1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIJING : Hu kuongoza nchi kwa miaka mitano mengine

22 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7Dg

Rais Hu Jintao wa China leo hii amechaguliwa kuwa mkuu wa chama tawala cha Kikumunisti kwa kipindi cha pili hiyo ikiwa ni idhini ya kuiongoza nchi kwa miaka mitano mengine.

Hu mwenye umri wa miaka 64 ametangazwa kuwa katibu mkuu wa chama na mkuu wa Kamati ya Kuu ya chama ambacho ni chombo cha kisiasa chenye nguvu kubwa kabisa nchini humo.

Akizungumza wakati timu mpya ya uongozi ikijitokeza mbele ya waandishi wa habari Hu amesema wanafahamu fika juu ya kazi zao ngumu na majukumu mazito na kwamba watajitahidi kuweza kustahiki imani kubwa waliowekewa na wanachama.

Hu pia amechaguliwa tena na Kamati Kuu kuwa mwenyekiti kwa kipindi cha pili wa Kamisheni Kuu ya Kijeshi ambao ni wadhifa mkubwa wa kijeshi nchini China.

Kufuatia kuchaguliwa tena kwa nyadhifa za mkuu wa chama na jeshi Hu anawekewa matumaini makubwa sana ya kuwa rais wa nchi kwa kipindi wakati bunge litakapokutana hapo mwezi wa Machi mwakani.