1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN:Ujerumani kuendelea kuwepo nchini Afghanistan

23 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBg1

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametetea kuwepo kwa majeshi ya Ujerumani nchini Afghanistan siku moja tu baada ya mwili wa mateka wa kijerumani aliyeuawa kupatikana.

Kansela Merkel alisisitiza uamuzi wa serikali yake kuhakikisha kuwa malengo ya majeshi ya Umoja wa Kujihami wa NATO nchini Afghanistan yanafikiwa.

Alisisitiza hayo mnamo wakati ambapo kumezidi kutolewa tahadhari na maafisa wa usalama ya kwamba huenda magaidi wakaindama Ujerumani kutokana na kuwepo kwa askari wake Afghanistan.

Wizara ya mambo ya ndani ya Ujerumani imesema kuwa mwili wa mateka wa kijerumani ulikutwa na majeraha ya risasi, lakini bado sababu ya kifo chake haijafahamika.Majaaliwa ya mateka mwengine wa kijerumani hayajulikani.

Wakati huo huo Serikali ya Afghanistan imesema kuwa imepeleka vikosi zaidi katika eneo ambalo wanashikiliwa mateka 23 raia wa Korea Kusini na wanamgambo wa Kitaliban.

Wanamgambo hao wametoa muda wa saa 24 kutimizwa kwa masharti yao wanayoitaka Korea Kusini kuondoa vikosi vyake nchini Afghanistan.

Ujumbe wa Serikali ya Korea Kusini umekwenda nchini Afghanistan kwa mazungumzo na serikali ya huko juu ya uwezekano wa kuachiwa kwa mateka hao.