1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blatter akabiliwa na mtihani mgumu wiki hii

Admin.WagnerD28 Septemba 2015

Utawala wa rais wa shirikisho la kandanda duniani FIFA Sepp Blatter unaweza kufikia mwisho wiki hii wakati kashfa ya rushwa dhidi ya shirikisho hilo ikitishia kumporomosha kiongozi huyo kutoka katika medani ya michezo.

https://p.dw.com/p/1GesT
Schweiz Sepp Blatter wird bei Pressekonferenz mit Geldscheinen beworfen
Kiongozi wa FIFA Joseph Sepp BlatterPicha: Reuters/A. Wiegmann

Blatter mwenye umri wa miaka 79 ambaye anatarajiwa kujiuzulu mwezi Februari mwaka ujao, lakini kwa kuwekwa chini ya uchunguzi wa kihalifu na maafisa wa Uswisi, mwisho wake unaweza kuja mapema zaidi.

Duru zinadokeza kwamba huenda akashawishika kujiuzulu mara moja.

Msemaji wa tume ya maadili ya FIFA Andreas Bantel ameliambia shirika la habari la AFP hawezi kueleza lolote kuhusiana na shauri hilo la mtu binafsi, na amekataa kuthibitisha ripoti kwamba kamati imeanzisha uchunguzi dhidi ya Blatter pamoja na rais wa shirikisho löa kandanda barani Ulaya UEFA Michel Platini, ambaye anawania kiti cha uongozi wa shirikisho hilo.

Schweiz, Sepp Blatter auf Pressekonferenz
Kiongozi wa shirikisho la FIFA Sepp BlatterPicha: Getty Images/P. Schmidli

Lakini amesisitiza kwamba ,"iwapo kuna shaka, kamati ya maadili itawasilisha hatua rasmi za kuchukuliwa.

"Sheria ni kwa kila mtu katika soka , bila kujali nafasi yake ama jina lake." Wachunguzi wa Uswisi waliingia katika makao makuu ya FIFA siku ya Ijumaa wakati wakiwalenga Blatter na Platini.

Maafisa wamesema uchunguzi wa kihalifu umeanzishwa dhidi ya Blatter kwa shaka ya kuhusika katika ubadhirifu wa kihalifu, wakati Platini anachunguzwa kuhusiana na malipo aliyotumbukiziwa katika akauti yake ya mamilioni ya dola.

Kipchoge ashinda mbio za Berlin Marathon

Eliud Kipchoge wa Kenya ameshinda Berlin Marathon jana Jumapili kwa kutumia masaa mawili, dakika 4, ikiwa ni mbio alizokimbia kwa kasi kubwa mwaka huu.

42. Berlin-Marathon Eliud Kipchoge
Eliud Kipchoge katika hatua ya mwisho ya Berlin MarathonPicha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Mshindi huyo wa London Marathon mwaka huu, sasa ameshinda mara tano kati ya Marathon sita alizoshiriki , nne zikiwa mfululizo, ikiwa ni pamoja na Chicago Marathon na Rotterdam ya Uholanzi.

Hata hivyo Kipchoge , ambaye ni bingwa wa dunia wa mbio za mita 5,000 mwaka 2003, hakuweza kukuifikia rekodi ya dunia iliyowekwa mjini Berlin mwaka jana. Eliud alipata matatizo katika soli ya ndani ya kiatu chake muda mfupi baada ya kuanza kukimbia , hali ambayo huenda ilimkwaza kukimbia kwa kasi zaidi.

Eliud Kipchoge amesema hata hivyo amefurahishwa na ushindi huo:

"Ninafurahi kushinda tena katika ardhi ya Ujerumani. Huu ni ushindi wangu wa pili hapa. Na nafikiri Ujerumani inanipenda. Nilipata matatizo katika kiatu, hata kabla ya kufikia kilometa moja."

Mshindi wa pili kwa wanaume alikuwa Mkenya pia Eliud Kiptanui akifuatiwa na Emmanuel Mutai na Muethiopia Fiyesa Lilesa.

Kwa upande wa wanawake Gladys Cheromo alinyakua taji hilo akikimbia kwa saa 2 dakika 19, na sekunde 25 akifuatiwa na Ethians Aberu Kebede wa Ethiopia mshindi wa Berlin Marathon mwaka 2012 na kisha Meseret Hailu katika nafasi ya tatu kutoka Ethiopia pia.

