1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benki ya Dunia yatoa ripoti kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa

Kabogo Grace Patricia30 Septemba 2009

Ripoti hiyo inasema kuwa nchi zinazoendelea zitahitaji kuwekeza katika miradi mikubwa ya miundombinu.

https://p.dw.com/p/JuyI
Rais wa Benki ya Dunia, Robert Zoellick.Picha: picture-alliance/ dpa

Uchunguzi wa Benki ya Dunia unaonyesha kuwa nchi zinazoendelea duniani zitahitaji kutumia zaidi ya dola bilioni 100 kwa mwaka katika miaka 40 ijayo ili kujiweka tayari kwa mabadiliko makubwa zaidi ya hali ya hewa.

Ripoti hiyo ya Benki ya Dunia inasema kuwa nchi masikini zitahitaji kuwekeza katika miradi mikubwa ya miundombinu ili kuweza kukabiliana na majanga kama vile mafuriko, ukame, joto kali na mvua za mara kwa mara kama hali joto ya dunia itaongezeka kwa selisiasi nyuzijoto mbili ifikapo mwaka 2050. Katherine Sierra, Makamu rais wa kitengo cha maendeleo cha Benki ya Dunia, anasema zikiwa zinakabiliwa na gharama za ujenzi wa miundombinu, pamoja na ukame, nchi zinazoendelea duniani zinahitaji kujiandaa kwa mabadiliko ya hali ya hewa.

Makadirio ya awali

Awali makadirio ya gharama yaliyotolewa na makundi mengine yalikuwa kuanzia dola bilioni 9 hadi 104, lakini ripoti ya Benki ya Dunia imesema gharama hizo zianzie dola bilioni 75 hadi 100 kulingana na maeneo mawili, ambapo eneo la kwanza ni kwa ajili ya nchi zenye mazingira makavu ambazo zitahitaji uwekezaji mdogo kuliko maeneo yenye unyevu nyevu, ambayo yatahitaji hatua zaidi kama vile kujenga kuta za bahari au mifereji mirefu.

Warren Evans, Mkurugenzi wa idara ya maendeleo ya Benki ya Dunia, anasema nchi za Asia Mashariki na zile zilizoko kwenye Bahari ya Pacific, ambalo lina nchi zenye uchumi unaokuwa kwa haraka sana zitaathirika vibaya kifedha, ikiwa zitagharimu kiasi cha robo ya gharama zote, hasa kutokana na kuongezeka kwa watu mijini, hasa kwenye maeneo ya pwani. Kwa mujibu wa uchunguzi huo wa Benki ya Dunia, gharama itakayotokana na kuishi katika dunia yenye hali ya ujoto ni sawa na kiwango cha msaada ambacho nchi zinazoendelea zinapata kwa sasa.

Mtazamo wa mashirika ya misaada

Mashirika ya misaada yanasema kuwa ni muhimu kwamba msaada wa fedha usipunguzwe ili kuchangia katika jitihada za mabadiliko ya hali ya hewa. Antonio Hill, mshauri wa juu kuhusu sera za hali ya hewa wa Shirika la misaada la Oxfam, anasema msaada wowote unaokuja ni lazima uwe nyongeza ya fedha. Shirika la kuwalinda wanyama la WWF, limesema kuwa makadirio ya Benki ya Dunia yalizingatia kuwa dunia itafanya kazi pamoja kuhakikisha hali joto haipandi kwa nyuzi joto mbili. Katika ripoti yake WWF imesema ahadi kutoka nchi zilizoendelea katika majadiliano ya sasa hazitoki kokote karibu na kiwango hicho cha kutimiza malengo hayo. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, hiyo inaonyesha msisitizo juu ya uhitaji wa ahadi zaidi zilizopo mezani kutoka kwenye nchi zilizoendelea, katika kupunguza kiwango cha matumizi ya gesi inayoharibu mazingira na kuchangia mabadiliko ya hali ya hewa kwenye nchi zinazoendelea.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE)

Mhariri:Abdul-Rahman