1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benki kuu ya dunia kuwa na kiongozi mpya, na IMF pia kupata kiongozi mwingine.

Sekione Kitojo29 Juni 2007

Kujiuzulu kwa ghafla kwa kiongozi wa shirika la fedha la kimataifa IMF kumezusha mara moja miito ya kubalidika kwa mfumo wa kumpata kiongozi wa shirika hilo kupindukia mipaka ya Ulaya, eneo ambalo limekuwa likitoa viongozi wote waliowahi kushika wadhifa huo. Wadhifa huo umekuwa kwa wakati wote ukienda kwa watu wa mataifa ya Ulaya tangu kuanza kwa shirika hilo mwaka 1945. Kwa kawaida benki kuu ya dunia inaongozwa na Mmarekani, ikiitupa kando Japan na nchi zinazoendelea.

https://p.dw.com/p/CHBr

Kujiuzulu kwa Rodrigo Rato kumekuja kiasi ya wiki kadha baada ya mjadala kama huo kuvuma kutokana na uteuzi wa rais mpya wa benki kuu ya dunia, kufuatia kujiuzulu kwa Paul Wolfowitz kutokana na kashfa ya kumpandisha cheo mpenzi wake.

Mashirika yote mawili , ambayo wachangiaji wake wakubwa ni Marekani na umoja wa Ulaya , yanakabiliwa na mbinyo mkali kutoa usemi zaidi kwa mataifa yanayochipukia juu ya jinsi yanavyoendeshwa.

Shirika la IMF limeanza hatua za mageuzi ambayo linamatumaini yatalielekeza katika njia hiyo, kwa hiyo kufungua utaratibu wa kumpata mtu atakayeshika nafasi ya Rato kwa watu ambao sio kutoka Ulaya litakuwa jambo muhimu, afisa mmoja wa bodi ya IMF anayetoka nchi zinazoendelea amesema.

Kwa upande mwingine kuondolewa kwa Paul Wolfowitz kumetoa changamoto kwa uongozi wa Marekani katika azma yake ya kupambana na umasiki kwa kupitia taasisi hiyo.

Lakini bodi ya mataifa wanachama wiki iliyopita bado ilimteua Mmarekani mwingine katika wadhifa huo, na kumuidhinisha waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani Robert Zoellick ambaye anaanza kazi Julai mosi.

Rato , waziri wa zamani wa fedha nchini Hispania , amekuwa mkurugenzi mtendaji mkuu wa IMF tangu 2004.

Amesema siku ya Alhamis kuwa ataondoka katika wadhifa huo baada ya mkutano wa taasisi hiyo mwezi Oktoba.

Muda mfupi tu baada ya kutoa uamuzi wake , wadadisi na makundi ya maendeleo katika IMF yamesema kuwa sasa umefika muda wa kufanya mageuzi katika utamaduni wa muda mrefu wa bara la Ulaya kuliongoza shirika hilo.

Badala ya kuendeleza utamaduni wa kumtafuta mrithi wa kiongozi wa taasisi hiyo katika maeneo ya Ulaya tu , magavana wa IMF wapanue uwigo wa msako wa kiongozi huyo ili kupata uzoefu wa viongozi katika mataifa yanayoendelea, amesema Bernice Romeo, mkurugenzi wa utetezi na kampeni wa shirika la kutoa misaada la Oxfam.

Ameongeza kuwa benki ya dunia imeshindwa kuchukua nafasi hii kujionyesha kuwa ni ya kisasa, taasisi ya kimataifa kwa kuwa na hatua za uficho kwa ajili ya rais wake. IMF haipaswi kufanya makosa kama hayo, amesema.

Kenneth Rogoff mkuu wa zamani wa kitengo cha uchumi cha IMF na hivi sasa akiwa mhadhiri mwalikwa katika chuo cha taasisi ya Brookings, amesema anawasiwasi kuwa Marekani haitatoa mbinyo kwa ajili ya kupata mageuzi katika uteuzi wa kiongozi wa IMF kwasababu washirika wake wa Ulaya wameunga mkono uteuzi wake wa rais wa benki kuu ya dunia Zoellick.

Iwapo kutakuwa na kitu chochote kizuri kutokana na mkasa wa kashfa ya Wolfowitz , ni utambuzi kuwa nyakati ambapo Wamarekani wamekuwa wakimteua tu kiongozi wa benki ya dunia na Ulaya kuteua kiongozi wa IMF umemalizika, amesema Rogoff.

Wakati tangazo la kujiuzulu kwa Rato lilikuja ghafla , kulikuwa tayari na uvumi mkubwa juu ya warithi wa kiongozi huyo. Miongoni mwa majina yaliyotajwa ni gavana wa benki ya Uingereza Mervyn King na Mfaransa Jean Lamierre ambaye anaongoza benki kuu ya Ulaya ya ujenzi mpya na maendeleo.