1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIRUT: Hatimaye Wapalestina wakimbia mapigano

23 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CBzM

Maelfu ya wakimbizi wa Kipalelstina wameikimbia kambi yao baada ya siku tatu za mapigano kati ya majeshi ya nchi hiyo na wapiganaji wa kundi la Fatah al Islam kusitishwa.

Wakimbizi hao wameondoka katika kambi hiyo ya Nahr al Bared, iliyoko kaskazini mwa Lebanon ambako zaidi ya wapalestina elfu 30 wanaishi.

Magari ya misaada ya umoja wa mataifa yaliyokuwa yakijaribu kusambaza chakula, maji na madawa kwa watu waliyonaswa na mapigano hayo, yalilazimika kuondoka, baada ya kuzuka upya kwa mapigano.

Inakadiriwa kuwa kuna wapiganaji kiasi cha 200 wa kundi la Fatah al Islam waliyojichimbia katika kambi hiyo, ambao wamekuwa wakipambana na majeshi ya Lebanon toka siku ya Jumapili.

Takriban watu 81 wameuawa kutokana na mapigano hayo ambayo ni mabaya kabisa kuikumba Lebanon toka kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1990.