1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Biden na Xi wahimiza mahusiano thabiti ya Marekani na China

16 Novemba 2021

Rais wa Marekani Joe Biden amezungumza kwa njia ya vidio na mwenzake wa China Xi Jinping, katika mkutano ambao viongozi wote wawili wamesema unalenga kupunguza mivutano isiyo ya lazima baina ya madola hayo yenye nguvu.

https://p.dw.com/p/432vp
USA I US-Präsident Biden spricht virtuell mit dem chinesischen Staatschef Xi
Rais Joe Biden na Xi Jinping wamezungumza kwa njia vidio Picha: Jonathan Ernst/REUTERS

Mkutano huo uliosubiriwa kwa hamu ulifunguliwa kwa viongozi hao wawili kupungiana mkono baada ya kuonana kupitia televisheni katika kile mtu angeweza kukifananiasha na mikutano mingine kwa njia ya video ambayo imekuwa ya kawaida tangu kuzuka kwa janga la Corona.

Akizungumza kutoka ikulu ya White House mjini Washington, rais Joe Biden amemweleza mwenzake wa China Xi Jinping kuwa wanapaswa kuhakikisha kwa kila njia ushindani kati ya mataifa hayo mawili haugeki kuwa uhasama.

Rais Biden ambaye aliambatana na maafisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Marekani akiwemo waziri wake wa mambo ya kigeni Antony Blinken, yule wa fedha Janet Yellen na mshauri wa taifa wa masuala ya usalama Jake Sullivan amesema anatumai atakuwa na mazungumzo ya kirafiki na ya dhati na rais Xi.

Kwa upande wake rais wa Xi Jinping amemrai rais Biden kuwa pande hizo mbili zinahitaji kuimarisha mawasiliano.

"Niko tayari kufanya kazi nawe ndugu rais, kujenga maridhiano na kuyaelekeza mahusiano kati ya China na Marekani katika njia sahihi" amesema rais Xi, ambaye amemtaja Biden kuwa "rafiki wa muda mrefu".

Marekani yasema ni mkutano wa kuihimiza China kuheshimu kanuni za kimataifa 

Kabla ya mkutano wa leo viongozi hao wawili walikwishazungumza kwa njia ya simu mara mbili tangu Biden alipoingia madarakani mnamo mwezi Januari.

China | Präsident Xi Jinping und Joe Biden
Viongozi hao wawili wamewahi kukutana ana kwa ana wakati Joe Biden alipokuwa makamu wa rais wa MarekaniPicha: Lintao Zhang/AP Images/picture alliance

Ikulu ya Marekani imesema Biden alitamani kukutana ana kwa ana na rais Xi, lakini kiongozi huyo wa China hajasafiri ne ya taifa lake tangu kuzuka kwa janga la corona na kwa hivyo mkutano wa njia ya video ndiyo ilikuwa chaguo pekee kwa mazungumzo baina yao.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Jen Psaki alisema rais Biden anashiriki mkutano huo utakaoendelea kwa saa kadhaa akiwa upande madhubuti baada ya miezi kadhaa ya kuimarisha mshikamano na washirika wake juu ya kuikabili China.

Amesema mkutano huo ni "nafasi muhimu ya kujenga misingi na masharti ya ushindani na China" lakini ni sharti taifa hilo la mashariki ya mbali liheshimu kanuni za kimataifa.

Taiwan kutawala ajenda ya mazungumzo kati viongozi hao 

Maafisa wa China kwa upande wao wamesema Taiwan ndiyo itakuwa ajenda kuu ya mazungumzo hayo kati ya Biden na Xi. Mivutano imeongezeka kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kijeshi za China kwenye anga la kisiwa hicho ambacho Beijingi itadai kuwa sehemu ya himaya yake.

China USA Treffen Joe Biden bei Xi Jinping in Peking
Suala la Taiwan ni ajenda muhimu ya mazungumzo ya Xi na Biden Picha: Reuters

Washington ambayo inaiunga mkono serikali ya kidemokrasia ya Taiwan imekwishaonesha nia na msimamo wa kutumia ushawishi wake kuilinda dhidi kitisho cha uvamizi au hujuma kutoka Beijing.

Masuala ya biashara na rikodi ya haki za binadamu nchini China ni miongoni mwa masuala mengine yatakayozungumziwa kwenye mkutano huo wa leo unaofanyika katika wakati mahusiano kati ya madola hayo mawili yenye nguvu yamepwaya hadi kiwango cha chini kabisa.