1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden aendelea na ziar yake Mashriki ya Kati

7 Machi 2016

Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden anatarajiwa kuwasili nchini Israel siku ya Jumanne (08.03.2016) kwa mazungumzo na waziri mkuu wa nchi hiyo Benjamin Netanyahu. Biden yuko katika ziara ya siku tano Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/1I8nZ
VAE Abu Dhabi Joe Biden besucht Große Moschee
Joe Biden alipoutembelea msikiti mkubwa wa Sheikh Zayed mjini Abu Dhabi, Famle za Kiarabu 07.03. 2016Picha: Reuters/Stringer

Biden anatarajiwa kukutana na Netanyahu pamoja na rais wa Israel, Reuven Rivlin mjini Jerusalem na baadaye kukutana na rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina, Mahmoud Abbas mjini Ramallah. Atakutana pia na rais wa zamani wa Israel, Shimon Peres.

Biden na Netanyahu wanatarajiwa kujadili mapambano dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu. Israel na Marekani zimekuwa zikijaribu kuondoa tofauti na misuguano ya awali kuhusiana na mkataba kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, ambao Netanyahu aliupinga vikali, na badala yake kuandaa mkataba mpya wa ulinzi kwa miaka kumi ijayo.

Mkataba wa sasa unaipa Israel dola bilioni 3.1 kwa mwaka, pamoja na fedha nyingine za kugharamia miradi mingine kama vile ulinzi dhidi ya makombora.

Waziri Mkuu Netanyahu amemtaja Biden kuwa rafiki na kusema ziara yake ni ushahidi wa mahusiano imara kati ya Israel na Marekani. "Rafiki yetu makamu wa rais wa Marekani Joe Biden atawasili kwa ziara. Ziara hii inaashiria uhusiano imara kati ya Israel na mshirika wake Marekani. Baadhi tayari walitabiri mahusiano haya yangesambaratika, lakini si kweli. Mahusiano yako imara katika kila upande na pia katika kuzikabili changamoto za kanda."

Netanyahu alikuwa na uhusiano mgumu na rais wa Marekani, Barack Obama, hususan kuhusiana na kukataa kwake mkataba kati ya Iran na mataifa ya magharibi juu ya mpango wake wa nyuklia.

Biden hatapendekeza kuyafufua mazungumzo ya amani

Ziara ya Biden inakuja wakati kukiwa na wimbi la machafuko nchini Israel na katika maeneo ya Wapalestina lililodumu miezi mitano, ambapo Wapalestina 181 pamoja na Waisraeli 28 wameuliwa. Kwa mujibu wa maafisa wa Israel, Wapalestina wengi waliokufa katika machafuko hayo waliuawa wakati walipokuwa wakifanya mashambulizi ya visu, bunduki au kuwagonga watu kwa magari. Wengine walipigwa risasi na maafisa wa usalama wa Israel wakati wa makabiliano au maandamano."

USA Israel Benjamin Netanjahu & Barack Obama Weißes Haus Washington
Benjamin Netanyahu, kushoto, na rais wa Marekani, Barack ObamaPicha: Reuters/K. Lamarque

Ikulu ya Marekani haikuyatilia maanani mapendekezo kwamba Biden ataanzisha juhudi mpya za kutafuta amani kati ya Waisraeli na Wapalestina wakati wa ziara yake. Afisa wa ngazi ya juu wa utawala wa Obama aliwaambia waandishi wa habari kuwa makamu wa rais Biden hatawasilisha mapendekezo yoyote mapya makubwa kuhusu amani ya Mashariki ya Kati, lakini atajikita zaidi katika kuimarisha ushirikiano katika masuala kadhaa yakiwemo mapambano dhidi ya Dola la Kiislamu na njia za kuutafutia ufumbuzi mzozo wa Syria. Afisa huyo pia amesema wanafuatilia kwa wasiwasi mkubwa machafuko yanayoendelea kati ya Waisraeli na Wapalestina katika miezi ya hivi karibuni.

Ziara ya Biden nchini Israel ni ya pili tangu ile ya kwanza aliyoifanya mwaka 2010, ambayo iligubikwa na tangazo la Israel la mradi mpya wa ujenzi wa makazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan, lililoikasirisha ikulu ya Marekani, iliyosema unavuruga uwezekano wa kupatikana suluhisho la amani kati ya Waisraeli na Wapalestina.

Biden ataizuru Israel akitokea Abu Dhabi, Falme za Kiarabu, ambako alifutilia mbali suluhisho la kijeshi kwa mzozo wa Syria na kuutembelea msikiti mkubwa wa Sheikh Zayed, akiwa ameandamana na mkurugenzi mtendaji wa msikiti huo, Yousif Abdallah Alobaidli na waziri wa mambo ya ndani, Reem al-Hashimi.

Anatarajiwa pia kuitembelea Jordan ambako atakutana na Mfalme Abdullah II mjini Amman.

Mwandishi:Josephat Charo/ape/

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman