1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BELFAST: Uingereza yawataka viongozi wa Ireland wagawane madaraka

9 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCKv

Uingereza imewatolea mwito wanasiasa wa Ireland Kaskazini wakubali kugawana madaraka baada ya vyama viwili vya kiprotestanti na kikatoliki kuongeza idadi zao za viti bungeni.

Matokeo ya awali ya uchaguzi wa bunge jipya nchini Ireland Kaskazini yanaonyesha chama kikubwa cha kiprotestanti, Democrtic Unionist Party, DUP, kikiongoza kwa idadi ndogo ya kura mbele ya chama cha kikatoliki cha Sinn Fein.

Huku vyama hivyo viwili vikishinda karibu nusu ya idadi ya viti bungeni, vinaonekana kuwa vyama vitakavyounda serikali mpya itakayogawana madaraka nchini humo.

Kwa mujibu wa mkataba wa amani uliotayarishwa na Uingereza na Ireland, vyama vimepewa hadi tarehe 26 mwezi huu kuunda serikali mpya.

Ireland Kaskazini imekuwa ikitawaliwa kutoka mjini London tangu mwezi Oktoba mwaka wa 2002, wakati madai ya ukachero uliofanywa na bawa la kijeshi la chama cha Sinn Fein, IRA, uliposababisha bunge kusitisha shughuli zake. Matokeo ya mwisho ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutangazwa baadaye leo.