1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benfica yapinga madai ya rushwa, yaapa kusafisha jina lake

Iddi Ssessanga
6 Septemba 2018

Klabu ya soka ya Benfica, ambayo ilishtakiwa kwa rushwa na waendesha mashitaka wa Ureno mapema wiki hii, wameyataja mashitaka hayo kama yasiyo na msingi na kuapa kusafisha jina lao.

https://p.dw.com/p/34RdB
Symbolbild Fußball Benfica Fans
Picha: Getty Images/AFP/P. Moreira

Klabu hiyo inashutumiwa na waendesha mashitaka kwa kudukuwa nyaraka za mahakama na iwapo watakutwa na hatia, sheria ya adhabu ya Ureno inaainisha kuwa wanaweza kufungiwa kushiriki mashindano kwa kipindi cha kati ya miezi sita hadi miaka mitatu.

Wanaweza pia kupoteza ruzuku za umma na kukabiliwa na vikwazo vingine.

Rais wa klabu hiyo, Luis Filipe Vieira, alisoma taarifa kwa waandishi habari siku ya Jumatano na kusema Benfica itatetea sifa yake, katika hali ya kushikilia msimamo na kwamba mashitaka dhidi yao hayakuwa na ukweli wowote, siyo hata ushahidi wa kimazingira, ambao unegeweza kuwatia hatiani Benfica.

"Tuhuma hizo hazibadili hata kidogo uhakika wetu kuhusu uhalali wa vitendo vya Benfica SAD na tabia yake, iwe katika kesi hii au nyingine yoyote," alisema na kuongeza kuwa "taasisi za kisheria zitalisafisha jina zuri la Benfica".

Vieira alitajwa kuwa mshukiwa rasmi katika uchunguzi wa rushwa mapema mwaka huu. Uchunguzi huo hata hivyo, hauhusiani na klabu.

Symbolbild Fußball Benfica Fans
Benfica ndiyo klabu inayoongoza kwa wanachama nchini Ureno. Picha: Imago

Mashitaka yanayowakabili

Siku ya Jumanne waendesha mashitaka waliishtaki Benfica SAD -- klabu ya michezo inayojumuisha timu ya soka yenye mafanikio zaidi nchini humo -- mshauri wa kisheria wa klabu na wafanyakazi wawili wa mahakama, kwa orodha ndefu ya mashitaka, yakiwemo rushwa na kuvunja usiri wa mhimili wa mahakama.

Wanadaiwa kula njama na kudukuwa mfumo wa rekodi wa kielektroniki wa mahakama na kupokea taarifa kuhusu chunguzi mbalimbali zinazoihusisha Benfica, na mahasimu wake kama Sporting na Porto, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Jaji hajaamuwa bado iwapo akubali kesi ya mwendesha mashitaka dhidi ya Benfica -- klabu maarufu zaidi nchini Ureno kwa uanachama -- au dhidi ya watu binafsi.

Shirikisho la Kandanda la Ureno limeamuru kufanyika uchunguzi wake, kwa msingi wa taarifa zilizotolewa na ofisi ya mwendesha mashitaka, ili kubaini iwapo kuna makosa yoyote ya kimichezo yaliotendeka.

Hilo linaweza kupelekea kuchukuliwa hatua za kinidhamu kama vile kukatwa pointi katika mashindano ya ubingwa ya Ureno au hata kushushwa daraja.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre

Mhariri: Yusra Buwayhidi