1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden atafakari ombi la kuifuta kesi dhidi ya Assange

Bruce Amani
11 Aprili 2024

Rais Joe Biden amesema anatafakari ombi la Australia la kuifuta kesi ya muongo mmoja ya Marekani kutaka kumshtaki muasisi wa tovuti ya kuvujisha nyaraka za siri Wikileaks Julian Assange.

https://p.dw.com/p/4eepP
Julian Assanges
Muasisi wa tovuti ya kuvujisha nyaraka za siri Wikileaks Julian Assange.Picha: George Chan/SOPA Images/picture alliance

Assange anatuhumiwa kuchapisha nyaraka nyingi za siri za Marekani. Kwa miaka mingi, Australia imekuwa ikiitolea wito Marekani kuitupilia mbali kesi yake dhidi ya Assange, raia wa Australia ambaye anapinga juhudi za Marekani kutaka ahamishiwe nchini humo kutoka gereza la Uingereza.

Na sasa Biden amesema Marekani inalitafakari suala hilo. Assange alishitakiwa kwa makosa 17 ya ujasusi na moja la matumizi mabaya ya kompyuta kuhusiana na uchapishaji wake wa nyaraka za siri za Marekani miaka 15 iliyopita.

Mahakama ya Uingereza yasema Assange haendi Marekani

Waendesha mashitaka wa Marekani wanadai kuwa Assange mwenye umri wa miaka 52, alimhimiza na kumsaidia mtalaamu wa ujasusi wa jeshi la Marekani Chelsea Manning kuiba nyaraka za kidiplomasia na faili za kijeshi ambazo WIkileaks ilichapisha, na kuyaweka maisha ya watu hatarini.

Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese amesema kauli ya Biden kuhusu Assange inatia moyo.