Bundesliga; Robert Lewandowski atisha

Ligi ya Ujerumani ilitimua vumbi tena mwishoni mwa juma ambapo mabingwa watetezi Bayern Munich walijipatia ushindi wao wa saba katika michezo saba bila kutoka jasho , wakati Robert Lewandowski akiweka rekodi mara mbili katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mainz 05 na kujitenga na kundi lote la timu za Bundesliga kwa pointi nne kileleni.

Fußball Bundesliga 1 FSV Mainz 05 - FC Bayern München
Robert Lewandowski akishangiria bao la 100 katika BundesligaPicha: Getty Images/Bongarts/S. Hofmann

Mshambuliaji wa Dortmund Pierre Emerick Aubameyang alipachika mabao mawili na kuwa mchezaji wa kwanza kufunga katika kila mchezo katika michezo saba ya mwanzo ya ligi ya Ujerumani Bundesliga katika msimu mmoja lakini bao la dakika ya 90 la kusawazisha liliipa Darmstadt sare isiyotarajiwa ya mabao 2-2. Sare hiyo sawa na ushindi ilikuwa furaha kubwa kwa mashabiki na wachezaji wa Darmstadt kama anavyosimulia hapa nahodha wao Aytac Sulu.

"Kwa michezo iliyobaki ya msimu huu hii ina maana kwamba chechefu tunahitaji pointi 30. Iwapo tunataka kuendeleza msimamo wetu katika ligi. Ni muhimu kwetu , kwamba kila mchezo unamalizika hivi, na kwamba tunataka kushinda. Wakati tukipata pointi moja ni vizuri, kwakuwa tunaposhinda pia inakuwa vizuri. Na iwapo tutashindwa, tutaangalia mchezo wenyewe na kusema ,lakini tumejitahidi kadri ya uwezo wetu."

Fußball Bundesliga 4. Spieltag Hannover 96 - Borussia Dortmund
Pierre-Emerick Aubameyang wa Dortmund akishangiria baoPicha: Getty Images/AFP/R. Hartmann

Lakini upande wa Borussia Dortmund, ilikuwa ni kidonge kichungu kwao kutoka sare na timu hiyo iliyopanda daraja msimu huu na katika mchezo huo , ilitawala katika kila eneo kwa muda mrefu, lakini magoli ya kutosha ushindi hayakupatikana, kama anavyoeleza mchezaji wa kati wa Borussia Ilkay Gündogan.

"Kwetu sisi ni uchungu sana, kwasababu katika kipindi cha pili tulizawadiwa kutokana na mchezo mzuri sana. Darmstadt walilinda goli lao tu na walifanya vizuri , kwa uwezo wao wote waliweza kulinda lango lao. Katika kipindi cha kwanza hatukuweza kupata njia ya kutatua tatizo hilo, katika kipindi cha pili tulicheza vizuri lakini tulipoteza ushindi kwa goli la kijinga , ambapo wote tulijipanga kijinga na kupoteza ushindi."

Schalke 04 imesogea hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Hamburg SV , nayo Wolfsburg ikiwa katika nafasi ya nne ilitoshana sare na Hannover 96 kwa kufungana bao 1-1.

Bayer Leverkusen inashikilia nafasi ya tano , baada ya kuizaba Werder Bremen kwa mabao 3-0.

Manchester United yaingia kileleni mara ya kwanza msimu huu

Katika Premier League ya Uingereza , Manchester United imechukua nafasi ya majirani zao Manchester City baada ya kuishinda Sunderland kirahisi kwa mabao 3-0. City iliangukia pua baada ya kutandikwa mabao 4-1 na Tottenham Hot Spurs.

Großbritannien Manchester United Trainer Louis Van Gaal
Kocha wa manchester United Louis Van GaalPicha: picture-alliance/dpa/N. Roddis

West Ham United inashikilia nafasi ya tatu baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Norwich City, ikiwa sawa kwa pointi na Arsenal. Kocha wa West Ham United Slaven Bilic hata hivyo amesema timu yake sio sehemu ya vigogo katika Premier League licha ya mwanzo mzuri msimu huu.

La Liga , Barca itamkosa Messi kwa mwezi mzima

Villareal kwa mshangao mkubwa inaongoza ligi ya Uhispania baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Atletico Madrid na Real Madrid imeambulia pointi moja baada ya kutoka sare bila kufungana na Malaga.

