1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden atetea kuondoa vikosi nchini Afghanistan

1 Septemba 2021

Rais wa Marekani Joe Biden amesema operesheni ya kuwaondoa watu nchini Afghanistan ilikuwa ya "mafanikio makubwa" na kupuuza ukosoaji kuwa haikuandaliwa vizuri.

https://p.dw.com/p/3zlVP
USA I Präsident Joe Biden zur Lage in Afghanistan
Rais Joe Biden wa Marekani Picha: Evan Vucci/AP/picture alliance

Katika hotuba yake kwa taifa aliyoitoa usiku wa kuamkia leo, rais Biden kwanza ametetea vikali uamuzi wake wa kuondoa wanajeshi wote wa Marekani nchini Afghanistan na kumaliza ushiriki wa nchi hiyo kwenye vita vya karibu miongo miwili.

Kiongozi huyo ambaye amekuwa kwenye shinikizo tangu alipotangaza uamuzi huo, amesema isingekuwa rahisi kurefusha muda kwa vikosi vya Marekani nchini Afghanistan na muda ulikuwa umewadia kwa wanajeshi wa taifa hilo kurejea nyumbani na kuufunga ukurasa wa vita vya muda mrefu zaidi kwa Marekani.

Biden amejinasibu kuwa ametimiza ahadi ya kumaliza vita nchini Afghanistan na kamwe asingekubali kuwa kiongozi wa kupeleka kizazi kingine cha vijana wa Marekani kuendeleza mapigano katika ardhi ya taifa hilo la Asia ya kati.

Biden: Lengo la vita nchini Afghanistan limekwisha 

Biden pia ametumia hotuba yake kukumbusha kwamba kwa sehemu kilichowapeleka vitani nchini Afghanistan kimekwisha.

Afganistan, Flughafen in Kabul
Picha: Wakil Kohsar/AFP/Getty Images

Marekani ilipeleka wanajeshi wake kupambana na ugaidi, kusambaratisha mtandao wa makundi ya itikadi kali na kulipa kisasi dhidi wote walioishambulia nchi hiyo mnamo Septemba 11 mwaka 2001.

Na kwa tathmini  ya Biden hayo yote yamefanikiwa na kuwaonya wale watakaojaribu tena.

"Kwa wale wanaolenga kuidhuru Marekani, kwa wale wanaojihusisha na ugaidi dhidi yetu au washirika wetu tambueni hili. Marekani haitapumzika. Haitasamehe, haitasahau. Tutawasaka hadi ukingo wa mwisho wa dunia hii. na mtalipa gharama kubwa" amesema Biden.

Ama kuhusu jinsi operesheni ya kuondoka nchini Afghanistan ilivyoendeshwa, rais Biden amejikingia kifua akisema ilifanyika kwa mafanikio makubwa sana licha ya lawama kwamba zoezi hilo liliendeshwa shaghala baghala.

Amesema Marekani imefanikiwa kuwaondoa  watu wasiopungua 120,000 ikijumuisha raia na washirika wake wa kiafghani katika kile rais huyo amekitaja kuwa operesheni kubwa zaidi ya kuhamisha watu kuwahi kutokea.

Nchini Afghanistan, Taliban yajiandaa kuunda serikali 

Afghanistan Bildergalerie Nach Abzug der Truppen
Wapiganaji wa Taliban Picha: HOSHANG HASHIMI/AFP via Getty Images

Katika hatua nyingine kundi la Taliban limetangaza kuwa linajiandaa kuunda serikali mpya nchini Afghanistan.

Msemaji wa kundi hilo Zabihullah Mujahid amesema bado hakuna taarifa mahsusi lakini muda wowote kuanzia sasa serikali mpya huenda itatangazwa.

Hayo yanajiri wakati kumezuka mapigano mapya kati ya Taliban na wapiganaji wanaopinga utawala wa kundi hilo katika bonde la Panjshir usiku wa kuamkia leo.

Panjshir ndiyo wilaya pekee ambayo haikukamatwa na kundi la Taliban liliposonga mbele mapema mwezi uliopita na kisha kuiangusha serikali mjini Kabul.