1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIJING: Marekani na Rushia zimekaribisha hatua ya Korea ya kaskazini kurejea kwenye mazungumzo juu ya nyuklia

1 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCwz

Korea ya kaskazini imekubali kurejea kwenye mazungumzo na nchi 6 zenye nguvu za kinyuklia. Korea ya kaskazini imesema itaomba iondolewe hatua ya kuzuwiliwa kutumia benki za kigeni na kwamba makubaliano hayo juu ya mazungumzo kuhusu mpango wake wa kinyuklia, yamefikiwa baada ya mazungumzo ya ana kwa ana na wawakilishi wa Marekani nchini Uchina. Hatua ilichukuliwa katika mkutano na maafisa wakuu wa Korea ya kaskazini, Uchina na Merekani mjini Beijing.

Rais wa Marekani, George W. Bush, baada ya kusikia habari hiyo, ametangaza furaha yake kwa kuwapongeza wale wote waliochangia kufikia hatua hiyo:

´´Ninayo furaha. Na ningependa kuishukuru Uchina ambayo iliandaa mkutano huo ambao umefanikiwa kufikia kwenye makubaliano ya kufanyika tena mazungumzo na nchi 6. Kila mara nilihisi kuwa ni muhimu Marekani kuwa kwenye meza ya mazungumzo na washirika wenzetu linapokuja suala tete kama hilo. Kwa hiyo ninatoa shukrani sio tu kwa Uchina, bali pia kwa Korea ya kusini, Japan na Rushia kukubali kurudi kwenye meza ya mazungumzo na Korea ya kaskazini´´.

Hata hivyo, rais Bush ameongeza kusema kwamba atatuma kundi la wachunguzi katika eneo lile kuhakikisha kwamba maazimio ya baraza la usalama la Umoja wa mataifa yanatekelezwa na kwamba wanaelekea kwenye mazungumzo yalioahidiwa.

Rushia nayo pia kupitia waziri wake wa mambo ya kigeni Sergei Lawrow, imekaribisha hatua hiyo ya Korea ya kaskazini:

´´Tunakaribisha utayarifu wa Korea ya kaskazini kurejea tena kwenye mazungumzo ya pande 6. Tunapenda kusisitiza mchango uliotolewa na wenzetu wa China. Tunaamini mazungumzo hayo yataanza tena haraka´´.

Matamshi ya Korea ya kaskazini kwamba itafanya mazungumzo na nchi 6 zenye nguvu za kinyuklia, yametolewa wiki tatu baada ya nchi hiyo kufanikiwa katika jaribio lake la kuripua bomu la kinyuklia.