Lakini katika mechi ya jana, Mueller mwenye umri wa miaka 30, ndiye aliyetawala na kupewa tuzo ya mchezaji bora wa mechi.

Barcelona walifungwa mabao manane kwa mara ya kwanza tangu 1946 baada ya Joshua Kimmich, Robert Lewandowski na Philippe Coutinho aliyefunga mawili, kuongeza idadi katika kipindi cha pili.

Barca walipiga shuti saba kuelekea langoni katika mechi nzima, na kupata bao la kujifunga lake David Alaba katika kipindi cha kwanza na kupitia Luis Suarez katika kipindi cha pili.

Champions League | Viertelfinale | FC Barcelona vs. Bayern München - Lewandowski Tor
Ushindi wa Bayern haukamiliki bila bao la Lewandowski Picha: Reuters/M. Fernandez

"ni matekeo mabaya mno. Ni aibu," alisema beki wa Barcelona Gerard Pique. "Hiki, leo, hakikubaliki."

ikitafuta taji lake la kwanza tangu 2013, Bayern sasa itashuka dimbani kupambana na ama Manchester City au Lyon, ambao watakutana leo katika robo fainali ya mwisho.

Paris Saint-Germain na Leipzig zipo katika nusu fainali nyingine ya mashindano hayo madogo yanayoandaliwa bila mashabiki mjini Lisbon, Ureno kutokana na janga la virusi vya corona.

"Kipigo kizito," alisema Kimmich. "Ni vigumu kuingia akilini kuichapa Barcelona 8 - 2. Tulikuwa makini sana kuanzia dakika ya mwanzo, tulitaka kushambulia na nia ya kufunga. Matokeo mazuri sana mwishowe, lakini hatujamaliza bado."

Ushindi huo mkubwa wa Bayern katika historia ya Champions League umeweka hai matumaini yake ya kubeba taji la sita, ambalo litawasogeza mbele ya Barcelona.

"Tulijua kuwa tukiwaweka katika shinikizo, tungepata nafasi za kufunga," Alisema kocha wa Bayern Hansi Flick. "Tuna wachezaji bora na nguvu kikosini, sasa tunahitaji kujiongeza nguvu na kuangazia mechi ijayo, ambapo tutaanza tena upya."

Bayern wameshinda mechi zote 9 za Champions League msimu huu na wanawinda taji la tatu la msimu baada ya kubeba Bundesliga na Kombe la Ujerumani.

Champions League | Viertelfinale | FC Barcelona vs. Bayern München - ENDSTAND
Ni wakati wa kutafakari kwa Lionel MessiPicha: Reuters/M. Fernandez

Matokeo hayo yamehitimisha msimu wa kusahaulika kabisa kwa Barcelona, ambao ulihusisha kubadilishwa kocha na ugomvi wa hadharani kati ya wachezaji na maafisa wa timu. Ni mara ya kwanza tangu 2008 ambapo klabu hiyo imemaliza msimu bila taji lolote muhimu. Haijabeba kombe la Ulaya tangu 2015.

Muda uliobaki kwa Quique Setien kama kocha unatarajiwa kuhesabiwa katika masaa. Tayari alikuwa chini ya shinikizo baada ya Barcelona kusalimisha uongozi wa kinyang'anyiro cha ligi ya Uhispania - na taji - kwa Real Madrid baada ya msimu kurejea kufuatia janga la corona.

"Kwa sasa ni mapema mno kusema kuhusu kama nitabaki katika klabu hii au la," alisema Setien. "Ukweli ni kwamba sio juu yangu. Ni bora kwetu sote kufahamu kilicho muhimu na kuzingatia mambo kadhaa ambayo yanachangia katika kipigo cha umuhimu huu na ambacho kinauma sana."

Kichapo cha Barcelona kina maana kuwa hakuna klabu ya Uhispania iliyotinga nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu 2007.

Mwandishi: Bruce Amani

dpa