1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden aomboleza mauaji ya kutumia bunduki huko Texas

30 Mei 2022

Rais wa Marekani Joe Biden amezitembelea familia za wahanga wa shambulizi la bunduki la wiki iliyopita ambalo lilisababisha vifo vya watoto 19 na walimu 2 wa shule ya msingi ya Robb iliyoko kusini mwa jimbo la Texas.

https://p.dw.com/p/4C1MA
USA Präsident Biden in Uvalde
Rais Biden na mkewe Jill wakimfariji mkuu wa shule ya Robb. Picha: Marco Bello/REUTERS

Akiwa ameambatana na mkewe Jill, rais Biden kwanza aliitembelea shule ya Robb eneo ambalo Jumanne iliyopita kijana mwenye bunduki ya rashasha alitekeleza shambulizi la kutisha kwa kuwamiminia risasi watoto wa shule ya msingi na kuwaua 19 pamoja na walimu wao wawili. Wanafunzi wote waliouwawa walikuwa na umri wa chini ya miaka 10. 

Biden na mkewe walibubujikwa machozi walipofika eneo la kumbukumbu ya wahanga ambako kuna picha za wanafunzi na walimu waliouwawa pamoja rundo la mashada ya maua na kadi zenye salamu nyingi za rambirambi kutoka kwa watu walioguswa na mkasa huo.

Wakiwa wamevalia mavazi meusi yanayoashiria maombolezo, rais Biden na mkewe walitembea taratibu kutazama picha ya kila aliyepoteza maisha wakati wa shambulizi la wiki iliyopita ambalo linatajwa kuwa baya zaidi kuwahi kutokea nchini Marekani kwa karibu muongo mmoja.

Kundi la watu waliopiga kambi nje ya kanisa ambako Biden baadae alikwenda kuhudhuria ibada ya kumbukumbu ya wahanga wa mkasa huo lilipaza sauti likisema "fanya chochote" na Biden aliitikia "Tutafanya, tutafanya".

Yumkini matamshi hayo ya watu yalikuwa yakimtaka Biden kutafuta njia ya kukomesha mauaji holela yanayotokana na mashambulizi ya kutumia bunduki ambayo yanaiandama Marekani kila uchao.

Baada ya ibada rais Biden alikutana na familia za wahanga kwa saa kadhaa kabla ya baadae kuwa na mazungumzo na maafisa wa usalama walioshiriki kutoa msaada wakati na baada ya shambulizi.

Wamarekani waghadhabishwa na ripoti ya kuwepo uzembe kumkabili mshambuliaji 

USA Präsident Biden in Uvalde
Rais Biden na mkewe wakitoa heshima mbele ya eneo la maombolezo ya mauaji ya shule ya msingi Robb.Picha: Mandel Ngan/AFP/Getty Images

Ziara ya Biden kwenye eneo hilo imefanyika wakati hasira ya umma inaongezeka baada ya kuzagaa  ripoti ya kuwepo uzembe kwa maafisa wa usalama waliofika mwanzo kumkabili mshambuliaji.

Inaarifiwa maafisa hao walibakia kwenye ukumbi wa shule hiyo kwa kiasi saa moja wakati mshambuliaji akiendelea kufanya mauaji. Wizara ya sheria ya Marekani imetangaza kuwa inafungua uchunguzi kubaini ukweli wa kile kilichotokea.

Wakati wa ziara hiyo Biden hakupangiwa kutoa hotuba mjini Texas lakini siku ya Jumamosi alizungumza kwa kirefu ambapo alitoa wito kwa mara nyingine kwa bunge la nchi hiyo kumaliza mkwamo wa miaka mingi wa kuongeza makali ya kanuni za kumiliki silaha.

Hususan bunduki za rashasha mfani wa AR-15 iliyotumiwa na mshambuliaji wa huko Uvalde, Texas.

Je, kisa cha Texas kitabadili nyoyo za wanasiasa wanaopigia upatu umiliki silaha? 

USA I Houston, Texas:
Mipaka ya haki ya kumiliki silaha nchini Marekani ni suala tetePicha: Gasia Ohanes/DW

Ziara ya jimboni Texas ilikuwa ni ya tatu kwa rais  Biden kuyatembelea maeneo yaliyoshuhudia shambulizi la bunduki.

Mapema mwezi huu alikwenda huko Buffalo, New York kutoa pole baada ya mshambuliaji mmoja kuwauwa Wamarekani 10 wenye asili ya kiafrika katika duka moja la bidhaa za nyumbani.

Miito ya kutaka umiliki holela wa bunduki uzuiwe nchini Marekani mara zote imeambulia patupu. Wanasiasa vigogo wa chama cha Republican mara zote ndiyo wamekuwa wakipinga kuimarishwa kwa kanuni za watu kumiliki silaha wakisema ni kinyume na katiba.

Wademocrats nao wanaohofia kuingia kwenye mapambano kamili kuepuka kuwaghadhabisha wapiga kura wanaopendelea haki ya watu kumiliki bunduki.