1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani, Uingereza na Australia kujikinga na China

Sudi Mnette
13 Machi 2023

Viongozi wa Marekani, Uingereza na Australia,wapo katika hatua ya kuzindua mipango ya kuipa Australia nyambizi zinazoendeshwa kwa nguvu ya nishati ya nyuklia, katika jitihada kubwa dhidi ya kukabiliana na kitisho China.

https://p.dw.com/p/4OcMx
Nordkorea Raketentest Miloitärmanöver USA und Südkorea
Picha: Gray Gibson/U.S. Navy/ABACAPRESS/picture alliance

Viongozi wa Marekani, Uingereza na Australia,wapo katika hatua ya kuzindua mipango ya kuipa Australia nyambizi zinazoendeshwa kwa nguvu ya nishati ya nyuklia, katika jitihada kubwa dhidi ya kukabiliana na kitisho China katika eneo la ukanda wa India na Pasifiki.

Rais wa Marekani Joe Biden, Waziri Mkuu wa Australia Anytony Albanese na Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak, wataridhia maelezo ya mpango wa kiusalama uliopewa jina la AUKUS, ambao kwa mara ya mwanzo ulitangazwa mwaka 2021, kwenye kambi ya kijeshi ya wanamaji ya San Diego Califonia.

Chini ya makubaliano hayo, Australia itanunua nyambizi tatu za nyuklia mwanzoni mwa miaka ya 2030, ikiwa na chaguo ka kununu nyingine mbili ikiwa itahitajika, wamesema maafisa wa Marekani.

Makubaliano ya AUKUS, yatakuwa na hatua kadhaa, ambapo kutakuwa na angalau nyambizi moja ya Marekani itakayotembelea bandari za Australia katika miaka ijayo na hatimae kumalizika mwishoni mwa miaka ya 2030 kwa toleo jipya la nyambizi zinazojengwa kwa usanifu wa Uingereza na teknolojia ya Marekani.

Mafunzo kwa wanajeshi wa Australia

Mkataba huo pia utahusisha jeshi la Marekani na Uingereza kupelekwa Magharibi mwa Australia, kusaidia kuwafundisha maafisa wa Kiaustralia masuala ya kiusalama. Hatua ya serikali ya kuimarisha shughuli za kijeshi katika Bahari ya Kusini mwa China, ambayo inasema ni sehemu yake licha ya sheria ya kimataifa ya bahari inayosema sehemu hiyo ni ya Vietnam, Malaysia, Ufilipino na nchi nyingine, imezidi kuongeza mvutano kati yake na Marekani.

US Couple Accused Of Selling Nuclear Submarine Secrets
Nyambizi ya jeshi la majini la MarekaniPicha: abaca/picture alliance

Marekani ilikuwa na shabaha ya kuanza upelekaji huu wa zamu kwa kutuma nyambizi moja katika eneo la Magharibi mwa Australia, kuanzia mwaka 2027 na katika kipindi cha miaka michache, ilikuwa inatarajiwa kuhusisha nyambizi nne za Marekani na moja ya Uingereza.

Marekani kushiriki tena mipango ya silaha za nyukilia tangu miaka ya 1950

Makubaliano ya AUKUS, yataakisi hatua ya mwanzo kwa Marekani kushiriki teknolojia ya nyuklia nje ya mipaka yake tangu miaka ya 1950, pale iliposhirikiana na Uingereza. Kwa sasa hakuna nchi mwanachama wa mkataba wa kuzuwia kuenea kwa silaha za nyuklia, NPT, iliyo na nyambizi za nyuklia, mbali ya mataifa ambayo mktaba huo unayatambua kama mataifa ya nyuklia, - ambayo ni Marekani, Urusi, China, Uingereza na Ufaransa.

Soma zaidi:QUAD lina hofu ya shughuli za kijeshi katika bahari ya China

China imeukosoa mpango wa AUKUS kama kitendo haramu cha kueneza silaha za nyuklia duniani. Na katika kuuzindua mpango huo, Australia pia iliikasirisha Ufaransa kwa kukatisha ghafla makubaliano ya kununua nyambizi za kawaida za Ufaransa.

Chanzo: RTR