Ushindi wa mabao 2-1 wa Barcelona dhidi ya Las Palmas umekuja na gharama kubwa wakati Lionel Messi alitoka nje baada ya kupata maumivu ya goti na hatakuwamo katika kikosi cha Barca kitakachoingia katika uwanja wa Bayer Arena kesho Jumanne kupambana na Bayer Leverkusen katika Champions League.

Wakati huo huo Marc-Andre ter Stegen mlinda mlango wa Barcelona kutoka Ujerumani ataingia katika kurunzi kesho usiku dhidi ya Bayer Leverkusen katika Champions League.

Fussball U21 Deutschland gegen Dänemark
Mlinda mlango wa Barcelona , Marc Andre ter StegenPicha: M. Rose/Bongarts/Getty Images

Mabingwa hao wa Ulaya Barcelona hawatafakari tu vipi watafanya uwanjani bila jogoo wao Lionel Messi katika mchezo wa kesho lakini pia bila mlinda mlango wao Claudio Bravo.

Ter Stegen atakaa langoni kuwazuwia washambuliaji wa Leverkusen wenye uchu wa kuzifumania nyavu, huku akiwa ameruhusu magoli 16 katika michezo saba msimu huu.

Dinamo Zagreb itabidi kutafuta njia ya kumzuwia mshambuliaji hatari wa Bayern Munich Robert Lewandowski wakati watakaowasili mjini Munich kuikabili Bayern Munich katika mchezo wa pili wa kundi F katika Champions League kesho Jumanne.

Kikosi cha kocha Pep Guardiola kinaogelea katika bahari ya ushindi mara tisa katika michuano yote kinayoshiriki wakati Lewandowski kwa hivi sasa akionekana kuwa hawezi kuzuiwa kuzifumania nyavu za adui.

Kocha wa Chelsea Jose Mourihno anarejea katika uwanja wa nyumbani Stadio do Dragao na timu yake ya zamani Porto, ambapo mlinda mlango wa Porto Iker Casillas na kocha huyo walikuwa hawana uhusiano mzuri wakati wakiwa Real Madrid. Lakini baada ya kuondoka Mourinho , Casillas alifanikiwa kukiongoza kikosi cha Real Madrid kupata ushindi katika fainali ya mwaka 2014 ya Champions League, na kupata medali yake ya tatu ya ubingwa wa taji hilo.

England Chelsea Meister Jubel
Kocha wa Chelsea Jose MourinhoPicha: Reuters/Sibley Livepic

Yanga na Simba

Huko nchini Tanzania, pambano la watani wa jadi Simba na Yanga , lililkuwa kivutio kikubwa mwishoni mwa juma. Baada ya wiki kadhaa za heka heka za kisiasa hatimaye, mashabiki na wanachama wa vyama vya siasa waligeukia upande wa michezo, mahasimu wa kisiasa wakiungana na marafiki kutofautiana katika uwanja wa kandanda. Hatimaye hali ilitulia siku ya Jumamosi jioni wakati Dar Young Africans ilipoibuka kidedea kwa kuikandika Simba kwa mabao 2-0 na kutulizaliza mzuka wa wana Msimbazi SSC, Simba Sports Club ambayo kwa kipigo hicho inashika sasa nafasi ya nne katika msimamo wa ligi.

Mlinda mlango wa Liberia apata ajali

Mlinda mlango wa Liberia Nathaniel Sherman anaelekea kuliacha soka na mapema baada ya kupata ajali na kuumiza jicho lake wakati alipojipiga katika dirisha katika hoteli waliyofikizia kabla ya pambano la kufuzu kucheza katika fainali za kombe la mataifa ya Afrika mwezi uliopita.

Sherman ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba ajali hiyo imesababisha kioo kuingia katika jicho lake. Amesema kwa sasa hawezi kuona, lakini ana matumaini ya kupona baada ya kufanyiwa upasuaji nchini India. Ajali hiyo ilitokea siku chache kabla ya ushindi wa kushitua dhidi ya Tunisia wa bao 1-0 Septemba 5 katika mchezo wa kufuzu kucheza katika fainali za mwaka 2017 za mataifa ya Afrika.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / ape / afpe / dpa

Mhariri: Mohammed Abdul- Rahman