1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benjamin Netanyahu apewa jukumu la kuunda serikali

Amina Mjahid
8 Mei 2020

Rais wa Israel Reuven Rivlin amemkabidhi jukumu la kuunda serikali ya muungano Waziri Mkuu wa nchi hiyo Benjamin Netanyahu hatua inayonuiwa kumaliza mgogoro wa kisiasa iliodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja.

https://p.dw.com/p/3bvvR
Benjamin Netanjahu, Reuven Rivlin und Benny Gantz
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, rais Reuven Rivlin na Benny Gantz kiongozi wa chama cha buluu na nyeupe IsraelPicha: Reuters/R. Zvulun

Taarifa kutoka  serikalini inasema  barua  ya rais iliyompa Waziri Mkuu Netanyahu jukumu hilo la kuanza kuunda serikali ya muungano imetumwa kwake mapema jana, na ofisi ya spika wa bunge la Knesset pia imejulishwa kuhusu hatua hiyo.

Rais wa Israel Reuven Rivlin, alimmpa jukumu la kuunda serikali waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ndani ya wiki mbili baada ya wabunge 72 kati ya 120 kumpitisha kiongozi huyo wa chama cha Likud kama Waziri Mkuu, na kutoa  nafasi ya kuwa na serikali ya muungano na mpinzani wake ambaye amegeuka kuwa mshirika Benny Gantz.

Hatua hiyo inanuiwa kumaliza mgogoro wa kisiasa uliodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja nchini Israel.

Bunge la Knesset lilimuidhinisha Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu baada ya mahakama kuu kusema haitoingilia mpango wowote mpya au kumzuwia Netanyahu kuiongoza serikali licha ya waziri Mkuu huyo kukabiliwa na mashitaka ya ufisadi. Hatua hiyo imeizuia Israel kufanya uchaguzi wake wa nne mkuu ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Netanyahu na Gantz kuongoza katika uwaziri Mkuu wa kupokezana

Kwa sasa Benjamin Netanyahu na Benny Gantz wanatarajiwa kuuapisha uongozi mpya Tarehe 13 mwezi May huku Netanyahu akiongoza kwa miazi 18 kabla ya kutoa nafasi kwa Gantz naye kuongoza katika uaziri mkuu wa kupokezana ambayo ni nafasi mpya ilioundwa na serikali.

Awali Gantz alikataa kushirikiana na Netanyahu katika kuunda serikali ya muungano akisema hawezi

kushirikiana na mtu anaekabiliwa na mashitaka ya ufisadi, lakini awali alibadilisha msimamo wake na kusema serikali ya muungano inahitajika ili kuikwamua nchi kutokana na changamoto za kiuchumi zinazosababishwa na janga la vitrusi vya corona.

Netanyahu aliye na miaka 70 amekanusha kufanya makosa yoyote kuelekea kesi yake inayotarajiwa kuanza kusikilizwa taraehe 24 mwezi May.

Hata hivyo wakosoaji wanasema mpango walioufikia si halali  na kupanga kwenda mahakamani kuupinga.

Wanasema kuwa sheria inapaswa kumzuia afisa yoyote wa serikali aliyeshitakiwa kwa makosa ya uhalifu kuendelea kuhudumu kama Waziri Mkuu. Pia wamepinga vikali nafasi ya uwaziri mkuu wa kupokezana ambayo inaweza kumruhusu Netanyahu kubakia uongozini wakati wote kesi yake itakapokuwa ikiendelea. 

Chanzo: afp,reuters